Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amefafanua kuhusu muujiza wa Yesu kutembea juu ya maji kuwa ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo kwa wenye imani haba, hofu na mashaka katika maisha. Baba Mtakatifu Francisko amefafanua kuhusu muujiza wa Yesu kutembea juu ya maji kuwa ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo kwa wenye imani haba, hofu na mashaka katika maisha. 

Muujiza wa Yesu Kutembea Juu ya Bahari: Imani, Matumaini na Mapendo

Mungu anajifunua mbele ya waja wake kama sauti ndogo na yenye utulivu, inayomwalika mwamini kuisikiliza na wala haimlazimishi wala kumfunga mtu kuisikiliza. Hii ndiyo maana ya kuwa na imani thabiti wakati wa misukosuko ya maisha kwa kuhakikisha kwamba, mwamini daima moyo wake unamwelekea Mwenyezi Mungu, ili kuonja wema, huruma na upendo wake wa daima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Mathayo, Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa anamwonesha Kristo Yesu akitembea juu ya maji yaliyokuwa na mawimbi makali na upepo wa mbisho. Tukio hili linakuja mara baada ya Kristo Yesu kuwalisha watu zaidi ya elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipojitenga na kupanda mlimani faraghani, kwenda kusali. Huko akaunganika na Baba yake wa mbinguni. Mwinjili Mathayo anaendelea kusema, hata wakati wa zamu ya nne ya usiku, Kristo Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari wakafadhaika, wakisema ni kivuli, wakapiga yowe kwa hofu, mara Yesu akanena na kuwaambia “Jipeni moyo ni mimi msiogope.” Kama ilivyokuwa kawaida yake, Mtakatifu Petro, akamjibu, akasema “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Changamoto pevu! Yesu akamwambia, “Njoo”. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa, akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema “Bwana niokoe”. Mara Kristo Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, “Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?

Huu ni mwaliko na changamoto kwa kujiachilia na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, wakati wowote wa maisha, lakini kwa namna ya pekee, pale ambapo mwamini anakumbana na majaribu pamoja na misukosuko ya maisha. Pale, mwamini anapohisi ndani mwake woga na mashaka, kwa kudhani kwamba, sasa anazama kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, kamwe asiogope kupiga yowe kwa kusema, “Bwana niokoe”. Hii ni sala nzuri sana, itakayomwonjesha mwamini uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yake kwa kumnyooshea mkono na kumwokoa na hivyo kumpatia nafasi ya kuendelea kumtafakari Kristo, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu ambao kamwe hauwezi kumwacha mtu kuhangamia. Huu ni mkono wenye nguvu na uaminifu wa Baba wa milele anayewatakia watu wake mema daima. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 9 Agosti 2020.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu si mkatili kiasi cha kujifunua kama upepo mkali unaopasua milima na kuvunja miamba au tetemeko la ardhi au moto mkali, kama anavyosimulia Nabii Yeremia katika Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Kwanza cha Wafalme: 19: 9, 11-13. Mwenyezi Mungu anajifunua mbele ya waja wake kama sauti ndogo na yenye utulivu, inayomwalika mwamini kuisikiliza na wala haimlazimishi wala kumfunga mtu kuisikiliza. Hii ndiyo maana ya kuwa na imani thabiti wakati majaribu na misukosuko ya maisha kwa kuhakikisha kwamba, mwamini daima moyo wake unamwelekea Mwenyezi Mungu, ili kuonja wema, huruma na upendo wake wa daima. Hili ndilo fundisho kuu ambalo Kristo Yesu alipenda kumwachia Petro na Mitume pamoja na wafuasi wake katika nyakati hizi. Kristo Yesu anafahamu fika kwamba, imani ya waja wake ni dhaifu sana, kiasi kwamba, wafuasi wake wanaweza kupoteza dira na mwelekeo wa maisha, wanapokumbana na nguvu za upinzani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ndiye anayeweza kuwaokoa kwa sababu hata kabla ya kuanza kumtafuta katika shida na mahangaiko yao, daima Kristo Yesu yuko pamoja na kati ya wafuasi wake. Anapowasimamisha waja wake walioteleza na kuanguka, anawawezesha kupata neema ya kukuza na kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mashua au mtumbwi unaoteseka kwa mawimbi mazito na upepo wa mbisho ni kielelezo cha Kanisa ambalo kila nyakati linakumbana na upepo wa mbisho na hata wakati mwingine majaribu makubwa. Baba Mtakatifu anasema, kuna mifano hai ya madhulumu na nyanyaso dhidi ya Kristo na Kanisa lake katika karne ya ishirini. Ni katika muktadha huu, baadhi ya waamini wanaweza kuingiwa na kishawishi na kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu ameliacha na kulitelekeza Kanisa lake. Lakini ni katika hali na mazingira kama haya, ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake unang’ara kama kielelezo cha ushuhuda wa imani, upendo na matumaini.

Huu ni uwepo wa endelevu wa Kristo Mfufuka katika Kanisa lake na hivyo kuwakirimia Wakristo neema ya kusimama kidete kutangaza na kushuhudia imani yao kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Damu ya mashuhuda wa Kristo ni mbegu ya Wakristo wapya na matunda yake ni upatanisho na amani ulimwenguni kote! Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwaombea neema ya kudumu katika imani na upendo wa kidugu, wakati wanapokumbana na giza na dhoruba katika maisha yao kiasi hata cha kutaka kuvuruga imani yao kwa Mwenyezi Mungu.

Papa: Bahari

 

 

 

 

09 August 2020, 13:30