Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kusali na kuwaombea wananchi wa Lebanon wanaokabiliwa nachangamoto mbali mbali baada ya mlipuko ambao umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kusali na kuwaombea wananchi wa Lebanon wanaokabiliwa nachangamoto mbali mbali baada ya mlipuko ambao umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.  (AFP or licensors)

Mlipuko wa Beirut: Sala ya Papa Francisko Kwa Watu wa Lebanon

Takwimu zinaonesha kwamba, watu 177 walifariki dunia. Zaidi ya watu 6, 000 walijeruhiwa vibaya na kwamba, kuna watu zaidi ya laki tatu hawana makazi ya kudumu. Mlipuko huu umesababisha hasara ya dola za kimarekani kati ya bilioni 10-15. Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wa Mungu nchini Lebanon, ili waweze kupata faraja na mshikamano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 16 Agosti 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alisema kwamba, bado anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia wanaokumbana na mateso pamoja na mahangaiko mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee nchini Lebanon ambako hivi karibuni walifikwa na janga la mlipuko uliotokea kwenye bandari ya Beirut nchini Lebanon. Takwimu zinaonesha kwamba, watu 177 walifariki dunia. Zaidi ya watu 6, 000 walijeruhiwa vibaya na kwamba, kuna watu zaidi ya laki tatu hawana makazi ya kudumu. Mlipuko huu umesababisha hasara ya dola za kimarekani kati ya bilioni 10 – 15.

Mlipuko huo umefuatiwa na maandamano makubwa ya wananchi wa Lebanon walioishutumu Serikali kwa rushwa na ufisadi na kutaka ing’atuke kutoka madarakani. Kufuatia shinikizo hili, Waziri mkuu Hassan Dias, tarehe 10 Agosti 2020 “akabwaga manyanga” na kutoka madarakani. Mawaziri na wabunge pia wamejiuzulu. Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa umezindua kampeni ya kutafuta kiasi dola milioni 565 ili kuwasaidia watu wa Mungu nchini Lebanon walioathirika kutoka na mlipuko mkubwa ambao umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Huu ni msaada unaopania kuwajengea wananchi uwezo wa kuokoa maisha na pole pole kuanza kujikwamua na hivyo kujielekeza katika ujenzi mpya wa Lebanon sanjari na kujikomboa kiuchumi. Fedha hii inalenga, Mosi kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na kuwafikishia walengwa kwa wakati.

Fedha hii itawekezwa zaidi kwenye miundo mbinu ya afya, ili kukarabati hospitali sita zilizobomolewa na zahanati 20 zilizoharibika vibaya kutokana na mlipuko huo. Fedha hii itasaidia kutoa malazi na makazi kwa wale wote ambao makazi yao yameharibiwa, sanjari na kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Hivi karibuni wafadhili mbali mbali wamechangia kiasi cha Euro milioni 250 ili kusaidia jitihada za ujenzi wa mji wa Beirut ambao kwa sasa umegeuka kuwa kama mahame ya kale.

Papa: Lebanon

 

16 August 2020, 13:48