Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa mwezi Septemba 2020 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa mwezi Septemba 2020 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.  (AFP or licensors)

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Septemba 2020: Mazingira Bora!

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Septemba 2020, anawaalika waaamini na watu wote wenye mapenzi mema kuheshimu na kuthamini rasilimali ya dunia, kwa kulinda, kutunza na kuwajibika zaidi. Waamini wajifunze kusali kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira. Watu wanaendelea kuikamua dunia kana kwamba, imegeuka na kuwa kama “kipande cha chungwa”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Jubilei ni muda muafaka wa mapumziko, ili kurejesha tena uhusiano mwema na kazi ya Uumbaji, tayari kuganga na kuponya mafungamano na uhusiano tenge katika maisha ya mwanadamu. Ni muda wa kudumisha uhuru, kusamehe madeni na kuondokana na tabia ya unyonyaji duniani ambayo imesababisha deni kubwa la kiekolojia kutokana na matumizi mabaya ya utajiri na rasilimali za dunia, pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Ni wakati wa kutenda haki, kusamehe madeni makubwa kutoka katika nchi zinazoendelea sanjari na kutambua madhara makubwa yaliyosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mchakato wa ufufuaji na ukuaji wa uchumi uwe ni endelevu na fungamani. Sera, sheria, kanuni na uwekezaji ulenge mafao ya wengi ili malengo ya kijamii kimataifa na utunzaji bora wa mazingira duniani, uweze kufikiwa. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Septemba 2020, anawaalika waaamini na watu wote wenye mapenzi mema kuheshimu na kuthamini rasilimali ya dunia, kwa kulinda na kutunza mazingira kwa kuwajibika zaidi.

Waamini wajifunze kusali kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watu wanaendelea kuikamua dunia kana kwamba, imegeuka na kuwa kama “kipande cha chungwa”. Wafanyabiashara na nchi za Kaskazini mwa dunia, zimeendelea kujitajirisha kwa kunyonya rasilimali na utajiri wa dunia kutoka katika nchi maskini zaidi duniani, kiasi cha kutengeneza “deni la kiekolojia”. Baba Mtakatifu anauliza swali la msingi, Je, ni nani ambaye atakayelilipa deni hili? Deni hili linaendelea kupanuka kutokana na makampuni makubwa ya kimataifa kuendelea “kuchota” rasilimali na utajiri wa Nchi changa duniani, jambo ambalo kamwe wasingalilitenda kwenye nchi zao asilia. Hili ni jambo linaloamsha hasira kali sana! Baba Mtakatifu anasema, leo hii na wala si kesho, watu wanawajibika kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote. Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, unaliwezeshaKanisa kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha na utume wake, daima likisoma alama za nyakati na kujibu kilio cha watu wa Mungu pamoja na Mama Dunia mintarafu mwanga na kweli za Kiinjili.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni wakati muafaka wa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kudhibiti ongezeko la nyuzi joto duniani hadi kufikia nyuzi joto 1.5.C., kama njia ya kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015. Umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unahitajika sana na kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (Cop26) utakaofanyika mjini Glasgow nchini Uingereza. Baba Mtakatifu anasema, bayianuai ni muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya ekolojia. Kumbe, kuna haja ya kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa kwa kulinda asilimia 30% ya dunia kama hifadhi maalum hadi kufikia mwaka 2030, ili kuondokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na kupotea kwa bayianuai. Mkutano wa Kunming, China (Cop15) unapaswa kuwa ni kielelezo makini kitakachoiwezesha dunia  kuwa ni mahali pa binadamu kupata utimilifu wa maisha kadiri ya mapenzi ya Mungu

