Tafuta

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, makubaliano ya Donbass yaliyofikiwa huko Minsk yatatekelezwa kwa vitendo, ili Ukraine iweze kupata amani ya kudumu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, makubaliano ya Donbass yaliyofikiwa huko Minsk yatatekelezwa kwa vitendo, ili Ukraine iweze kupata amani ya kudumu. 

Papa: Makubaliano ya Donbass Yalete Amani Nchini Ukraine

Papa: Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na zoezi la kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini pamoja na udhibiti wa silaha. Ni kwa njia ya mchakato huu, wadau mbali mbali katika mgogoro huu, wataweza kujengeana imani na matumaini kama msingi wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa; mambo msingi ambayo watu wa Mungu nchini Ukraine wanayasubiri kwa hamu kubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 26 Julai 2020 ameonesha furaha yake baada ya makundi yanayohusika na mgogoro wa kivita huko nchini Ukraine kufikia uamuzi wa kusitisha mapambano ya silaha, kuanzia tarehe 21 Julai 2020. Makubaliano haya ya Donbass yamefikiwa huko Minsk. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote walioshiriki katika kufikia makubaliano haya yanayoonesha utashi mwema wa kutaka kusitisha vita, ili amani iweze kutawala tena miongoni mwa watu wa Mungu nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anasali na kumwomba Mwenyezi Mungu, ili makubaliano haya yaweze kutekelezwa kwa vitendo. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na zoezi la kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini pamoja na udhibiti wa silaha.

Ni kwa njia ya mchakato huu, wadau mbali mbali katika mgogoro huu, wataweza kujengeana imani na matumaini kama msingi wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa; mambo msingi ambayo watu wa Mungu nchini Ukraine wanayasubiri kwa hamu kubwa! Itakumbukwa kwamba, kunako mwezi Februari 2015 Mkataba wa II wa Minsk ulitiwa mkwaju, ili kutegua mabomu yaliyokuwa yametegwa ardhini pamoja na kuondokana na mapambano ya kivita, ili hatimaye, misaada ya kiutu, iweze kuwafikia walengwa. Wachunguzi wa mambo ya kivita wanasema, mapambano ya silaha nchini Ukraine, yamesababisha watu zaidi ya 13, 000 kupoteza maisha pamoja na watu milioni 3 kukosa makazi ya kudumu hasa katika eneo la mikoa ya mashariki mwa Luhansk na Donetsk tangu mwaka 2014 licha ya Mkataba wa kusitisha mapambano ya silaha huko Minsk kuchapishwa.  

Kumbe, Makubaliano haya ya Donbass yaliyofikiwa huko Minsk na utekelezaji wake kuanza tarehe 21 Julai 2020 ni mwaliko wa kuachana na mapambano ya silaha nzito na yale ya kushitukiza. Kwa sasa ni marufuku kushambulia miundombinu kama vile majengo ya shule, hospitali na ofisi za umma. Makubaliano haya yanapaswa kutekelezwa kwa dhati bila masharti yoyote. Viongozi wakuu wa Serikali ya Urussi na Ukraine, wamepongeza hatua hizi ambazo zimefikiwa ili kurejesha tena amani na utulivu nchini Ukraine. Mazungumzo haya yamezihusisha nchi za: Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Ukraine.

Papa: Amani Ukraine
27 July 2020, 13:02