Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena, amewaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena, amewaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Sala Kwa Bikira Maria Dhidi ya Virusi Vya COVID-19

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza yake ya Kimama, ili aweze kuwasaidia binadamu kupambana kikamilifu, na hatimaye kupata ushindi dhidi ya janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Umoja na mshikamano; utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Salam na matashi mema kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema mara baada ya katekesi yake, Jumatano tarehe 12 Agosti 2020, amewakumbusha kwamba, Maandiko Matakatifu yanafundisha kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa upendo wake mkuu; amemuumba kwa sura na mfano wake. Hiki ndicho kiini cha utu na heshima ya binadamu, mwenye haki zake msingi. Kama binadamu ana uwezo wa kujifahamu, kumiliki, kujitoa huru, kujisadaka kwa kushirikiana na kujumuika na watu wengine ndani ya jamii. Nchi nyingi duniani zimemteuwa Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni kuwa ni msimamizi na mlinzi wa nchi zao kama ilivyo kwa Ufaransa.

Bikira Maria aendelee kuwaombea ili waamini waweze kuimarisha: imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kupambana na “ndago za uchoyo na ubinafsi”, ili kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na mshikamano wa kweli. Kwa wale wanaotembelea Madhabahu ya Bikira Maria, waendelee kuwa waangalifu dhidi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hija hizi za kiroho, uwe ni muda muafaka wa kutafakari kwa makini, kusali na kudumisha udugu wa kibinadamu katika imani na mapendo. Familia ya Mungu nchini Poland, tarehe 15 Agosti 2020 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Ushindi wa Muujiza wa Vistula. Haya ni mapambano makali ya silaha yaliyoanza kutimua vumbi tarehe 12-25 Agosti 1920 na hatimaye, Poland ikaibuka kidedea dhidi ya Urussi. Watu wa Mungu kutoka Poland, wakaona ushindi huu ni matunda ya sala, ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza yake ya Kimama, ili aweze kuwasaidia binadamu kupambana kikamilifu, na hatimaye kupata ushindi dhidi ya janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Tarehe 11 Agosti 2020 Mama Kanisa ameadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Clara wa Assisi, Mtawa, Bikira na Muasisi wa Mashirika la Watawa wa ndani. Alijenga urafiki wa dhati kabisa na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zake katika: ufukara, moyo wa unyenyekevu pamoja na kumtegemea zaidi Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Mtakatifu Clara awe ni kielelezo makini cha upendo kwa Mungu na jirani unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani. Wazee, vijana wa kizazi kipya, wagonjwa na wanandoa wapya, wawe na ujasiri wa kupambana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha, kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa njia ya sala na maombezi ya Bikira Maria. Mwishoni kabisa, Baba Mtakatifu anawaweka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, chini na tunza ya Bikira Maria katika hija ya maisha ya hapa duniani kuelekea katika utimilifu wa ahadi za Kristo Yesu.

Papa: Wito Maalum
12 August 2020, 12:45