Ni katika muktadha huu, kuanzia tarehe 1 Septemba 2020 ni Maadhimisho ya Kipindi cha Kazi ya Uumbaji kinachofikia kilele chake hapo tarehe 4 Oktoba 2020, Mama Kanisa anapoadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kudumisha mazingira bora, amani pamoja na kusimamia utu, heshima na haki msingi za maskini. Hiki ni kipindi ambacho Wakristo wanapenda kukitumia kupyaisha imani yao kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuungana kwa ajili ya sala na kazi za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Tangu kuchapishwa kwa Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, hapo tarehe 24 Mei 2015, Siku hii imekuwa ikiadhimishwa na Kanisa Katoliki, kwa kuwa na mwelekeo wa kiekumene.“Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa huru katika nchi yote kwa watu wote waiketio. Itakuwa Jubilei kwenu”. Rej. Law 25: 10.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya VI ya Kuombea Kazi ya Uumbaji kwa Mwaka 2020 anajielekeza zaidi katika Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Maadhimisho ya Siku ya Mama Dunia. Kadiri ya Maandiko Matakatifu, Jubilei ni Kipindi cha kumbukumbu, toba na wongofu wa ndani, muda muafaka wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Baba Mtakatifu anasema, Mama Kanisa anawaalika waja wake kutambua kwamba, hatima ya maisha yao ni kuingia katika Sabato ya milele na kuneemeka kama jumuiya ya upendo. Uwepo wao ni kielelezo cha mafungamano na Mwenyezi Mungu Muumbaji pamoja na jirani zao wanaounda familia moja sanjari na viumbe wote wanaoishi katika nyumba ya wote. Kuna mahusiano na mafungamano ya ajabu yanayobubujika kutoka katika upendo alionao Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake wote, upendo unaoviunganisha viumbe vyote.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Jubilei ni kipindi maalum cha kumbukumbu inayopyaisha mafungamano ya maisha. Mahusiano na mafungamano ya kimaumbile hayatengani na udugu, haki na uaminifu kwa wengine. Maadhimisho ya Jubilei ni muda wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza mchakato wa kupyaisha mahusiano na mafungamano yaliyojikita kati ya Mungu, jirani na kazi ya uumbaji katika ujumla wake. Ni muda wa kuganga na kuponya mahusiano yaliyoharibika, ambayo kimsingi ni muhimu sana kwa mfumo mzima wa maisha. Jubilei ni muda uliokubalika wa kurejea tena kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa vyote, ili kujenga na kudumisha amani na Mwenyezi Mungu asili ya mambo yote. Hii ni changamoto ya kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi, kiasi cha kugeuza mambo yote kuwa kama ni bidhaa.

Jubilei ni muda wa kuwafikiria maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuthamini urithi wa pamoja, kwa kushirikiana na kuishi kwa amani na furaha; kwa kusaidiana na kulindana, ili kuondokana na mashindano yasiyokuwa na mvuto wala mashiko. Jubilei ni muda wa kuwaacha huru wale wote waliosetwa na kutumbukizwa katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, hii ikiwa ni pamoja na biashara haramu ya binadamu na kazi za suluba kwa watoto wadogo sanjari na kusikiliza kilio cha Mama Dunia, ili kurejea tena kwa haki katika uhalisia wa kazi ya uumbaji. Binadamu anapaswa kukumbuka kwamba, hata yeye ni sehemu ya kazi ya uumbaji na wala si mtawala. Uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote ni chanzo kikuu cha athari za mabadiliko ya tabianchi na janga la Virusi vya Corona, COVID-19 ambalo limewaathiri sana maskini na wanyonge sehemu mbali mbali za dunia. Haya yote ni matokeo ya uchoyo na ulaji wa kutisha.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Maadhimisho ya Kipindi cha Kazi ya Uumbaji, iwe ni fursa ya kumpatia Mwenyezi Mungu sifa na utukufu; nafasi ya kugundua tena na tena uzuri wa kazi ya Uumbaji na hivyo kumrudishia Mungu sifa na utukufu. Dunia iwe ni mahali pa sala, tafakari na mshangao, ili kuweza kuishi kwa amani na utulivu na kazi nzima ya Uumbaji kama wanavyofanya watu asilia kutoka Ukanda wa Amazonia. Mwenyezi Mungu aliitenga Siku ya Sabato kwa ajili ya kustarehe na ardhi iweze kupta rutuba. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, mambo yamegeuka sana kiasi cha mwanadamu kujikuta akiwa ametumbukizwa katika mzunguko wa uzalishaji na ulaji, kiasi cha kutishia mazingira nyumba ya wote. Kuna ukataji mkubwa wa miti, mmomonyoko wa ardhi, ongezeko la jangwa pamoja na maziwa ya acidi kutokana na ongezeko la joto duniani, kuendelea kuongezeka maradufu. Hiki ni kilio cha Mama Dunia! Maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kupumzika kwa kuondokana na shughuli zao za kila siku ili kutoa nafasi kwa ardhi iweze kupata tena rutuba na ekolojia kurejea katika hali yake ya kawaida, ili kumuenzi mwanadamu.

