Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa wanachama wa Chama Cha Wanaharakati Wasiokuwa na Ardhi Vijijini nchini Brazil. Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa wanachama wa Chama Cha Wanaharakati Wasiokuwa na Ardhi Vijijini nchini Brazil. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Wanaharakati Wasiokuwa na Ardhi

Papa Francisko anawapongeza wanaharakati hawa kwa kuendelea kujizatiti katika shughuli za umoja, upendo na mshikamano kwa ajili ya mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na mardhi nchini Brazil. Wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuwagawia waathirika mahitaji yao msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wafanyakazi Vijijini Nchini Brazil imeadhimishwa tarehe 25 Julai 2020. Kardinali Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe wa matumaini na mshikamano na Wanachama wa Chama cha Wanaharakati Wasiokuwa na Ardhi vijijini huko nchini Brazil yaani: “Il Movimento dos Trabalhadores Rurais Sem Terra, MST”. Hiki ni kikundi cha harakati za kisiasa na kijamii, kinachopania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mapinduzi kwenye sekta ya kilimo nchini Brazil. Lengo ni kuondokana na ukoloni mamboleo unaoyamilikisha makampuni makubwa ya kigeni sehemu kubwa ya ardhi, wakati wananchi wa kawaida wanaambulia patupu! Wanaharakati wanataka ardhi igawanywe sawa na kuwa na umiliki sawa wa ardhi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Wanaharakati wanataka mageuzi katika mfumo wa elimu na mambo ya kisiasa na kwamba, haya ni mapambano yanayowaunganisha watu wote nchini Brazil. Takwimu zinaonesha kwamba, Chama cha Wanaharakati Wasiokuwa na Ardhi vijijini kina zaidi ya wanachama milioni 1. 5 walioenea sehemu mbali mbali za Brazil. Kuna vyama vya ushirika vipatavyo 100 na viwanda vya kilimo ni 96. Ni katika muktadha huu, Kardinali Michael Czerny, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwapongeza wanaharakati hawa kwa kuendelea kujizatiti katika shughuli za umoja, upendo na mshikamano kwa ajili ya mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na mardhi nchini Brazil. Wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuwagawia waathirika mahitaji yao msingi. Janga hili limesababisha maafa makubwa hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali.

Sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu ni matunda ya tafakari ya kina kuhusu kazi ya uumbaji inayomwajibisha mwanadamu kuilinda, kuitunza na kuiendeleza kama njia inayofaa kwa ajili ya kuheshimu kazi ya uumbaji na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumba mwenyewe! Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na mwelekeo wa Kiekaristi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kutambua kwamba, kazi ya uumbaji ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitunza na kuiendeleza. Kumbe, anao wajibu wa kushirikishana zawadi hii na jirani zake, ili watu wengi zaidi waweze kupata furaha kwa kushiriki matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa heshima na nidhamu unadai mchakato wa kufunga na kujinyima, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni changamoto ya kujikita katika wongofu wa kiekolojia unaowataka watu wa Mungu kuondokana na tabia ya uchoyo pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa dunia, kwa kuanza kujenga na kudumisha ekolojia kwa heshima na nidhamu; umoja na mshikamano wa dhati. Muujiza wa Yesu wa kuwalisha watu elfu tano, kwa mikate mitano na samaki wawili kama unavyosimuliwa na Mwinjili Marko 6: 34-44 ni changamoto ya kushirikishana na kushikamana kama chachu ya maisha mapya yanayofumbatwa katika mchakato wa ujenzi wa mafungamano na udugu wa kibinadamu; chachu muhimu sana katika kuleta mabadiliko ya kijamii.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, ukarimu huu, utawachangamotisha wananchi na makundi mbali mbali ya kijamii kujitosa bila ya kujibakiza kwa sababu Mwenyezi Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. Rej. 2 Kor 9:7. Baba Mtakatifu anawaalika wanachama hawa kumshukuru Mungu na kumwomba ili aendelee kubariki kazi ya mikono yao, familia na walengwa wote watakaotumia msaada huu. Roho Mtakatifu Mfariji awalinde dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Awakirimie moyo wa ujasiri na matumaini katika kipindi hiki kigumu cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awabariki wakulima wote wanaoendelea kujisadaka katika mchakato wa ujenzi wa upendo na mshikamano sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Papa: Wakulima Vijijini
29 July 2020, 13:07