Tafuta

Vatican News
2018.08.23 Mtakatifu Monica na Mtakatifu Agostino 2018.08.23 Mtakatifu Monica na Mtakatifu Agostino  (©Renáta Sedmáková - stock.adobe.com)

Papa Francisko:Jitihada zetu ziwasaidie wengine waweze kuwa na kiu ya Mungu!

Tarehe 27 Agosti 2020 katika mitandao ya kijamii Papa Francisko anashauri kutokuwa na utulivu wa moyo lakini mtakatifu kwa kutafuta wema na kweli ambayo ni Mungu.Jitihada zetu ni kuwasaidia wengine waweze kuwa na kiu ya Mungu.Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Monika,ambaye ni mwombezi wa mioyo kama hii isiyo na utulivu,ni mfano wa kuomba bila kuchoka kwa machozi mengi.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Wazo la Papa Francisko katika mitandao ya kijamii, Alhamisi tarehe 27 Agosti 2020 anaandika “katika mioyo yetu tunapaswa kutokuwa na utulivu lakini Mtakatifu katika utafutaji wa wema wa kweli ambao ni Mungu. Tuwasaidie wengine ili waweze kuhisi kiu ya Mungu. Ni Yeye tu  anayetoa amani na furaha ya moyo wetu”. Mantiki ya  kutokuwa na utulivu ndani ya mioyo na  suala la amani limekuwa ni jambo  daima kwa kila  mwanadamu, ambaye hawezi kuvipata hadi anapotulia katika moyo wa Mungu kwa mjibu wa Mwalimu wa Kanisa Mtakatifu Agostino. Papa anapotpa ushauri huu kwa  mwanga wa utulivu mtakatifu anatambua  wazi kwamba mahangaiko yote yanatakiwa yakabidhiwe kwa mwenyezi Mungu. Mantiki hii ya utulivu imefafanuliwa sana na wabobeaji wa kiroho, watakatifu  wa Kanisa na walimu wa Kanisa, kwa mfano wa Mtakatifu Agostino ambaye leo hii Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya mama yeke Mtakatifu Monika.

Mtakatifu Monika ni mwembezi mkubwa katika shida na majaribu

Mtakatifu Monika anapendwa sana kwa maana amekuwa mwombezi na kamwe hamtupi mtu wakati wa shida na majaribu, bali anaendelea kutoa maombi yake ya kimyakimya bila kuchoka hadi ushindi unapopatikana dhidi ya mwovu. Alifanya hivyo kumwombea mwanaye uongofu kwa machozi mengi sana na akafanikiwa. Kuonekana furaha za mtu zilizo za nje haina maana kwamba hana matatizo yanayomsubua rohoni, lakini ni namna gani ya kuyaweka yote mikononi mwa Bwana. Kama Yesu anavyotualika tutambue namna kusali “Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujaza. Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba”(Mt 6-25).

Hali ya kibinadamu na mikasa yake kwa mfano wa Agostino

Tunaweza kudhibitisha kwamba  kila mtu katika hali ya kibinadamu lazima awe na jambo  linalo msibu maana ni sehemu ya maisha na udhaifu wake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Monika, maisha ya mwanzoni ya  mtoto wake Mtakatifu Agostino kwa hakika yalimsononesha sana kama ilivyo kwa mama wengi duniani wanaosumbuliwa na watoto wao kwa tabia zao mbaya. Lakini kwa neema za imani alizojaliwa huyu mama Monika kwake Kristo zilimwezasha kumsaidia hata  mme wake kubatizwa na kufa kifo chema kunako mwaka 371. Mtakatifu Monica aliendelea kuomba huko kutolea machozi katika sala hadi hapo mwanae Agostino alipoongoka.  Hii ni kutaka kuonesha kwamba uovu wote unashindwa kwa njia ya  sala za mama huyu na ambaye mwanae  akiwa tayari amekwisha kuwa Askofu wa Ippona alisema “Ni vigumu kwa mtoto huyo aliyetolewa machozi mengi kupotelea katika giza la mwovu”. Pamoja na tabia na  shigo ngumu ya mtoto wake, Mtakatifu Monika hakukata tamaa na wala kiburi cha mwovu alichokuwa nacho Agostino  hakikumnyamazisha kilio cha Monika mbele ya Mungu baki katika majitoleo ya sala, siku hadi siku, hadi alipopata ushindi mkuu wa mwanaye, ambaye leo hii anasifikia sana katika mafundisho na maandiko yake.