Janga la Corona, COVID-19 limewasaidia watu kuanza kufikiria njia mpya za maisha, kwa sababu baada ya watu kufungiwa kwenye karantini, hali ya hewa na mazingira kwa ujumla yameboreka sana. Huu ni muda wa kuendelea kupandikiza tunu msingi za maisha kwa kujikita na mambo yanayosaidia kupyaisha maisha. Ni fursa ya kutathmini matumizi ya nishati, ulaji, usafiri na lishe, kwa kuondokana na mambo ya ziada pamoja na mambo yale ambayo ni hatari sana kwa mchakato wa ukuaji wa uchumi, biashara, uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa. Haki ikiwa kichwani mwa binadamu, binadamu anaweza kuisaidia dunia kuboreka zaidi. Watu mahalia walindwe dhidi ya makampuni makubwa yanayoendelea kufaidika na utajiri wa madini, mafuta ghafi, mbao na mazao ghafi ya kilimo. Utawala thabiti wa sheria kitaifa na kimataifa unahitajika ili kudhibiti ukwapuaji mkubwa wa rasilimali na madini pamoja na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka kwa wale wote wanaoathirika na vitendo hivi.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya VI ya Kuombea Kazi ya Uumbaji sanjari na maadhimisho ya Kipindi cha Kazi ya Uumbaji kwa Mwaka 2020 kwa kusema kwamba, Jubilei ni muda muafaka kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Ni fursa ya kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na kilio cha maskini, kinachoendelea kuongezeka kila kukicha. Hata hivyo pia kuna ushuhuda wa watu wa Mungu wanaoendelea kusimama kidete kujenga, kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Kuna watu wanaoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kuwalinda na kuwatetea maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana na jumuiya mahalia zinaendelea kujitokeza kujibu changamoto za kipeo cha ekolojia! Kwa hakika mambo yanaweza kubadilika.

Maadhimisho ya “Mwaka Maalum wa Laudato si” kuanzia tarehe 24 Mei 2020 hadi tarehe 24 Mei 2021, yanaendelea kuhamasisha watu katika ngazi mbali mbali kusimama kidete kulinda mazingira nyumba ya wote. Watu wa Mungu katika ngazi na nyanja mbali mbali za maisha wajifunze kuwa na sera na mbinu mkakati kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwa kushirikiana na kushikamana, binadamu anaweza kujenga dunia inayosimikwa katika haki, amani na maendeleo fungamani. Kwa hakika maadhimisho haya kwa sasa yana mwelekeo wa kiekumene kwa kutambua kwamba, wote wanaoishi hapa ulimwenguni ni kama watoto wa familia kubwa ya binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwimbia Mwenyezi Mungu wimbo wa sifa na shukrani, kwa kuendelea kuenzi juhudi za waja wake, kwa Neno wa Mungu kufanyika mwili na kukaa kati ya watu wake sanjari na kuendelea kupyaisha uso wa nchi kwa mapaji ya Roho Mtakatifu.

Nia za Papa Septemba
24 September 2020, 14:49