Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowaandikia watawa wa Shirika la Malaika Mkuu Mikaeli, C.S.M.A, amewataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowaandikia watawa wa Shirika la Malaika Mkuu Mikaeli, C.S.M.A, amewataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi 

Barua ya Papa Francisko Kwa Shirika la Malaika Mkuu Mikaeli

Papa anamshukuru Mungu kwa uwepo na karama ya Shirika! Anafafanua umuhimu wa Jubilei na changamoto zilizoko mbele yao. Anawataka waendelee kujiweka chini ya ulinzi wa Malaika mkuu Mikaeli. Anawatia shime ili wasonge mbele kwa kujiamini, furaha na uaminifu uliopyaishwa, huku wakiendelea kufuata nyayo za mwanzilishi wa Shirika lao Mwenyeheri Bronislao Markiewicz.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Malaika Mkuu Mikaeli, C.S.M.A, “Congregatio Sancti Michaëlis Archangeli” lililoanzishwa na Mwenyeheri Bronislao Markiewicz (1842-1912) mwaka 2020 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu lilipoidhinishwa rasmi na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomtumia Padre Dariusz Wilk, C.S.M.A., Mkuu wa Shirika kama sehemu ya maadhimisho haya anamshukuru Mungu kwa uwepo na karama ya Shirika hasa kwa maskini pamoja na utume wao; umuhimu wa Jubilei hii pamoja na kutambua changamoto zilizoko mbele ya maisha na utume wao, daima waendelee kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Malaika mkuu Mikaeli. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anasema, anataka kuwatia shime ili wasonge mbele kwa kujiamini, wakiwa wenye furaha na uaminifu uliopyaishwa, huku wakiendelea kufuata nyayo za mwanzilishi wa Shirika lao Mwenyeheri Bronislao Markiewicz. Katika maisha na utume wake amekuwa kama punje ya haradali iliyokuwa ndogo sana lakini kwa sasa umekuwa ni mti mkubwa unaotoa hifadhi kwa ndege wa angani.  Rej. Lk. 13: 18-19.

Mwenyeheri Bronislao Markiewicz amezaliwa Jimbo Katoliki la Przemyśl, huko ndiko alikopandikiza kwanza mbegu ya utume wake, ambao unaendelea kuzaa matunda sehemu mbalimbali za dunia. Kabla ya kuanzisha Shirika, Mwenyeheri Bronislao Markiewicz alikuwa ni Msalesiani wa Don Bosco aliyejenga mahusiano ya pekee sana na Mtakatifu Yohane Bosco. Aliporejea nchini Poland akitokea nchini Italia aliendelea kuwahudumia watoto maskini na wale waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu na hatarishi. Akawahamasisha waamini waliojiunga pamoja naye na kuanzisha Shirika la Malaika Mkuu Mikaeli. Kunako mwaka 1912 Mwenyeheri Bronislao Markiewicz akafariki dunia. Tarehe 29 Septemba 1921 Shirika likaidhinishwa na Kardinali Adam Stefan Stanisław Bonifacy Józef Sapieha Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, Poland.  Amana, urithi wa maisha na utume wa mwanzilishi wa Shirika uliwasukuma wanashirika kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto zilizokuwa zinajitokeza, kiasi cha kuzitolea ushuhuda kwa kumwaga damu yao kama ilivyokuwa kwa Wenyeheri Ladislao Błądziński na Adalberto Nierychlewski.

Karama ya Shirika inajipambanua vyema zaidi kwa kujikita katika huduma kwa watoto maskini, yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwataka waanze kujikita zaidi katika kuwapokea, kuwalinda na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwapatia elimu makini, fursa ya michezo na makazi ili waweze kupata huduma msingi, malezi na makuzi yao. Watoto wapewe elimu dunia na malezi ya Kikristo, zawadi kubwa ambayo Shirika linaweza kutoa kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Vijana hawa wanawahitaji walezi wanaowaongozwa kwa upendo wa kibaba, wema wa Injili, kwa ajili ya makuzi yao ya kiutu na kidini, ili hatimaye, wote waweze kwenda kwa Baba wa milele. Watoto na vijana hawa si kwamba, wanakosa mahitaji yao msingi, lakini mara nyingi ndio wale wanaotumbukizwa kwenye mifumo ya utuma mamboleo pamoja na matmizi mabaya ya dawa za kulevya.

Shirika linapaswa kujikita zaidi katika utume wa vijana kijamii ili kuwaokoa katika “makucha” ya watu waovu na wadhalimu. Utume huu unaweza kutekelezwa kwa njia machapisho mbalimbali kutoka Kiwanda cha “Michalinem” pamoja na Majarida ya “Temperanza”, “Lavoro” na “Chi come Dio”. Huu ni urithi na amana ya Shirika ambayo pia ni muhimu sana katika mchakato wa mawasiliano ya jamii yanayo endelea kuboreshwa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kiasi cha kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kuzalisha “chakula” kinachohitajika kwa ajili ya akili na majiundo makini ya dhamiri nyofu. Katika maadhimisho ya Jubilei hii, Baba Mtakatifu anawaalika wanashirika kuwa wapole na wanyenyekevu ili kuweza kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu na kumwachia nafasi ya kusaidia kupyaisha umoja wa kidugu, ili kutekeleza utume wao kwa moyo wa dhati kabisa. Kamwe wasichoke kusikiliza na kujibu kilio cha watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; daima wajitahidi kugusa madonda ya mateso na mahangaiko ya wengine, wasitafute maficho binafsi na yale ya kijumuiya na badala yake waingie kwenye uhalisia wa maisha ya jirani zao ili kugundua nguvu ya wema.

Kwa kuishi namna hii, kwa hakika, watakuwa ni mashuhuda wa Kristo na walinzi wa watu. Ulimwengu mamboleo unawahitaji watawa ambao wako tayari kuangalia mahitaji ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kumwilisha karama za Mashirika yao katika nyanja mbalimbali za maisha kama hospitali kwenye uwanja wa mapambano. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ili kuweza kufikia lengo hili katika utume wao, hawana budi kuvunjilia mbali kuta za utengano na hali ya kutowajali wengine, ili kudumisha umoja, daima wakijitahidi kudumu katika karama yao. Kilio cha Malaika mkuu Mikaeli “Ni nani aliye sawa na Mungu?” Malaika Mkuu anawalinda watu wa Mungu dhidi ya ubinafsi, mambo msingi yanayobainishwa kwenye Majarida ya Shirika, kama dira na mwongozo wa utekelezaji wa karama yao ya Shirika.

Tunu hizi msingi ziwe ni kielelezo cha wito na utume wao, ili hatimaye, kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ubaya wa moyo, kwa kusambaza matendo ya huruma ya Mungu: kiroho na kimwili. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia kila la heri na baraka katika huduma yao kwa Kanisa na waendelee kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Injili yake. Bikira Maria na Malaika Mkuu Mikaeli wawe ni walinzi madhubuti katika njia ya Shirika, wanapotekeleza utume wao.Wanashirika wote wamepewa baraka ya kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. 

Barua 100 Yrs
29 September 2020, 15:56