Tafuta

Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa Raia Mjini Vatican mwaka 2020 kinaadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, kielelezo cha ushirikiano kati ya Vatican na Italia katika ulinzi na usalama Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa Raia Mjini Vatican mwaka 2020 kinaadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, kielelezo cha ushirikiano kati ya Vatican na Italia katika ulinzi na usalama 

Miaka 75 ya Kikosi Cha Ulinzi Na Usalama wa Raia Mjini Vatican

Papa amekutana na kuzungumza na askari, wafanyakazi pamoja na familia za Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa Raia mjini Vatican. Katika hotuba yake, amegusia historia, Mchango wa Papa Pio XII katika Waraka wake wake wa “Defensor Civitatis” yaani “Mlinzi wa Mji wa Roma” pamoja na tunu msingi zinazopaswa kumwilishwa katika huduma ya ulinzi na usalama wa raia mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa Raia mjini Vatican kinaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake na Papa Pio XII katika Waraka wake wa Kitume “Defensor Civitatis” yaani “Mlinzi wa Mji wa Roma”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 28 Septemba 2020 amekutana na kuzungumza na askari, wafanyakazi pamoja na familia za Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa Raia mjini Vatican. Katika hotuba yake, amegusia historia ya Kikosi hiki, Mchango wa Papa Pio XII katika Waraka wake wake wa “Defensor Civitatis” yaani “Mlinzi wa Mji wa Roma” pamoja na tunu msingi zinazopaswa kumwilishwa katika huduma ya ulinzi na usalama wa raia mjini Vatican. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maadhimisho ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa Raia mjini Vatican, kielelezo cha ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya Italia. Ushirikiano huu unapata chimbuko lake kunako tarehe11 Februari, 1929, Kanisa Katoliki lilipotiliana sahihi Mkataba na Serikali ya Italia “Patti Lateranensi” iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha shughuli za Kanisa na Serikali.

Huo ukawa ni mwanzo wa Serikali huru ya Vatican, iliyoruhusu waamini, wageni na watalii kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican chini ya ulinzi na usimamizi wa Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa Raia mjini Vatican, kilichokuwa chini ya Serikali ya Italia. Kutokana na dharura na hali ngumu ya maisha iliyokuwepo, nguvu nyingi za kisiasa na kijamii zilielekezwa katika mchakato wa ujenzi wa demokrasia. Mwezi Machi 1945, chini ya uongozi wa Waziri mkuu na ambaye alikuwa Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Italia Ivanoe Bonomi, alipoanzisha Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kunako mwaka 1943, mji wa Roma ulivamiwa na wanajeshi kutoka Ujerumani na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Wanajeshi hawa hawakuthamini uhuru wa mji wa Vatican na Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa muda wa miezi tisa, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ukageuka kuwa ni mahali pa machafuko na kinzani, kiasi kwamba, waamini na watu wenye mapenzi mema hawakupata nafasi rahisi ya kutembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 4 Juni 1944 mji wa Roma ukakombolewa, lakini ukawa umeacha madonda na makovu makubwa kwenye dhamiri za watu, uharibifu mkubwa mali na miundombinu, umaskini na mateso kwa familia nyingi. Kwa hakika haya ndiyo madhara ya vita! Waamini, mahujaji na wageni waliopata nafasi ya kwenda kutembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Pettro mjini Vatican, walikwenda pia kumpongeza Papa Pio XII aliyejipambanua kuwa “Defensor civitatis”. Ofisi za Kikosi cha Ulinzi na Usalama wa raia mjini Vatican kikawa na jukumu la kutoa huduma makini kwa Italia na Vatican katika jumla wake. Hii ilikuwa ni fursa ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili pamoja na kuhakikisha ulinzi na usalama wa Baba Mtakatifu. Tangu wakati huo, askari wa kikosi cha ulinzi na usalama wa raia mjini Vatican wameendelea kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa. Hii ni huduma inayojipambanua kwa: bidii, weledi sanjari na moyo wa sadaka. Ni huduma inayofumbatwa katika uvumilivu mkubwa kwa kukutana na kujadiliana na watu kutoka katika nchi na tamaduni mbalimbali duniani, bila kusahau majadiliano na wakleri.

Baba Mtakatifu anawashukuru kwa ulinzi na usalama wanaompatia wakati anapotembelea sehemu mbalimbali za Italia. Hii ni kazi ngumu sana inayohitaji busara na hekima ili kwamba, hija za Khalifa wa Mtakatifu Petro zinamwezesha kukutana na watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anawahimiza wanajeshi wa kikosi cha ulinzi na usalama wa raia mjini Vatican kuendelea kutekeleza dhamana na majukumu yao mintarafu mwanga angavu wa historia yao, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati, ili hatimaye, waweze kupata mafanikio makubwa zaidi. Huu ni utume unaowataka kumwilisha ndani mwao tunu msingi za maisha ya kiutu na kiroho, daima wakijitahidi kuwa ni mashuhuda wa imani hai ya Kikristo. Hii ni amana na utajiri wa maisha ya kiroho, waliyorithishwa na familia zao na kwa sasa wanahimizwa kuwarithisha pia watoto wao! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Malaika Mkuu Mikaeli na ya Bikira Maria, ili awalinde na kuwaombea wao pamoja na familia zao.

Miaka 75 ya Usalama
28 September 2020, 16:32