Tafuta

Vatican News
  Baba Mtakatifu ametoa zawadi ya mashine 18 za kupumlia kwa ajili ya wagonjwa wa Corona, COVID-19 nchini Brazil Baba Mtakatifu ametoa zawadi ya mashine 18 za kupumlia kwa ajili ya wagonjwa wa Corona, COVID-19 nchini Brazil 

Papa Francisko Atoa Msaada wa Mashine 18 za Kupumlia Brazil

Papa Francisko ameguswa sana na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Brazil na kuamua kuwapatia zawadi ya mashime 18 za kupumlia, kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa waliowekwa kwenye uangalizi maalum. Msaada umetolewa na Asasi ya kujitegemea ya “Hope Onlus” inayotekeleza dhamana na wajibu wake hasa katika sekta ya elimu na afya, kwa kutoa vifaa tiba ili kuokoa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mzunguko mpya wa katekesi unaongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 19 Agosti 2020 amekita tafakari yake hasa kuhusu: Upendeleo kwa maskini na fadhila ya upendo.  Amesema kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limepelekea umaskini mkubwa kuanikwa bayana na ukosefu wa usawa sehemu mbali mbali za dunia kudhihirika hadharani. Gonjwa hili halibagui wala kuchagua kati ya maskini na tajiri, wale wote wanaokumbana nalo “uso kwa uso wanakiona cha mtema kuni.” Jambo la kuhuzunisha ni kuona kwamba, kumekuwepo na pengo kubwa kati ya maskini na matajiri na ubaguzi umeongezeka maradufu. Changamoto ya Virusi vya Corona, COVID-19 inahitaji kwanza kabisa kupatiwa tiba muafaka, kwani Virusi vya Corona, COVID-19 hata kama ni vidogo kiasi gani vimeipigisha dunia magoti!

Baba Mtakatifu anasema, kirusi kikubwa zaidi kinachopaswa kuvaliwa njuga, ili hatimaye, kupatiwa tiba muafaka ni ukosefu wa haki jamii na fursa sawa; ubaguzi pamoja na ukosefu wa ulinzi kwa maskini na wanyonge katika jamii. Jibu makini linalotolewa mintarafu mwanga wa Injili ni kukataa katu katu uchoyo na ubinafsi; kwa kuonesha uzuri wa Injili unaotoa upendeleo na kipaumbele cha pekee kwa maskini, walio wadogo kabisa, wale ambao jamii inawatupilia mbali na kuwageuzia kisogo. Rej. EG. Namba 195.  Upendeleo kwa maskini si suala la kisiasa bali ni kiini cha Injili ambacho kinachota utajiri wake kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu na kama kiini cha Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa amesema, wasamaria na watu wenye mapenzi mema, wanaendelea kuitikia wito wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 hasa kwa kusaidia nchi maskini zaidi duniani. Takwimu za maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 nchini Brazil, hadi kufikia tarehe 20 Agosti 2020 majira ya saa 1: 30 za asubuhi, kulikuwa na watu milioni 3, 460, 413 walioambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19. Wagonjwa waliofariki dunia ni 11, 189. Waliolazwa hospitalini ni wagonjwa 2, 615, 254. Ni katika muktadha huu anasema Kardinali Konrad Krajewski, Baba Mtakatifu Francisko ameguswa sana na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Brazil na kuamua kuwapatia zawadi ya mashime 18 za kupumlia, kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa waliowekwa kwenye uangalizi maalum.

Huu ni msaada uliotolewa na Asasi ya kujitegemea ya “Hope Onlus” inayotekeleza dhamana na wajibu wake hasa katika sekta ya elimu na afya, kwa kutoa vifaa tiba ili kuokoa maisha. Utaratibu wa kugawa vifaa hivi kadiri ya mahitaji ya watu wa Mungu ni dhamana ambayo inatekelezwa na Ubalozi wa Vatican nchini Brazil, upendeleo wa pekee, ukiwa ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Papa: COVID-19 Brazil

 

20 August 2020, 13:05