Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 30 Agosti 2020 ametafakari kuhusu Kashfa ya Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 30 Agosti 2020 ametafakari kuhusu Kashfa ya Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu. 

Papa Francisko: Tafakari Kuhusu Kashfa ya Fumbo la Msalaba!

Kwa Kristo Yesu, kashfa inakuja pale Mkristo anapoukimbia Msalaba, yaani kukimbia na kutofanya mapenzi ya Mungu, utume na kazi ya ukombozi ambayo alitumwa na Baba yake wa mbinguni kuja kuutekeleza. Ni kutokana na mazingira haya, Kristo Yesu, akageuka na kumwambia Petro “Nenda nyuma yangu, Shetani! U kikwazo kwangu, maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Mathayo katika Sura ya 16: 13-20 anamweka Mtume Petro mbele ya macho ya Mitume wa Yesu na kushuhudia kwamba kwa hakika Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai. Naye Yesu akajibu na kumwambia “Heri wewe Simon Bar-yona, kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote ya kwamba yeye ndiye Kristo”. Rej. Mt. 16:13-20. Jumapili ya 22 ya Mwaka A wa Kanisa, Injili ni mwendelezo wa Injili ya Mathayo Sura ya 16: 21-27. Katika sehemu hiii ya Injili, Kristo Yesu anatangaza kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu. Wakiwa njiani kuelekea Yerusalemu, Kristo Yesu anaanza kuwafundisha wazi wazi kuhusu Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake, kielelezo cha utukufu wa Mungu.

Lakini kwa bahati mbaya sana, maneno yake hayakueleweka barabara miongoni mwa wanafunzi wake, kwa sababu imani yao bado ilikuwa haijafikia ukomavu na zaidi sana ilikita mizizi yake katika kufuatisha namna ya dunia hii, na kwamba, walipaswa kugeuzwa na kufanywa upya nia zao, ili wapate kujua hakika ya mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. Rej. 12:2. Mitume wa Yesu walikuwa wamezama katika mambo ya ulimwengu huu. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 30 Agosti 2020 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha wa mateso na kifo cha aibu Msalabani, Mtume Petro akamchukua pembeni na kuanza kumkea kwamba “Hasha, Bwana, Mwenyezi Mungu hapendi hivyo, hayo hayatakupata kamwe”. Mtakatifu Petro anamwini na kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai, anataka kumfuasa kikamilifu, lakini, hakubaliani na maelekezo yaliyotolewa na Kristo Yesu kwamba, utukufu wake umetundikwa juu ya Msalaba.

Kwa Mtakatifu Petro, wanafunzi wengine na hata Wakristo katika ulimwengu mamboleo bado Msalaba unaonekana kuwa ni kashfa ya mwaka. Kwa Kristo Yesu, kashfa inakuja pale Mkristo anapoukimbia Msalaba, yaani kukimbia na kutofanya mapenzi ya Mungu, utume na kazi ya ukombozi ambayo alitumwa na Baba yake wa mbinguni kuja kuutekeleza. Ni kutokana na mazingira haya, Kristo Yesu, akageuka na kumwambia Petro “Nenda nyuma yangu, Shetani! U kikwazo kwangu, maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu” Rej. Mt. 16: 23. Lakini, ni muda mfupi tu aliopita anasema Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kristo Yesu alikuwa amempongeza Mtakatifu Petro na kuahidi kwamba, angekuwa ni msingi wa ujenzi wa Kanisa lake, lakini baada ya kitambo kidogo anamwambia ni Shetani. Hii ni hali ya kawaida kwa waamini wakati wa ibada na mafanikio, wakati wa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani, wanamwona Kristo Yesu akiwa karibu nao na hivyo kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Lakini, pale Msalaba unapoibuka katika maisha, wote wanatamani kukimbia, kwa sababu hii ndiyo kazi ya Ibilisi, Shetani anayetaka kuwaondoa katika Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu!

Wakati huo huo, Kristo Yesu, akawageukia wanafunzi wake na kuwapatia masharti ya kumfuasa akisema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike Msalaba wake, anifuate”. Hii ndiyo njia makini anayopaswa kuifuata mfuasi wa Kristo Yesu, akitangaza na kushuhudia umuhimu wa kujikana mwenyewe unaozama katika toba na wongofu wa ndani, kwa kuambata na kukumbatia tunu msingi za Kiinjili. Pili, mfuasi wa Kristo Yesu anapaswa kuuchukua Msalaba wake na kumfuasa Kristo Yesu, akiwa tayari kuvumilia mateso na mahangaiko ya maisha ya kila siku; lakini zaidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa imani, huku akiendelea kupambana na mahangaiko pamoja na matokeo yake. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, kuuchukua Msalaba ni sehemu ya ushiriki wa kazi ya ukombozi wa ulimwengu iliyoanzishwa na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutambua maana na umuhimu wa Msalaba walioutundika kwenye kuta za nyumba zao, au kitani cha Msalaba wanachovaa shingoni, iwe ni alama ya waamini kutaka kujiunga na Kristo Yesu, ili kuwahudumia jirani kwa upendo wa dhati kabisa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Msalaba ni alama takatifu ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni Sadaka ya Kristo Yesu na kamwe, Msalaba usigeuzwe kuwa ni alama ya mapambo shingoni au kuhusianishwa na imani za kishirikina. Kila mara mwamini anapomtaza Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, wamwone kuwa ni Mtumishi mwaminifu wa Mungu, aliyetekeleza dhamana na utume wake, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za binadamu. Matokeo yake, kama kweli waamini wanataka kuwa wafuasi wake, wanapaswa kufuata nyayo zake, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa tafakari yake, amemwomba Bikira Maria aliyeungana na Mwanaye wa pekee katika Njia ya Msalaba hadi Mlimani Kalvari, awasaidie waamini kupambana kikamilifu na matatizo pamoja na majaribu ya maisha, kama kielelezo makini cha ushuhuda wa Injili. Waamini wanawajibika kupambana bila ya kujibakiza dhidi ya Shetani, Ibilisi, wapambane dhidi ya ubaya wa moyo na dhambi.

Papa: Fumbo la Msalaba

 

 

30 August 2020, 14:28