Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asema kuhusu mifano ya Ufalme wa mbinguni, Kristo Yesu ni hazina iliyofichika ambayo waamini wanapaswa kuitafuta kwa hali na mali. Baba Mtakatifu Francisko asema kuhusu mifano ya Ufalme wa mbinguni, Kristo Yesu ni hazina iliyofichika ambayo waamini wanapaswa kuitafuta kwa hali na mali. 

Papa Francisko: Ufalme wa Mungu: Kristo Yesu, Hazina Iliyofichika!

Kwa mwamini aliyebahatika kupata hazina hii, ana moyo unaosimikwa katika kipaji cha ubunifu kwa kuendelea kuchakarika usiku na mchana, si kwa kujenga marudio, bali kutengeneza mambo mapya yanayomwezesha kuwa na dira na mwongozo wa maisha unaowawezesha waamini kumpenda Mungu na jirani zao pamoja na kujipenda wao wenyewe. Kristo Yesu ni hazina iliyofichika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Mathayo katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa anabainisha kwamba, Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika; Umefanana na mfanya biashara mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoiona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua na kwamba, Ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya wa kila aina. Rej. Mt. 13:44-52. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 26 Julai 2020 ametafakari kuhusu mifano miwili ya Ufalme wa mbinguni inayofananishwa na hazina iliyositirika na lulu nzuri na yenye thamani kubwa. Kwa wale wote wanaogundua hazina na lulu hii nzuri, wanauza vyote walivyo navyo na kwenda kuinunua hazina hii ambayo kwa sasa imekita mizizi yake katika sakafu ya nyoyo zao.

Kwa mifano hii miwili anasema Baba Mtakatifu Francisko, anaonesha jinsi ambavyo Kristo Yesu anataka kuwashirikisha waja wake katika ujenzi wa Ufalme wa mbinguni, kwa kujitosa kinaga ubaga bila hata ya kujiachilia hata kidogo, kwa kuuza vyote na kuanza kuchanja mbuga ili kuweza kuinunua hazina hii na hivyo kuondokana na usalama waliokuwa wamejiwekea katika mali za ulimwengu huu. Ujenzi wa Ufalme wa mbinguni unahitaji neema na ushiriki mkamilifu wa kila mwanadamu. Mifano ya watu hawa wawili katika Injili ya leo  ni kielelezo makini cha maamuzi magumu waliyofanya. Kwa furaha kubwa, wote wawili wakafanikiwa kupata hazina na lulu iliyokuwa imefichika. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuiga mfano wa hawa watu wawili wanaosimuliwa katika Injili ya Mathayo, ili hata wao waweze “kuchakarika usiku na mchana” ili kutafuta hazina ya Ufalme wa mbinguni.

Hii ni changamoto ya kuondokana na “blanketi zito” la uhakika wa usalama wa maisha yao, unaowafanya kutojishughulisha na mchakato wa kutafuta hazina na ujenzi wa Ufalme wa mbinguni. Leo hii kuna kishawishi kikubwa cha kumiliki vitu, kiu na uchu wa fedha na mali; madaraka pamoja na ubinafsi unaowafanya watu kujifikiria wao wenyewe. Katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna watu ambao wamekata tamaa kwa sababu wameteseka kutafuta hazina ya kweli katika maisha, lakini wakaishia kuvutwa na mng’ao wa mambo ya nje na mambo mpito ambayo yameacha giza totoro lisilokuwa na mwanga hata kidogo. Ufalme wa mbinguni ni kinyume chake kwani unakita mizizi yake katika mambo msingi ya maisha; amana na utajiri unaopyaisha maisha ya kila siku na kumwongoza mwamini katika mwono na upeo mpana zaidi. Kwa mwamini aliyebahatika kupata hazina hii, ana moyo unaosimikwa katika kipaji cha ubunifu kwa kuendelea kuchakarika usiku na mchana, si kwa kujenga marudio, bali kutengeneza mambo mapya yanayomwezesha kuwa na dira na mwongozo wa maisha unaowawezesha waamini kumpenda Mungu na jirani zao pamoja na kujipenda wao wenyewe.

Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, hazina na lulu iliyofichika ni Kristo Yesu, chemchemi ya furaha ya kweli ulimwenguni, furaha inayomwezesha mwamini kutambua maana ya maisha yake na kuwa ni chachu ya kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafuta usiku na mchana hazina ya Ufalme wa mbinguni, ili kwa njia ya maneno na matendo yao, yaoneshe na kushuhudia upendo wa Mungu aliowapatia kwa njia ya Kristo Yesu.

Papa: Ufalme wa Mbinguni
26 July 2020, 14:38