Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni donda ndugu katika mwili wa binadamu katika ulimwengu mamboleo! Anawashukuru wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa waathirika. Papa Francisko: Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni donda ndugu katika mwili wa binadamu katika ulimwengu mamboleo! Anawashukuru wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa waathirika. 

Papa: Biashara ya Binadamu Ni Kashfa na Donda Ndugu!

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni donda ndugu katika mwili wa binadamu katika ulimwengu mamboleo. Anapenda kutumia fursa hii, kuwashukuru wale wote wanaoendelea kusimama kidete ili kuwasaidia na kuwahudumia wahanga wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Umoja na mshikamano ni muhimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2020 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Hii siku iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2013 ili kusaidia juhudi za kimataifa za kuragibisha athari za biashara hii katika maisha ya binadamu, haki msingi, utu na heshima yake. Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya viungo vya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, tarehe 30 Julai 2020 anasikitika kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni donda ndugu katika mwili wa binadamu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kuwashukuru wale wote wanaoendelea kusimama kidete ili kuwasaidia na kuwahudumia wahanga wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Kuna hatua kubwa ambazo zimekwisha kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa, lakini, bado kuna haja ya kuendelea kupambana ili hatimaye, kashfa hii dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu iweze kufutika machoni pa uso wa dunia! Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 alipokuwa anahutubia kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati katika kupambana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mapambano haya lazima kwanza kabisa yalinde na kuheshimu: utu na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Pili ni kwa kusimama kidete kupambana na umaskini wa hali na kipato na tatu ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vatican daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na biashara haramu ya binadamu ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuridhia Itifaki ya Umoja wa Mataifa katika mchakato wa kupambana na biashara haramu ya binadamu, kwani ni biashara inayowanyanyasa watu wengi zaidi. Ndiyo maana Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliwataka viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha utashi wa kisiasa katika mapambano haya.

Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake mbali mbali limeendelea kujipambanua kuwa ni kati ya wadau wakuu wanaopambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na kuwasaidia waathirika ili waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida. Utumwa mamboleo unaendelea kukua na kukomaa, kumbe, unahitaji watu kulitambua hilo na kuchukua hatua madhubuti, hii ikiwa ni pamoja na kubadili mtindo wa maisha. Ikumbukwe kwamba, mafanikio katika maisha yanapatikana kwa juhudi na maarifa, kwa kujinyima na kujiwekea malengo thabiti. Serikali mbali mbali zinapaswa pia kujizatiti katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kuwapatia mahitaji msingi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, ndiyo maana kunako mwaka 2015 alipokuwa anazungumza na mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi na mashirika mbali mbali mjini Vatican aliwataka kuhakikisha kwamba, wanasaidia katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Ni katika muktadha huu, Kikundi cha Mtakatifu Martha kilianzishwa katika jitihada hizi za Baba Mtakatifu Francisko kuwahusisha wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo! Baba Mtakatifu hivi karibuni akizungumza na wajumbe wa RENATE, yaani Mtandao wa Mashirika ya Kitawa Kimataifa katika Mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu. Utumwa mamboleo ni matokeo ya umaskini, ukosefu wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; ubaguzi na ukosefu wa elimu, fursa za ajira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kumbe, hata utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya utumwa mamboleo na kwamba, huu ni utashi wa kimaadili unaopaswa kufanyiwa kazi na wadau mbali mbali duniani. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2015, Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na kashfa ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo, alianzisha Siku ya Kupambana na Biashara ya binadamu na Utumwa Mamboleo ndani ya Kanisa Katoliki inayoadhimishwa tangu wakati huo, tarehe 8 Februari, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Josephine Bakhita, aliyetekwa nyara kutoka Sudan, akakombolewa na hatimaye, akabatizwa na kuwa mtawa!

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu, UNODC inasema, asilimia 71% ya waathirika wote ni wanawake na watoto. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 usiwe ni kisingizio cha kushindwa kuwahudumia waathirika wa biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kuunda na kujenga mitandao ya kijamii itakayosaidia kudumisha ulinzi na usalama na waathirika, kwa kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao msingi sanjari na msaada wa huduma ya afya, kisheria na kisaikolojia, ili kuwasindikiza hatua kwa hatua katika mchakato wa kuandika tena historia mpya ya maisha yao. Wakimbizi, wahamiaji na wafanyakazi wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika sekta isiyokuwa rasmi, wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi ya kuweza kutumbukizwa katika biashara na mifumo ya utumwa mamboleo.

Caritas Internationalis inawataka viongozi wa Serikali mbali mbali kuhakikisha kwamba, wahanga hawa wanatendewa haki pamoja na kupatiwa huduma msingi kwa ajili ya maisha yao. Watoto walindwe dhidi ya nyanyaso za kijinsia pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; nyanyaso zinazo tekelezwa kwenye internet na mitandao ya kijamii. Hii ni dhamana ya watu wote wenye mapenzi mema kuwa macho na makini dhidi ya wale wote wanaotaka kuendeleza biashara na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Papa: Utumwa mamboleo 2020

 

30 July 2020, 13:20