Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika mzunguko mpya wa katekesi unaoongozwa na kauli mbiu uponyaji wa ulimwengu, jumatano tarehe 2 Septemba 2020 amezungumzia kuhusu: Mshikamano na Imani. Baba Mtakatifu Francisko katika mzunguko mpya wa katekesi unaoongozwa na kauli mbiu uponyaji wa ulimwengu, jumatano tarehe 2 Septemba 2020 amezungumzia kuhusu: Mshikamano na Imani.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Uponyaji wa Ulimwengu: Mshikamano na Imani

Kanuni za kudumu kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa zinakita mizizi yake katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Mafao kwa wote, auni, na mshikamano. Mshikamano unatoa mwanga wa mafungamano ya maumbile ya kijamii kwa kukazia usawa, heshima, haki na watu kujisadaka katika ujenzi wa umoja unaofumbatwa katika kanuni maadili, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiunga pamoja naye, ili kutafakari kuhusu janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kuangalia madhara yake, mintarafu magonjwa ya kijamii. Tafakari hii makini, inaongozwa na Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii ni nafasi muafaka ya kutumia Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuisaidia familia ya binadamu kuweza kuganga na kuponya ulimwengu huu unaoteseka kutokana na magonjwa makubwa na mazito! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa pamoja, wataweza kushiriki tafakari hii kama wafuasi wa Kristo Yesu anayeganga na kuponya, ili kujenga ulimwengu bora zaidi unaosimikwa katika matumaini kwa ajili ya kizazi cha sasa na vile vijavyo. Baba Mtakatifu katika mzunguko mpya wa katekesi unaongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 2 Septemba 2020, kwenye Uwanja wa Jengo la Mtakatifu Damas lililoko mjini Vatican, katekesi iliyofanyika mubashara kwa ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbalimbali za dunia, amejielekeza zaidi katika mshikamano unaoratibiwa na fadhila ya imani.

Kanuni za kudumu kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa zinakita mizizi yake katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Mafao kwa wote, auni, na mshikamano. Hizi ni kanuni zinazojaribu kujibu kadiri ya mahitaji ya nyakati sanjari na hatua za maendeleo ya jamii. Mshikamano unatoa mwanga wa mafungamano ya maumbile ya kijamii kwa kukazia usawa, heshima, haki na watu kujisadaka bila ya kujibakiza katika ujenzi wa umoja unaofumbatwa katika kanuni maadili, ustawi na mafao ya wengi.  Katekesi ni utaratibu wa mafundisho ya Kanisa katika ukamilifu, kwa nia ya kuwatayarisha waamini kwa maisha kamili mintarafu mwanga wa Injili. Baba Mtakatifu anasema janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limeonesha kwamba, binadamu wote ni sawa, wanahitajiana na kukamilishana wanapokabiliana na wema au ubaya. Kumbe, kuna haja ya kushirikiana kwa dhati ili kuweza hatimaye, kuvuka salama salimini kutoka katika janga la Virusi vya Corona, COVID-19 kwa njia ya mshikamano. Hii inatokana na ukweli kwamba, binadamu wote wana asili moja inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu; binadamu wote wanaishi hapa duniani, bustani safi ambayo Mwenyezi Mungu amemtengenezea mwanadamu na kwamba, wote wamekombolewa kwa njia ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, pale, binadamu anaposahau tunu hizi msingi katika maisha yake ule uwezo wake wa kutegemeana na kukamilishana unageuka na kuwa ni hali ya kuwategemea wengine, jambo linalosababisha ukosefu wa usawa kijamii na hivyo kupelekea pengo kubwa kati ya maskini na matajiri. Huo ndio mwanzo wa baadhi ya watu kusukumizwa pembezoni mwa jamii na hivyo kudhohofisha mshikamano na mafungamano ya kijamii sanjari na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, anakazia kuhusu mwingiliano na umuhimu wa kuishi katika ulimwengu ambao kwa sasa “umegeuka na kuwa kama kijiji, lakini kwa kushindwa kunafsisha mwingiliano huu katika mshikamano. Haya yote ni matokeo ya uchoyo na ubinafsi wa kitaifa, makundi yenye nguvu pamoja na itikadi kali zinazoendelea kuzalisha miundo mbinu ya dhambi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, neno “Mshikamano” wakati mwingine limepewa tafsiri potofu, kwa kuchakachuliwa kiasi cha kueleweka vibaya. Kimsingi linataja kitu ambacho ni zaidi ya matendo machache ya ukarimu wa hapa na pale kwani hii ni sehemu ya haki na usawa wa hadhi kama binadamu. Hiki ni kielelezo cha urafiki, mapendo na hitaji la lazima la udugu wa kibinadamu na wa Kikristo. Unaoneshwa mahali pa kwanza kwa mgawanyo wa mali na malipo ya kazi. Mshikamano wa Kimataifa ni hitaji la utaratibu wa maadili ili kudumisha amani ulimwenguni. Nguvu ya mshikamano inavuka mali na vitu vinavyoonekana, kwa kueneza mema ya kiroho ya imani. Ili kweli mafungamano ya kijamii yaweze kuwa ni kielelezo cha mshikamano na hatimaye kuzaa matunda yanayotarajiwa, kuna haja kwa mshikamano kukita mizizi yake katika maisha ya mwanadamu na katika kazi ya uumbaji, kwa kuwaheshimu binadamu pamoja na mazingira. Baba Mtakatufu anaendelea kuwapongeza wavuvi wanaojitolea kuvua taka za plastiki badala ya samaki, ili kuboresha mazingira nchini Italia. Hawa ni wavuvi kutoka eneo la “San Benedetto del Tronto”.

