Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Oktoba 2020 anatarajiwa kuweka sahihi katika Waraka Mpya wa Kitume "Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii" Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Oktoba 2020 anatarajiwa kuweka sahihi katika Waraka Mpya wa Kitume "Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii" 

Papa: Waraka wa Kitume: "Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii"

Papa Francisko tarehe 3 Oktoba 2020 majira ya jioni baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mt. Francisko wa Assisi, atatia mkwaju kwenye Waraka wake wa Kitume ambao umepewa kichwa cha habari “Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Huu ni utajiri wa maneno kutoka kwa Mt. Francisko wa Assisi, anayewaalika watawa wote, kuchukuliana kama ndugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Oktoba 2020 majira ya jioni baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa lililoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi, lililoko mjini Assisi, nchini Italia, atatia mkwaju kwenye Waraka wake wa Kitume ambao umepewa kichwa cha habari "Fratelli Tutti": “Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Huu ni utajiri wa maneno kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi, anayewaalika ndugu zake watawa wote, kuchukuliana kama ndugu; na kwa mchungaji mwema, ili kuweza kuwaokoa kondoo wake anavumilia mateso ya Msalaba. Kutokana na hatari za maambukizi mapya ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Ibada hii ya Misa itaadhimishwa kwa faragha na kuhudhuriwa na watu wachache tu. Baada ya maadhimisho haya, Baba Mtakatifu atarejea tena mjini Vatican kuendelea na shughuli zake.

Hii ni kadiri ya taarifa iliyotolewa na Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican. Waraka huu wa kitume ni mwendelezo wa Waraka wa Lumen Fidei uliochapishwa kunako mwaka 2013 na Waraka wa kitume wa Laudato si wa Mwaka 2015. Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unagusa na kuzama kabisa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anayewaita watu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ndugu zake, ili kujenga na kudumisha Injili ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati, huku binadamu wote wakitambua kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, wote ni ndugu wamoja wanaounda familia kubwa ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, udugu wa kibinadamu unapata chimbuko lake kutoka katika  imani kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote na ni Baba wa amani! Historia inaonesha kwamba, hii itakuwa ni mara ya nne kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea mji wa Assisi.

Kwanza kabisa ilikuwa ni tarehe 4 Oktoba 2013 na kwa mwaka 2016 alitembelea mji wa Assisi mara mbili. Kwa upande wake Askofu mkuu Domenico Sorentino wa Jimbo la Assisi - Nocera Umbra - Gualdo Tadino anasema kwamba, wanausubiri kwa mikono miwili ujio wa Baba Mtakatifu Francisko mjini Assisi. Huu ni  Waraka ambao, unawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujisikia kuwa ni ndugu wamoja katika shida, mahangaiko na changamoto dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Waraka huu ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Waraka
05 September 2020, 16:27