Tafuta

Vatican News
Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Julai 2020: Ulinzi wa Familia. Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Julai 2020: Ulinzi wa Familia. 

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Julai 2020: Ulinzi wa Familia

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Julai 2020, anazielekea familia ambazo hazina budi kulindwa hasa katika nyakati hizi ambazo kuna matatizo na changamoto pevu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuzialika Serikali kulinda na kuzidumisha familia sanjari na kuzisindikiza kwa upendo, heshima pamoja na kuwa na mwongozo imara. Familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tangu mwanzo amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa familia, kwa kutambua kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumba “Domus ecclesiae”, shule ya upendo, huruma, haki, ukarimu na utakatifu wa maisha. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana, kutegemezana na kukamilishana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, inayofumbatwa katika Injili ya uhai, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zinavyobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi, kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu: Maandiko Matakatifu, Mafundisho ya Kanisa na Utu wema! Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Julai 2020, anazielekea familia ambazo hazina budi kulindwa hasa katika nyakati hizi ambazo kuna matatizo na changamoto pevu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuzialika Serikali kulinda na kuzidumisha familia sanjari na kuzisindikiza kwa upendo, heshima pamoja na kuwa na mwongozo imara. Hali halisi ya familia katika ulimwengu mamboleo imebadilika kwa kiasi kikubwa, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa miaka kadhaa iliyopita. Huu ni wakati ambapo familia nyingi zimezama katika tamaduni, kiasi cha kukosa muda kwa mambo msingi ya kifamilia. Kwa mfano utekelezaji wa majukumu ya kazi, kwani baadhi ya familia kimekuwa ni kikwazo kikubwa. Leo huu mawasiliano ya kidigitali mkondoni yamechukua nafasi ya upendo mubashara ndani ya familia.

Familia nyingi zinajikuta zikiwa zimezama katika upweke hasi na huko zinateseka na kulalama katika hali ya kimya kikuu na mateso. Katika kipindi hiki cha kipeo cha janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kuna wanafamilia ambao wamepoteza fursa za ajira na wengine bado inawawia vigumu kupata fedha ya kuweza kujikimu. Familia ni uti wa mgongo katika ustawi na maendeleo ya jamii. Ni katika muktadha huu, Serikali zinawajibika kuibua sera na mikakati itakayosimama kidete kuzilinda familia. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video anaendelea kudadavua kwamba, hali hii ni kati ya matatizo na changamoto za hatari sana ambazo familia zinakumbana nazo katika ulimwengu mamboleo. Kuna mambo madogo madogo ambayo yanaweza pia kujenga furaha, amani na matumaini ndani ya familia, kwa wazazi kutenga muda wa kukaa, kucheza na kuzungumza na watoto wao.Ni katika hali na mazingira haya, Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kukuza na kudumisha utume wa familia, kwa kuzisaidia kwa hali na mali, pamoja na kuibua mbinu mkakati utakaoziwezesha familia kuvuka matatizo na changamoto hizi, hadi kutua nanga katika bandari salama.

Kwa upande wake, Padre Frédéric Fornos S.J., Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anakiri kwamba, bado kuna watu wengi sehemu mbali mbali za dunia, wanaendelea kuathirika kutokana na janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna familia ambazo zinamahitaji makubwa na baadhi yao hazina uhakika wa fursa za ajira kwa siku za usoni. Wote hawa wanapaswa kusindikizwa kwa huruma na upendo. Ikumbukwe kwamba, familia ni msingi wa ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu, kumbe zinapaswa kusaidiwa ili ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya jamii. Familia si jambo la mtu binafsi bali ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa jamii. Kuliko nyakati nyingine zozote zile katika historia ya mwanadamu, familia katika ulimwengu mamboleo zinapaswa kuungwa mkono, kuimarishwa na kusindikizwa kwa upendo, kwa kuheshimiwa na kupewa mwongozo thabiti.

Kumbe, kwa waamini kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuombea familia, ni kuungana pamoja katika safari ya huduma mintarafu familia. Huu ni mwaliko wa kuendelea kuunga mkono vyama na mashirika ya kitume yanayojitanabaisha kwa ajili ya utume wa familia, kujizatiti kuzisaidia familia hizi katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha ya binadamu. Padre Frédéric Fornos S.J., Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, sala ya kweli ni ile inayofumbatwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Mwezi Julai, iwe ni fursa kwa wanafamilia kujikita zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia! Bila shaka watu kwa sasa wanafahamu maana ya familia katika undani wake.

Papa: Nia Julai: familia
03 July 2020, 13:54