Tangu mwanzo, Maandiko Matakatifu yamegusia kuhusu Mnara wa Babeli, jinsi watu walivyokuwa na lugha moja, lakini kwa kiburi wakataka kujijengea mji na mnara na kilele chake kifike mbinguni ili wajifanyie jina na wala wasitawanyike usoni pa nchi yote, lakini matokeo yake, “wakakiona cha mtema kuni”, Bwana akaichafua lugha ya dunia yote na watu wakatawanyika usoni pa nchi yote. Hii ndiyo jeuri ya binadamu aliyetaka kujijengea jina hadi kufika mbinguni na kusahau umuhimu wa mshikamano na mafungamano ya kibinadamu; mshikamano na kazi ya uumbaji pamoja na Mwenyezi Mungu Muumbaji wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Binadamu “alitia nia” ya kutaka kujenga mnara na kilele chake kifike mbinguni, lakini matokeo yake, akaisambaratisha jumuiya. Watu wanataka kuunganisha miundo mbinu ili kukuza umoja; wanataka kuunganisha lugha, ili waelewane, lakini matokeo yake ni madhara makubwa katika utamaduni. Binadamu anataka kuwa ni mmiliki wa Dunia mama, lakini matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa bayianuai na ukosefu wa usawa wa kiekolojia.

Ni katika muktadha huu, vitu na mali vinapewa kipaumbele cha kwanza kiasi kwamba, maisha ya binadamu si mali kitu. Kuna simulizi la kale linaonesha kwamba, matofali yalikuwa na thamani kubwa sana kuliko hata maisha ya binadamu. Hawa walikuwa ni watumwa waliotumikishwa sana, utu, heshima na haki zao msingi hazikuwa ni mali kitu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Leo hii fedha ina thamani kubwa sana kuliko hata maisha ya binadamu. Thamani ya fedha inaposhuka kwenye Soko la Fedha Kimataifa, hii ni habari inayopewa kipaumbele cha kwanza kwenye vyombo vikuu vya habari duniani. Lakini kuna mamilioni ya watu wanaopekenywa na umaskini na baa la njaa duniani, lakini hii si habari yenye mvuto na mashiko anasema Baba Mtakatifu Francisko. Pentekoste ni kinyume kabisa cha Mnara wa Babeli. Siku ile ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Jumuiya ya Mitume iliyokuwa imejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, ikapokea nguvu ya Mungu kutoka juu, ikawasukuma kutoka ndani, tayari kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ni Bwana.

Roho Mtakatifu anawajalia waamini kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na utulivu katika utofauti. Roho Mtakatifu ni nguvu inayowaunganisha watu wa Mungu. Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa ujenzi wa Jumuiya ya waamini. Mtakatifu Francisko wa Assisi akiwa amevuviwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, alivipatia viumbe vyote majina ya kaka na dada. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, katika Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, aliwakirimia zawadi ya imani; Jumuiya ikaunganika katika umoja, utofauti na mshikamano. Huu ni utofauti unaosimikwa katika msingi wa mshikamano, kwa kutambua uwepo na mchango wa pekee kutoka kwa kila mtu, ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kamwe zawadi hii haiwezi kufifishwa na uchoyo wala ubinafsi. Utofauti unaosimikwa katika mshikamano wa upendo ni dawa mchunguti inayoweza kuganga na kuponya miundombinu na michakato yote ya kijamii ambayo imeibua mifumo ya ukosefu wa usawa kunakochochewa na mifumo mbalimbali ya unyonyaji, ukandamizaji, rushwa na ufisadi.

Kumbe, mshikamano ni njia pekee inayopaswa kutumiwa na watu wa Mungu baada ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVId-19. Hii ni njia inayoganga na kuponya magonjwa kati ya mtu na mtu pamoja na magonjwa ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mshikamano ukiwa unaongozwa na imani unawawezesha waamini kunafsisha upendo wa Mungu katika utamaduni wa utandawazi, kwa kujenga na kudumisha madaraja ya kuwakutanisha watu badala ya kuta zinazowatenganisha na madaraja yanayoporomoka utadhani ni matofali ya “barafu inayoyeyuka”. Mshikamano unaoongozwa na kuratibiwa na imani ni sementi ya mafungamano ya jumuiya inayoenzi mchakato wa ukuaji makini na thabiti wa kiutu! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Katekesi yake kwa kusema kwamba, katika kipeo na dhoruba kali za maisha, Kristo anawataka wafuasi wake, kuamka na kuanza kujenga mshikamano wa upendo unaoratibiwa na fadhila ya imani; kwa kusikiliza na kutenda, ili kuenzi juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanyika ili kumwokoa mwanadamu anayeonekana kuzama kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa njia ya kipaji cha ugunduzi, zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu, awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga mifumo mipya itakowawezesha kudumisha mafungamano yanayokita mizizi yake katika ukarimu unaorutubisha udugu wa kibinadamu na mshikamano wa dhati!

Papa: Katekesi

 

02 September 2020, 14:53