Tafuta

Papa Francisko amefafanua kuhusu dhamana na utume wa waandishi wa habari Wakristo duniani: Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayoleta imani na matumaini. Papa Francisko amefafanua kuhusu dhamana na utume wa waandishi wa habari Wakristo duniani: Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayoleta imani na matumaini. 

Papa: Dhamana na Utume wa Wanahabari Wakristo Duniani!

Papa anasema, vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa vinapaswa kusaidia makuzi ya Jumuiya za Kikristo, ili ziweze kujielekeza zaidi katika mtindo bora zaidi wa maisha, unaowajumuisha na kuwashirikisha watu wote pasi na ubaguzi au kwa kuathirika na maamuzi mbele. Inasikitisha kuona kwamba, watu wanajikita zaidi katika tabia ya kupika majungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume “Tertio Millennio Adveniente”: Yaani “Maandalizi ya Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo! Alisema kwamba, Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo, umuhimu wa Ukristo na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo. Maandalizi ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo katika maisha na utume wa Kanisa. Maandalizi ya Jubilei hatua kwa hatua kwa kutambua umuhimu wa Jubilei ya Miaka 200 ya Ukristo katika historia ya maisha ya mwanadamu. Ni muda wa kushukuru, kufurahia, kufanya toba na kuomba msamaha; kwa kujenga na kudumisha umoja wa Wakristo unaofumbatwa katika ushuhuda na uekumene wa damu ili kuweza kumtafakari Kristo Yesu, Roho Mtakatifu na hatimaye, Mungu Baba Mwenyezi na hatimaye, kulipatia Fumbo la Utatu Mtakatifu, sifa, utukufu na heshima kwa sababu Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume “Tertio Millennio Adveniente”, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo, alijielekeza zaidi katika kuwaandaa watu wa Mungu ili kuweza kumpokea Kristo Yesu na ujumbe wake unaokoa. Ujumbe huu, ni kiini na chemchemi ya matumaini na mwaliko kwa Kanisa kupaaza sauti yake, kwa kuwawezesha wakristo kutumia vyema vipaji na akili zao kuchangia katika maboresho ya ulimwengu wanamoishi, kwa njia ya tafakari makini zinazojenga. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanatafuta na kudumisha yale mema na mazuri yanayopatikana kutoka kwa watu na hivyo “kufyekelea” mbali maamuzi mbele. Na badala yake ni kuendelea kutoa kipaumbele cha kwanza utamaduni wa watu kukutana, hali inayowawezesha kuufahamu ukweli wa mambo, huku wakiwa na mwelekeo wenye matumaini makubwa! Vyombo vya mawasiliajo ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa vina wajibu wa kutoa habari makini zaidi mintarafu maisha na utume wa Kanisa sanjari na ujenzi wa dhamiri nyofu.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo ni tukio ambalo limeacha alama ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, Jarida la Kikristo linalochapishwa mara moja kwa juma nchini Ubelgiji linalojulikana kama “Tertio” lilianzishwa na kwa sasa linaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Ni katika mkutadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 18 Septemba 2020 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Jarida la “Tertio” kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Katika ulimwengu mamboleo, habari imekuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha ya kila siku. Habari hizi zikiwa zimeandaliwa kwa ubora na umakini mkubwa zinawasaidia watu wa Mungu kuweza kutambua matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika jamii inayowazunguka. Huu ni mwaliko kwa kila mtu na jamii katika ujumla wake kufanya upembuzi yakinifu mintarafu tabia na mwenendo wa mtu binafsi, ndugu na jamii husika, tayari kushiriki katika mchakato wa kuunda dhamiri nyofu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa vinapaswa kusaidia malezi na makuzi ya Jumuiya za Kikristo, ili ziweze kujielekeza zaidi katika mtindo bora zaidi wa maisha, unaowajumuisha na kuwashirikisha watu wote pasi na ubaguzi au kwa kuathirika na maamuzi mbele. Inasikitisha kuona kwamba, watu wanajikita zaidi katika tabia ya kupika majungu. Ikumbukwe kwamba, "wambea hawana bunge na wala umbea si mtaji na kama ungekuwa mtaji wangetajirika wengi”. Umbea unafunga nyoyo za Jumuiya na umoja wa Kanisa. Shetani, Ibilisi ni mpiga majungu nambari moja, anayetembea hapa na pale akipepeta mdomo kwa kuzungumza mabaya ya watu wengine, kwa sababu ni mwongo anayetaka kupandikiza mbegu ya utengano ndani ya Kanisa, kwa kuwasambaratisha ndugu ili wasijenge Jumuiya.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mawasiliano ni utume muhimu sana katika maisha ya Kanisa. Wakristo wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika nyanja za mawasiliano ya jamii wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Injili. Kwa weledi wake, mwanahabari Mkristo anapaswa kutoa ushuhuda uliopyaishwa katika ulimwengu wa mawasiliano bila kufika ukweli wala kuchakachua habari. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao ukweli wa historia ya Habari Njema ya Wokovu. Hizi ni historia zinazowajenga watu badala ya kuwaporomosha; zinawasaidia watu kugundua asili yao na nguvu zinazohitajika ili kusonga mbele. Hata katika makelele na ujumbe mwingi, bado kunahitajika historia ya binadamu inayomzungumzia binadamu mwenyewe na uzuri unaomzunguka. Ni historia inayouangalia ulimwengu sanjari na yote yanayoendelea kutendeka kwa jicho jema.

Ni simulizi inayoweza kumwonesha mwanadamu kuwa ni sehemu ya maisha na kwamba, wanategemeana. Kimsingi, hili ni simulizi ambalo linawafunulia watu mwingiliano na mafungamano yanayowaunganisha kwa pamoja. Baba Mtakatifu Francisko anawaambia Wanahabari Wakristo kwamba,  wao ni wadau wakuu katika kutamba hadithi hizi. Mawasiliano yanapaswa kuwa ni chemchemi ya imani na matumaini kwa siku za usoni, ili kuwawezesha watu kuishi leo yao kwa imani na matumaini. Katika kipindi hiki cha janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 waandishi wa habari wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Vyombo vya habari viwasaidie watu wa Mungu kuondokana na upweke hasi, kwa kuwahabarisha, kuwafariji na kuwafurahisha.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari kwa Jarida la “Tertio” kwa ushuhuda wao wa miaka 20, kwani Mama Kanisa anawaangalia kwa imani na matumaini makubwa, kwani wanapaswa kusoma alama za nyakati na kutoa tafsiri nyakati hizi, ili hatimaye, kuonesha dira na utangazaji wa Habari Njema kadiri ya lugha na uelewa watu katika ulimwengu mamboleo. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka waandishi wa habari wa Jarida la “Tertio” kutoka Ubelgiji chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na madaraja ya kuwakutanisha watu na jamii katika ujumla wake. Anamwomba Bikira Maria, ili aweze kuwaombea ili waweze kuwa ni wafuasi waaminifu na wadumifu wa Kristo Yesu. Mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume wadau wote wa Jarida la “Tertio”. kutoka nchini Ubelgiji.

Papa: Mawasiliano
18 September 2020, 16:23