Tafuta

Vatican News
2020.08.28  Papa Francisko kutembeleza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Agostino, Roma 2020.08.28 Papa Francisko kutembeleza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Agostino, Roma  

Papa Francisko:Kubali kuwa wokovu wa Bwana waweza kuja kwa njia tusiyotarajia!

Katika ujumbe kwa njia ya mitandao ya kijamii Papa anasema "Mtumaini Bwana na jitahidi kuingia katika mipango yake,ukubali kwamba wokovu wake unaweza kuja kwetu kwa njia nyingine kuliko zile tunazotarajia".28 Agosti Kanisa linakumbuka Mtakatifu Agostino,mwalimu wa Kanisa ambaye alipitia mengi hasa maisha ya anasa hadi kuongoka kwa njia ya maombezi na machozi ya mamaye.

Na Sr. Angela Rwezaula -Vatican

Katika ukurasa wa mitandao ya kijamii wa Papa Francisko, ujumbe wake amesema ”Mtumaini Bwana na jitahidi kuingia katika mipango yake, ukubali kwamba wokovu wake unaweza kuja kwetu kwa njia nyingine kuliko zile tunazotarajia”. Kwa kutafakari kwa kina juu ya ujumbe huu katika mwanga wa wa siku ya leo kumbe basi  unaweza kuangazia maisha ya Mtakatifu Agostino wa Hippo ambaye tarehe 28 Agosti ya kila mwaka  Mama Kanisa anamkumbuka mtakatifu huyu Padre, Askofu na mwalimu wa Kanisa ambaye katika maisha yake amepitia mengi hasa kuanzia maisha ya anasa, hadi kufikia kuongoka. Anakumbukwa sana  uongofu wake na urithi wa barua nyingi zenye ushuhuda wa upendo kwa Bwana. Yeye anathibitisha, si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mdhambi. Kama tarehe 27 Agosti Mama Kanisa alimkumbuka Monika Mama yake, basi ni kusema kuwa utakatifu wake ni matunda ya sala, tafakari na machozi mengi ya mama yake.

Alizaliwa nchini Algeria 

Mtakatifu Agostino wa Hippo alizaliwa huko Thagaste, leo mji huo unaitwa Souk Ahras nchini Algeria, kunako tarehe 13 Novemba mwaka 354 na mauti yakamfikia mnamo tarehe 28 Agosti mwaka 430. Yeye alikuwa mtawa wa shirika la kiagostino.  Katika suala la neema na dhambi ni Agostino aliyefundisha kwamba ubinadamu umerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu. Uhuru wa asili umepotezwa na dhambi hiyo, na hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwao. Utakaso unaopatikana kwa imani unasababisha ondoleo kamili la dhambi zote kabisa. Halafu mwamini anazidi kufanywa mpya kwa mchakato utakaokamilishwa na ufufuko wa siku ya mwisho. Mchakato huo wote ni kazi ya neema ya Mungu na  bila hiyo, binadamu hawezi kuongoka, kukwepa dhambi na kufikia utimilifu wa wokovu.

Mafundisho makuu ya  Mtakatifu Agostino

Hayo yote ni zawadi tu ya Mungu, kama vilivyo pia udumifu na stahili za mtu. Sisitizo hilo la kwamba neema ni dezo, lilimuongoza Augustino kufundisha juu ya uteule, neema ambayo hakuna anayeweza kuikataa na ambayo inafikisha kwa hakika mbinguni. Kwa nini Mungu hawapi wote neema hiyo ni fumbo ambalo tuliinamie tu, kwa sababu hatuwezi kabisa kulielewa. Kwa vyovyote haiwezekani kumlaumu Mungu kwa ajili hiyo, eti si haki. Mawazo hayo yalikuja kukaziwa zaidi tena na watu kama Martin Luther, Yohane Kalvini na Janseni, namna iliyokataliwa na Kanisa Katoliki.

Mawazo yake Mtakatifu Agostino yanaacha mshangao mkubwa

Ee upendo wenye kuwaka daima usiweze kuzimika kamwe, Mungu wangu uniwashe moto! Unijalie mimi, mimi pia, Bwana wangu mpenzi, nikujue, nikupende na kukufurahia. Nisipoweza kufanya hayo kikamilifu katika maisha haya, unijalie walau kusonga mbele kila siku hata niweze kufikia kuyafanya kwa ukamilifu. Acha nikufahamu zaidi na zaidi hata ukamilifu. Acha nikupende kila siku zaidi na zaidi hata ukamilifu; furaha yangu iwe kubwa kwa yenyewe, na kamili ndani yako. Wewe ni nini kwangu? Uniwie huruma, niweze kusema. Mimi ni nini kwako, hata uniagize nikupende, halafu nisipokutii unanikasirikia na kunitishia maafa makubwa? Je, kutokupenda si balaa kubwa tayari? Lo, kwa huruma yako, Bwana Mungu wangu, uniambie wewe ni nini kwangu. “Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako”. Sema hivyo, nami nitasikiliza. Tazama, moyo wangu unakusikiliza, Bwana; uuweke tayari ukaniambie, “Mimi ni wokovu wako”. Nitafuata sauti ya neno lako hilo hata nikufikie. Usinifiche uso wako: nife nisije kufa, bali niuone uso wako.

Historia yake na maandiko yake bado ni ya kusisimua sana katika maungamo

Unijalie nifanye unachoagiza, halafu uniagize unachotaka: Nimechelewa kukupenda, Uzuri wa kale na mpya daima; nimechelewa kukupenda. Tazama, wewe ulikuwa ndani mwangu, nami nilikuwa nje na kukutafuta huko. Mimi, mbaya, nilikuwa ninaparamia vitu vizuri ulivyoviumba. Wewe ulikuwa nami, lakini mimi sikuwa nawe. Vilikuwa vikinishika mbali nawe viumbe vile ambavyo kama visingekuwa ndani yako hata kuwepo visingekuwepo. Uliniita, ukanipigia kelele, ukashinda uziwi wangu. Uliniangaza, ukanimulikia kama umeme angani, hatimaye ukaponya upofu wangu. Ulinipulizia harufu yako nami nikainusa, na sasa nakuonea shauku. Nimekuonja na sasa nakuonea njaa na kiu. Umenigusa nami sasa nawaka tamaa ya kupata amani yako. Sasa nakupenda wewe tu, nakufuata wewe tu, nakutafuta wewe tu, niko tayari kukutumikia wewe tu, kwa kuwa wewe tu unatawala kwa haki, natamani kuwa chini ya uwezo wako. Naomba kitu hiki tu kutokana na hisani yako kuu: kwamba unigeuzie kabisa kwako, usiruhusu chochote kunizuia nisielekee kwako. Historia yake na maandiko yake ni ya kusisimua sana na kuvutia kuendelea kumtafuta Bwana kila wakati, kwa utambuzi wa kuwa sisi sote ni wadhambi, na kukumbuka ushuhuda wake kwamba hatutaweza kabisa kutulia, hadi tunapumzika ndani mwake Yeye!

ST AUGUSTINE SONG
28 August 2020, 14:38