Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asema, Ibada kwa Bikira Maria ni amana na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kitamaduni na kamwe isihusishwe na unahifu wa kitaifa na kimataifa unaokiuka misingi ya Injili. Baba Mtakatifu Francisko asema, Ibada kwa Bikira Maria ni amana na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kitamaduni na kamwe isihusishwe na unahifu wa kitaifa na kimataifa unaokiuka misingi ya Injili. 

Papa Francisko: Msihusishe Ibada ya Bikira Maria na Uhalifu Kitaifa!

Kuna haja ya kuondokana na Ibada kwa Bikira Maria zinazohusishwa na magenge ya kihalifu kitaifa na kimataifa kwa kuzingatia tunu msingi za Kiinjili zinazofumbatwa katika haki, ukweli, uaminifu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Hiki ni kiini cha barua ya Baba Mtakatifu Francisko aliyomwandikia Padre Stefano Cecchin, Rais wa Taasisi ya Elimu ya Bikira Maria Kimataifa mjini Roma,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada kwa Bikira Maria ni amana na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kitamaduni, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, utajiri huu unalindwa na kuendelezwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na Mama Kanisa. Kuna haja ya kuondokana na Ibada kwa Bikira Maria zinazohusishwa na magenge ya kihalifu kitaifa na kimataifa kwa kuzingatia tunu msingi za Kiinjili zinazofumbatwa katika haki, ukweli, uaminifu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa muhtasari hiki ndicho kiini cha barua ya Baba Mtakatifu Francisko aliyomwandikia Padre Stefano Cecchin, Rais wa Taasisi ya Elimu ya Bikira Maria Kimataifa mjini Roma, ambayo tarehe 18 Septemba 2020 imeandaa kongamano kama kielelezo cha ufunguzi wa Idara mpya katika taasisi hii, itakayokuwa inajihusisha na upembuzi yakinifu kuhusu matukio ya magenge ya kihalifu kitaifa na kimataifa yanayohusianishwa na Ibada kwa Bikira Maria. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Ibada kwa Bikira Maria zinaondolewa katika magenge haya ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha kweli na tunu msingi za Kiinjili.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa kufikiria na hatimaye kuanzisha Idara mpya itakayowahusisha wadau mbali mbali ndani na nje ya Kanisa, ili kusaidia mchakato wa kutoa mapendekezo muhimu yatakayosaidia kuunda, kulea na kukuza dhamiri nyofu kwa kujikita katika hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya kihalifu kitaifa na kimataifa. Huu ni mwelekeo, mwono, programu na mbinu mkakati mpya mintarafu Ibada kwa Bikira Maria inayogusa maisha na undani wa watu wa kawaida. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: Bikira Maria Mama wa Mungu katika Fumbo la Kristo na Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanaangalia dhima ya Bikira Maria katika mpango wa wokovu mintarafu Agano la Kale, Bikira Maria katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na katika maisha ya Kristo Yesu. Bikira Maria na Kanisa katika kazi ya ukombozi, mwombezi kwa ajili ya wokovu na Bikira Maria kama mfano wa utimilifu wa Kanisa ambalo pia ni Bikira na Mama.

Kumbe, Kanisa linapaswa kuuiga utakatifu wa Bikira Maria. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unabainisha Ibada kwa Bikira Maria katika Kanisa: tabia na msingi wake pamoja na kanuni za kichungaji. Bikira Maria ni ishara na tumaini thabiti na ya faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri. Baba Mtakatifu Francisko katika mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium” anapenda kukazia utekelezaji wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Madhabahu ni mahali muafaka na mlango wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya  utimilifu na utakatifu wa maisha. Ni vituo vya sala, toba na wongofu wa ndani. Madhabahu ni mahali muafaka panapowasaidia waamini  kupyaisha ari na moyo wa utume ndani ya Kanisa, kwa kujikita zaidi katika maisha ya kijumuiya!

Ni maeneo yanayodhihirisha ufunuo wa: ukuu, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake, mafundisho msingi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Hapa kipaumbele cha kwanza ni uwepo wa Mungu ndani ya Kanisa na katika maisha ya kila mwamini. Waamini wajizoeshe kusali na kuimba Zaburi sanjari na maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Ikumbukwe kwamba, mchakato mzima wa uinjilishaji unarutubishwa kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Madhabahu pawe ni kimbilio la maskini wa: kiroho na kimwili; hapa pawe ni mahali ambapo mwamini anatambua na kuonja nguvu ya Mungu inayoponya na kuokoa! Kwa hakika madhabahu ni mahali muafaka pa kukuza na kudumisha Ibada safi kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Padre Stefano Cecchin, Rais wa Taasisi ya Elimu ya Bikira Maria Kimataifa mjini Roma, katika mahojiano maalum na Vatican News, anasema kuna haja ya kuwaokoa waamini wenye imani dhaifu wanaovutwa kiurahisi kwa miujiza, ili kukabiliana na shida pamoja na changamoto za maisha mintarafu magonjwa, ukata na hali ngumu ya uchumi pamoja na wasi wasi kutokana na matatizo katika maisha. Taasisi hii itashirikiana kwa karibu sana na viongozi wa Kanisa, Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Malezi na Katekesi makini na endelevu kuhusu tunu msingi za maisha ya Kikristo ni muhimu sana ili kuwaokoa waamini wanaotumbukizwa katika magenge ya kiuhalifu kwa sababu ya hofu, wasi wasi na imani haba. Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Taasisi ya Elimu ya Bikira Maria Kimataifa mjini Roma kuwa ni mahali pa kuwakutanisha watu; jukwaa la majadiliano katika ukweli na uwazi hata katika kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, waamini wanasaidiwa kukuza na kudumisha Ibada safi kwa Bikira Maria pamoja na kuwa na uelewa sahihi wa mafundisho mbali mbali yanayotolewa na Mama Kanisa. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya wajanja wachache wanaotaka kutumia shida, mahangaiko na matatizo ya baadhi ya watu kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi.

Papa Barua: Ibada B. Maria

 

 

22 August 2020, 13:57