Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhtasari wa fadhila za Kimungu ambazo ni: imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhtasari wa fadhila za Kimungu ambazo ni: imani, matumaini na mapendo!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakita mizizi yake hasa katika misingi ya: haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuzingatia pia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kazi ya Uumbaji ambayo binadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Mzunguko Mpya wa Katekesi yake kuhusu: “Uponyaji wa Ulimwengu” kutoka kwenye Maktaba yake ya Binafsi, Jumatano, tarehe 5 Julai 2020, amewakumbusha waamini kwamba, binadamu wanapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi ili kujenga na kuboresha mazingira nyumba ya wote yanayoteseka kutokana na magonjwa makubwa, ili hatimaye, kujenga dunia iliyo bora zaidi. Hii ni dunia inayosimikwa katika Injili ya matumaini kwa vijana wa vizazi vijavyo. Katika kipindi hiki cha janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-16, Baba Mtakatifu, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Roho Mtakatifu, ili aweze kukuza ndani mwao fadhila ya imani, matumaini na mapendo.Hizi ni fadhila ambazo zinatoa dira na mwelekeo mpya, kwa kujikita katika kipaji cha ubunifu sanjari na kuwahamasisha kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa binadamu kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwenyezi Mungu anapenda binadamu wote waweze kuokolewa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali daima. Wajitahidi kuyatafakari na hatimaye, kujibidiisha kuyafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanafumbatwa katika utu wa binadamu, ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi; udugu wa kibinadamu na mshikamano; ushiriki wa watu katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati mintarafu mustakabali wa maisha yao kwa kuzingatia kanuni auni! Ni mafundisho yanayokita mizizi yake hasa katika misingi ya: haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuzingatia pia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kazi ya Uumbaji ambayo binadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu.

Huu ndio mwongozo rasmi wa maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata katika masuala ya kidini! Majadiliano hayana budi kuzingatia ukweli na uwazi bila ya kumezwa na kishawishi cha maamuzi mbele. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana; kwa kuheshimiana na kuthamianina hata katika tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, lengo ni kusaidia mchakato wa ukuaji wa Jumuiya inayosimikwa katika mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Papa: Mafundisho Jamii ya Kanisa

 

 

06 August 2020, 06:59