Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawasihi wadau katika mgogoro wa Ukanda wa Caucasus kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi ili kupata suluhu ya kudumu badala ya kutumia nguvu za kijeshi. Baba Mtakatifu Francisko anawasihi wadau katika mgogoro wa Ukanda wa Caucasus kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi ili kupata suluhu ya kudumu badala ya kutumia nguvu za kijeshi. 

Machafuko ya Kisiasa Ukanda wa Caucasus: Majadiliano Ni Muhimu!

Baba Mtakatifu Francisko ameombea amani katika Ukanda wa Caucasus na kuwasihi wadau wote wanaohusika katika mgogoro huu kutekeleza kwa vitendo na udugu wa kibinadamu mambo msingi yatakayosaidia kupata suluhu ya kudumu katika mgogoro huu. Kamwe wasitumie nguvu wala silaha za vita, bali njia muafaka ni mazungumzo na majadiliano katika ukweli na uwazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 27 Septembe 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alionesha masikitiko yake makubwa kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza kwenye Ukanda wa Caucasus, eneo linaloundwa na Georgia, Armenia na Azerbaijan. Baba Mtakatifu ameombea amani katika Ukanda huu na kuwasihi wadau wote wanaohusika katika mgogoro huu kutekeleza kwa vitendo na udugu wa kibinadamu mambo msingi yatakayosaidia kupata suluhu ya kudumu katika mgogoro huu. Kamwe wasitumie nguvu wala silaha za vita, bali njia muafaka ni mazungumzo na majadiliano katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ukimya kwa ajili ya kuombea amani Ukanda wa Caucasus.

Jumamosi, tarehe 26 Septemba 2020, Kardinali Crescenzio Sepe, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Napoli, Kusini mwa Italia, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza mtumishi wa Mungu Sr. Maria Luigia Pascale wa Ekaristi Takatifu, ambaye hapo awali alijulikana kama Maria Velotti, Muasisi wa Shirika la Watawa wa Mtakatifu Francisko Waabuduo Msalaba Mtakatifu, kuwa Mwenyeheri. Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii mpya ya Mwenyeheri. Ni mfano bora wa kuigwa katika kutafakari Fumbo la Njia ya Msalaba na Injili ya upendo inayomwilishwa katika upendo kwa Mungu na jirani.

Papa: Vita

 

28 September 2020, 15:31