Tafuta

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa litaanza "kutimua vumbi" kuanzia tarehe 2-12 Septemba 2021 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Visima vyangu vyote vimo kwako" Zab. 87:7 Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa litaanza "kutimua vumbi" kuanzia tarehe 2-12 Septemba 2021 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Visima vyangu vyote vimo kwako" Zab. 87:7 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa Sept. 2021: Shuhuda!

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria: Kaulimbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7 sasa litaadhimishwa kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 12 Septemba 2021. Maandalizi yamepamba moto kwa shuhuda mbalimbali zilizotolewa kwa njia ya mitandao ya jamii mintarafu: Imani, Ekaristi Takatifu na Madhara ya Virusi vya COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) lililokuwa limepangwa kuadhimishwa kuanzia tarehe 13-20 Septemba 2020, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7 sasa limesogezwa mbele na litaanza kuadhimishwa tarehe 5 hadi tarehe 12 Septemba 2021. Maamuzi haya mazito yametolewa na Baba Mtakatifu Francisko baada ya kushauriana na Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria. Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Sala ya Malakaika wa Bwana Jumapili tarehe 20 Septemba 2020, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewatia moyo na matumaini, watu wa Mungu nchini Hungaria na wale wote waliokuwa wamejiandaa kwa ajili ya maadhimisho hayo. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kuendelea na maandalizi haya kiroho, kwa kuunganika pamoja. Waamini watambue kwamba, Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Sekretarieti kuu ya Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari inabainisha kwamba, zaidi ya waamini 60,000 walikuwa wamekwisha kujiandisha kushiriki katika maadhimisho haya, kama yalivyokuwa yamepangwa hapo awali.

Kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Kongamano hili, hivi karibuni, wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliweza kushiriki katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mitandao ya kijamii. Kardinali Peter Erdo’ Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, Hungaria alitoa hotuba elekezi na wajumbe wakachangia kuhusu mang’amuzi yao mintarafu janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona Covid-19; madhara yake katika imani, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, changamoto na fursa zinazoendelea kujitokeza kutokana na janga hili. Kwa upande wake, Askofu mkuu Piero Marini, Rais wa Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa amesema, janga la Virusi vya Corona, COVID-19, limegusa na kutikisha imani ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia kwani Ekaristi Takatifu ni mahali ambapo waamini wanatolea sadaka ya shukrani na sifa, tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa Unjilishaji mpya, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Kipindi cha watu kuwekwa karantini, umekuwa ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu unaopata chimbuko lake kutoka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekarisri Takatifu. Kumbe, huu ni wakati wa toba na wongofu wa kiekolojia, ili kuweza kuwa na matumaini ya ulimwengu ulio bora zaidi kwa siku za usoni. Wajumbe wengine wamekazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani kama njia ya kupyaisha maisha ya kiroho, daima watu wakiwa na hofu ya Mungu katika maisha yao. Katika shida na mahangaiko mbalimbali kama inavyojitokeza kwa wakati huu kutokana na janga la Virusi vya Corona, VOVID-19, kuna haja kwa waamini kuimarisha imani na matumaini yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; imani ambayo inamwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu yajenge na kuimarisha umoja miongoni mwa waamini; wajitahidi kujichotea neema na baraka kutoka mbinguni ili kushiriki katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na maridhiano mintarafu ujumbe kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe.

Wajumbe wamewapongeza watu wa Mungu kutoka Hungaria wanaoendelea kuchangia mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini Barani Afrika; amani na mshikamano na udugu wa kibinadamu huko Mashariki ya Kati. Waamini wametakiwa kuachana na tafsiri potofu kwa kudhani kwamba, Virusi vya Corona, COVID-19 ni kielelezo cha dhambi na hasira ya Mungu kwa binadamu. Mwenyezi Mungu daima ni mwingi wa huruma na mapendo, yuko kati pamoja na waja wake. Neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, ziwaimarishe waamini katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho, tayari kusimama na kuendelea na mapambano ya maisha. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili na matumaini kwa wale wote wanaoteseka na kunyanyasika katika maisha, ili wote waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Itakumbukwa kwamba, Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani.

Hili ni Fumbo kubwa linalopaswa kuadhimishwa vyema; Kuabudiwa na Kutafakariwa kikamilifu. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Kaa Nasi Bwana”: Mane, Nobiscum Domine”, anawaalika waamini kujenga utambuzi hai wa uwepo halisi wa Kristo Yesu, katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu na katika Ibada nje ya Misa. Itakumbukwa kwamba, Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, kuanzia tarehe 25-31 Januari 2016 huko Cebu, nchini Ufilippini yaliongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani mwenu, matumaini ya utukufu”.  Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai 1: 27.  Hii ilikuwa ni fursa makini ya kukuza na kuimarisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu nchini humo sanjari na Maadhimisho ya Miaka 500 tangu walipoinjilishwa kwa mara ya kwanza.  Hii ni changamoto ya kuhamasisha mchakato wa uinjilishaji mpya, ari na moyo wa kimissionari ili kumshuhudia Kristo Yesu kwa kina na mapana zaidi. Kwa mara ya kwanza, Hungaria ilikuwa mwenyeji wa Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa kunako mwaka 1938.

Kardinali Peter Erdo’ Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, Hungaria anasema, maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa yanapaswa kugusa hali halisi ya maisha ya watu wa Mungu ndani na nje ya Hungaria. Lengo ni kutangaza na kushuhudia uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi, ili kuwawezesha waamini kutambua na kukiri kwamba, kwa hakika Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho haya ni fursa kwa waamini kujichotea nguvu, ari na mwamko mpya wa maisha na utume wao katika medani mbali mbali za maisha na hasa wakati huu, hofu kubwa ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, inapoendelea kutishia usalama na maisha ya watu wengi duniani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, udugu na mshikamano kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa walemavu ndani ya jamii.

Ekaristi Takatifu ni kikolezo makini cha Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume wa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kongamano hili litawawezesha waamini kutambua umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kukoleza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kumbe, maadhimisho ya Makongamano la Ekaristi Takatifu katika ngazi mbali mbali ni fursa makini inayopania kupyaisha imani inayomwilishwa katika maisha ya watu, kielelezo makini cha imani tendaji.

Kongamano la Ekaristi Kimataifa

 

23 September 2020, 14:50