Tafuta

Vatican News
2020.07.22 Papa Francisko huko aRio de Janeiro 2013 katika siku ya Vijana duniani.Misa ilifanyika Copacabana 2020.07.22 Papa Francisko huko aRio de Janeiro 2013 katika siku ya Vijana duniani.Misa ilifanyika Copacabana 

Ni miaka 7 tangu Papa afanye ziara huko huko Rio de Janeiro katika Siku ya Vijana!

Ilikuwa ni tarehe 22 Julai 2013,yaani miaka saba iliyopita ambapo Papa Francisco alianza ziara yake ya kwanza kimataifa ya kitume ili kushiriki Siku ya Vijana Duniani huko Rio,nchini Brazil. Wito wake wa nguvu ulikuwa ni kuwataka vijana wampeleke Kristo ulimwenguni,bila kuogopa kwa utambuzi kwamba imani ni mapinduzi ya kweli duniani ambayo inabadili mioyo.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Miaka saba iliyopita Papa Francisko alifanya ziara yake ya kitume ya kwanza kimataifa nchini Brazili, katika fursa ya Siku ya 28 ya vijana duniani iliyoanza tarehe (22-29 Julai 2013).  Mada iliyokuwa inaongoza siku ya vijana ilikuwa imefikiriwa na Papa Mstaafu Benedikto XVI” isemayo  Enendeni na kuwa wafuasi kwa watu wote.” Na ndiyo maneno hayo ya Papa Fracisko aliyoanza nayo katika afla ya kukaribishwa kwenye Bustani la Jumba Kuu la Guanabara  huko Rio de Janeiro nchini Brazil. "Mimi sina dhahabu wala shaba lakini ninaleta kile chenye thamani kubwa ambacho nimepewa na Yesu Kristo", alisema Papa.

Kitovu ni Yesu kila kitu kianzie kwake

Katika sherehe ya kukaribishwa kwenye  fukwe za Copacabana, Papa Francisko aliwasa vijana kuwa imani ni mapinduzi kwa sababu  katikati hauwekwi umimi, bali Kisto, na kila kitu kianzie kwake! Mara nyingi sisi tunashawishika kutaka kuwa kitovu cha ulimwengu, kuamini kuwa ni sisi peke yetu wa kujenga maisha yetu binafsi au kufanya yawe yenye furaha au kumiliki, kuwa na mali na madaraka.

Imani, matumaini na upendo

Lakini hayo yote Papa Francisko alisema, "tutambue kwamba siyo hivyo". Kwa uhakika kuwa na mali na madaraka vinaweza kukupatia hali ya juu, hasa ya kudanganywa kwamba una furaha, lakini mwisho wake ndiyo yanayo kusukuma daima kutafuta zaidi bila kutosheka.  Papa Francisko  aliwaachia ushauri wa kumweka Kristo katikati ya maisha yao na kusimika imani yao kidete kwake Yeye peke yake,  kwa maana hawatadanganyika katika maisha yao, yaani wawe na matumai pia kuwa upendo mkuu kwa Kristo na kwa jirani!

Kazi ya kichungaji ni kuwa waaminifu kwa Yesu

Akiadhimisha misa Takatifu na maaskofu,  mapadrena  na watawa, aliwaalika kutoka nje ya maparokia yao, katika taasisi zao ili kutangaza Kristo bila kujidai, kueneza Injili na kuwa wahudumu wa muungano na utamadunu wa kukutana. Kazi ya kichungaji siyo ubunifu,  siyo mikutano au mipango ambayo inahakikisha matunda, hapana bali ni kuwa  waaminifu kwa Yesu, na  ambao wote wanaitwa kutafakari, kuabudu na kukumbatia kupitia sala, kukutana kila siku na Ekaristi takatifu na kwa watu wenye kuhitaji sana msaada.

Kukaa na Kristo haina maana ya kujitenga bali kukutana na wengine

Aidha Papa Francisko alisema kukaa na Kristo siyo kujitenga peke yako, bali ni kukaa kwa  ajili ya kukutana na wengine. Alihimiza kuwasaidia vijana wagundue kwamba kuwa wanafunzi wa umisionari ni matokeo ya kubatizwa, ni sehemu muhimu ya kuwa Mkristo na kwamba nafasi ya kwanza ya kuinjilisha ni ndani ya nyumba yao, masomo yao au mazingira ya kazini, familia na marafiki. Na uwasikiliza vijana, maswali yao wanapokuwa kwenye shida, kiukweli, unahitaji muda wa kukaa  pamoja nao!

Vijana wawe wanariadha wa kweli  wa Kristo

Wakati wa mkusanyiko wa mkesha wa Siku ya Vijana Duniani uliofanyika katika forodha ya Copacabana, alitoa wito kwa vijana wawe wanariadha wa kweli wa Kristo. Papa alisema “ Cheza kwenye timu yako. Ninyi mko kwenye uwanja wa imani! Ni wajenzi wa Kanisa nzuri zaidi na ulimwengu bora. Ninaomba tafadhali muache Kristo na Neno lake liingie katika maisha yenu na linaweze kuota na kukua. Msiangushe mbegu nje ya uwanja na kuacha kupeperushwa na mambo ya kijujuu tu, msikose msimamo mbele  ya matatizo ambayo yanaondoa ujasiri wa kwenda kinyume au kukimbilia vishawishi hasi.

22 July 2020, 13:35