Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asema, mgogoro wa matumizi ya maji ya mto Nile unapaswa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya Sudan, Misri na Ethiopia kwa ajili ya mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko asema, mgogoro wa matumizi ya maji ya mto Nile unapaswa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya Sudan, Misri na Ethiopia kwa ajili ya mafao ya wengi.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Mgogoro wa Mto Nile Unahitaji Majadiliano ya Kweli!

Baba Mtakatifu anawaalika wadau wote wanaohusika na mgogoro wa matumizi ya maji ya Mto Nile yaani: Misri, Sudan na Ethiopia kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi, ili Mto Nile uendelee kuwa ni chemchemi ya uhai kwa kuwaunganisha watu na wala si kuwagawa pamoja na kuendeleza maboresho ya urafiki, maendeleo fungamani ya binadamu na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, Jumamosi tarehe 15 Agosti 2020, amesema kwamba, anafuatilia kwa umakini mkubwa mgogoro mkubwa wa Mto Nile kati ya Misri, Ethiopia na Sudan. Baba Mtakatifu anawaalika wadau wote wanaohusika na mgogoro huu, kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili Mto Nile uweze kuendelea kuwa ni chemchemi ya uhai kwa kuwaunganisha watu na wala si kuwagawa pamoja na kuendeleza maboresho ya urafiki, maendeleo fungamani ya binadamu na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa nchi hizi husika kuondokana na kishawishi cha kutaka kujenga uadui, hali ya kutoelewana au kinzani. Majadiliano yapewe kipaumbele cha kwanza kati ya Misri, Ethiopia na Sudan, kama njia pekee inayotafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya watu wao na ulimwengu katika ujumla wake.

Ujenzi wa mradi wa bwawa kubwa la kufua umeme linalojulikana kama “Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD), unaotekelezwa na Serikali ya Ethiopia kilometa 15 kati ya mpaka wake na Sudan, karibu sana na Ziwa Tana, ambao ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 60% hadi wakati huu, umekuwa ni chanzo cha mgogoro mkubwa wa kidiplomasia kati ya Ethiopia, Misri na Sudan ambazo zote ni watumiaji wakubwa wa maji ya Mto Nile. Itakumbukwa kwamba, asilimia 90% ya mahitaji ya maji nchini Misri yanayokana na Mto Nile, bila kuangalia matumizi yake viwandani na katika kilimo cha umwagiliaji. Huu ni mgogoro ambao unapata chanzo chake tangu mwaka 1929 na hatimaye mwaka 1959 Uingereza ikatunga sheria juu ya matumizi ya maji ya Mto Nile kwa Misri na Sudan. Uingereza ikaipatia Misri kura ya “veto” kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile. Hii ni sheria ambayo haina mashiko hata kidogo kwa Ethiopia.

Kutokana na kukua kwa haraka kwa: idadi ya watu na uchumi nchini Ethiopia, hitaji la umeme wa uhakika likawa ni kipaumbele cha kwanza kwa Ethiopia na hivyo kuamua kujenga bwawa la kufua umeme la “Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) litakaloweza kuzalisha umeme kwa mahitaji ya ndani na zaidi sana kuweza kuziuzia hata nchi jirani. Inakadiriwa kwamba, mradi huu hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya dola za kimarekani bilioni 4.6 na linatarajiwa kuzalisha umeme wa megawati 6, 000. Huu ni mgogoro ambao kwa miaka mingi umekuwa ukishughulikiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa makubaliano na sheria zifuatazo: Sheria ya “Helsink ya Mwaka 1996”; Makubaliano ya “Nile Basin Initiative, NBI” ya mwaka 1999, Makubaliano ya “Cooperative Framework Agreement”, CFA ya mwaka 2010 yaliyofanyika mjini Entebe, Uganda na Mwaka 2013 ikaundwa Tume ya Pamoja. Juhudi zote hizi hazikuweza kufua dafu kwa mgogoro uliokuwa unafukuta chini kwa chini. Mwaka 2017, Misri ikaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuiondoa Sudan katika mchakato wa majadiliano hayo.

Wazo hili likapingwa vikali na wadau katika mgogoro huu. Mabadiliko katika uongozi nchini Misri yamekuwa pia ni chanzo cha kuyumba kwa msimamo wake katika suala zima la matumizi ya maji ya Mto Nile. Upembuzi yakinifu uliofanywa kunako mwaka 2013 ulibaini athari kubwa za mazingira ambazo zingesababishwa na ujenzi wa bwawa hili kwa Sudan na Misri. Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Sudan na Misri kunako mwaka 2018 ukasua sua sana kiasi cha nchi hizi mbili kuanza “kutunishiana misuri” kwa kuweka majeshi yake mpakani mwa nchi hizi mbili. Katika sakata hili, Sudan inaonekana kuunga mkono juhudi za Serikali ya Ethiopia katika ujenzi wa bwawa hili na matokeo yake, Misri inaonekana kubaki ikiwa imesimama peke yake. Hatima ya sakata lote hili ni umuhimu wa pande zote zinazohusika kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi zao na ulimwengu katika ujumla wake, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Idadi ya wananchi wa Ethiopia inazidi kuongezeka maradufu wakati idadi ya wananchi wa Misri inapungua, kila kukicha.

Kumbe, Ethiopia inaonekana kuwa na hitaji kubwa la uhakika wa maji safi na salama pamoja na nishati ya umeme kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na ziada kuweza kuuzwa nchi za nje. Lakini, ikumbukwe kwamba, mgogoro huu ni tete unaweza kusababisha janga la ukosefu wa maji katika Ukanda wa Mto Nile na athari zake zikawa ni kubwa: kiuchumi, kisiasa na hata kukosekana kwa amani na utulivu. Maji ni uhai! Hii ni nishati ambayo inapaswa kutumiwa kwa uangalifu mkubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Chini ya mgogoro wa bwawa la Ethiopia kuna mataifa makubwa ambayo yamewekeza sana katika nchi hizi nayo ni: China, Marekani na Urussi.

Papa: Afrika

 

 

16 August 2020, 13:28