Sala, wema na fadhili zinashinda nguu za mwovu

Papa Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii  ameshauri kutokuwa na utulivu mtakatifu, na zaidi jitihada za kuwasaidia wengine kuwa na kiu ya Mungu. Maneno haya ni wazi kabia kuangazia sura ya Mtakatifu Monika ambaye aliweza kujikabidhi kwenye mahangaiko ya utulivu, kwa maana hiyo wa sala, wema na fadhili, kwa hakika  zinashida nguvu za mwovu, na kumpa heshima mama huyu ambaye leo hii amekuwa ni mfano wa uvumilivu na sala kwa Mama wengi ulimwenguni kote. Akamwombea mwanaye hadi kuwa na kiu ya Mungu shauku ambayo yeye mwenyewe “anajuta kumtambua Bwana akiwa tayari amechelewa”, Lakini akampenda tu. Mama huyu Monika anatufundisha kujieupusha maisha ya bandia ili kusogelea maisha ya udani yenye mwanga ambayo yanaongozwa hadi kufikia furaha kamili ya maisha.  Mwanaye Agostino mwanzoni aliishi maisha ya kijujuu ya bandia yaliyo ya mpito tu, kwa kuvutiwa na anasa. Kwa machozi  mengi yam ama Monika aliwez kweli kushinda hali ya wogoa na kuuutafuta ukweli .

Maisha kwa ufupi ya Mtakatifu Monica

Monika alizaliwa mwaka 331 huko Tagaste nchini Algeria. Tangu utoto wake alifundishwa kumtumikia Mungu na kujietenga na dhambi. Monika alizoea kwenda kusali peke yake kanisani, alikuwa akiwapenda maskini na aliwagawia chakula chake. Alipokua wazazi wake wakamwoza kwa kijana mmoja jina lake Patriki, naye ambaye alikuwa mtu wa ukoo bora, lakini hakuwa mkristu na mwepesi wa kukasirika. Monika alistahimili kwa upole alipogombezwa na mumewe. Alizaa watoto watatu na mmoja wao ndiye Augustino, Mtakatifu na Mwalimu wa Kanisa. Monika aliwafundisha kumpenda Bwana wetu Yesu na kulitaja jina lake kwa heshima. Hata mume wake Patriki naye akaongoka akawa mkristu kwa sababu ya mwenendo safi wa Mtakatifu Monika. Hata hivyo Mtoto wake Augustino alikwenda  kukaa Kartago (Tunisia) ili asome shule, akaendelea katika maarifa yote, lakini alizidi kufanya uashereti na mambo yote yasiyofaa. Alimsikitisha sana mama yake. Siku moja Monika alimwendea askofu mmoja wa huko akamuulizia, je itakuwaje na mwanangu? Naye askofu akamjibu “Usiogope mama, mtoto huyu wa machozi mengi hivi hayawezi kupotea”. Kweli Monika hakumwomba Mungu bure, maana Augustino aliongoka, akabatizwa na Mtakatifu Ambrosi na badaye akaja kuwa mtakatifu na Kanisa kumtambua  mwalimu shujaa wa mafundisho ya Kanisa katoliki. Monika kwamba alipojiona  anakaribia kufa, wakati wako safarini kuelekea kwao alipozaliwa aliwaambia wanawe: “Mnizike mpendavyo ila ninawambeni kitu kimoja tu: Mnikumbuke kwenye altare ya Bwana” na akafa huko Ostia kando ya mji wa Roma nchini Italia mwaka 387.

Sala ya Mama Mkristo kwa Maombezi ya Mtakatifu Monika

Mtakatifu Monika, mwanamke na mama mwenye kuteseka, unajua machozi yangu, mahangaiko na uchungu wangu. Wakati fulani uliteseka kama mimi; naomba unionee huruma kwa mateso niliyonayo, Uniombee. Kutoka kwa Roho Mtakatifu ulipokea zawadi ya ufahamu na busara , nguvu na sala. Uniombee ili nami nijaliwe zawadi zile zile. Kwa kuwa ulikuwa mpatanishi, daima uwaombee mume na watoto wangu na usali kwa ajili ya amani ya nyumba yetu. Kwa maombezi yako ulimwokoa mumeo na mwanao. Utuombee neema ya Mungu ili tuwe na imani katika nyumba yetu. Kutokana na kuhudhuria Misa kila siku uliweza kupata nguvu na faraja; basi utuombee nasi nguvu na faraja katika maisha yetu daima.

Utuombee kwa ajili ya mahitaji yetu muhimu ya kidunia; kusudi tuweze kufanya kazi na kuwa na amani katika familia yetu. Uwakumbuke watoto wangu, ili daima wajue pendo la kweli na hivyo wamtumikie Mungu kwa mapendo safi. Uniombee, ili niwe mama mwema kwao, na mwisho wa maisha haya, mimi pamoja na mume wangu, watoto wangu na wapendwa wangu wote tuweze kufika kwa Mungu, huko ambako wewe upo pamoja na mume wako na watoto wako wote. Kwa njia ya Kristo, Bwana wetu. Amina.

Mtakatifu Monika, Mlinzi wa akina mama Wakristo. Utuombee.

27 August 2020, 14:45