Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao! Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao!  (AFP or licensors)

Jengeni Utamaduni wa Kusoma na Kutafakari Neno la Mungu!

Baba Mtakatifu amewataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao. Wajenge mazoea ya kutembea na Biblia Takatifu, ili kujipatia muda wa kulisoma. Neno la Mungu ili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa inategemea sana mahali itakapoangukia. Ikiangukia kwenye udongo mzuri itazaa matunda mengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 12 Julai 2020, amefananua kuhusu sehemu ya Injili ya mpanzi kama ilivyoandikwa na Mathayo 13:1-23. Hii ni sehemu ya Injili inayogusia kuhusu: mifano ya Ufalme wa Mungu na sababu ya Kristo Yesu kufundisha kwa mifano pamoja na ufafanuzi uliotolewa na Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Baba Mtakatifu katika tafakari yake, amesema, Neno la Mungu ni Yesu mwenyewe na kuna njia mbali mbali za kuweza kumpokea Yesu katika maisha na kwamba, mfano wa mpanzi ni nguzo na “mama ya mifano yote” iliyotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake kwa sababu unazungumzia kuhusu usikivu wa Neno la Mungu. Baba Mtakatifu amewataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yao. Wajenge mazoea ya kutembea na Biblia Takatifu, ili kujipatia nafasi ya kusoma kidogo kidogo sehemu ya Maandiko Matakatifu. Neno la Mungu ili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa inategemea sana mahali itakapoangukia. Ikiangukia kwenye udongo mzuri itazaa matunda mengi.

Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu ni Neno wa Baba wa milele aliyemwilishwa tumboni mwa Bikira Maria. Kumbe, kulipokea Neno la Mungu, maana yake ni kumpokea Kristo Yesu. Kuna njia mbali mbali za kuweza kulipokea Neno la Mungu. Mosi, waamini wanaweza kulipokea Neno la Mungu kama zile mbegu zilizoanguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila. Tabia ya watu kutokuwa makini ni kati ya changamoto kubwa zinazomkabili mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Watu wengi wanapoteza dira ya maisha kutokana na umbea na mambo ya siasa hali ambayo inawafanya wakati mwingine, kukosa mwelekeo sahihi wa maisha hata ndani na nje ya familia zao. Ni katika muktadha huu, anasema Baba Mtakatifu, watu wanaweza kukosa hata nafasi ya ukimya na tafakari katika maisha yao; muda wa kujadiliana na Mwenyezi Mungu, hali ambayo inaweza hata kuhatarisha imani. Pili, waamini wanaweza kulipokea Neno la Mungu, kama ilivyokuwa kwa zile mbegu zilizoangukia penye miamba pasipokuwa na udongo mwingi, mara zikaota, kwa udongo kukosa kina na jua lilipozuka ziliungua.

Hawa ni wale waamini wanaolipokea Neno la Mungu kwa furaha na bashasha, lakini furaha hii inadumu kwa kitambo kidogo. Kwa waamini kama hawa wanapokabiliwa na matatizo, changamoto, mateso na madhulumu katika maisha, imani ambayo haikuwa imezama katika undani wa maisha ya mtu, inanyauka na kutoweka kama mbegu iliyoanguka penye miamba! Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Tatu, waamini wanaweza kulipokea Neno la Mungu kama mbegu zile zilizoanguka kwenye miiba, ile miiba ikamea ikazisonga. Huu ni uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka; mafanikio, hofu na wasiwasi katika ulimwengu mamboleo. Katika hali na mazingira ya namna hii, Neno la Mungu kamwe haliwezi kuzaa matunda yanayokudusiwa kwa sababu limezongwa na mambo mengi. Mwishoni, waamini wanaweza kulipokea Neno la Mungu kama zile mbegu zilizoanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini na moja thelathini. Haya ni mazingira ambayo yanaziwezesha mbegu kuzaa matunda yanayo kusudiwa. Huu ni mfano wa waamini ambao wanalisikiliza Neno la Mungu na kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha yao ya kila siku!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mfano wa mpanzi ni “nguzo na mama ya mifano yote” kwa sababu ni mfano unaozungumzia kuhusu usikivu wa Neno la Mungu. Ikumbukwe kwamba, Neno la Mungu ni mbegu yenye uwezo na nguvu. Mwenyezi Mungu anaipanda mbegu hii sehemu mbali mbali kwa moyo wa huruma, ukarimu na upendo bila ya kujiangaisha kuangalia mahali inapoangukia. Hiki ni kielelezo cha Moyo wa Mwenyezi Mungu. Kumbe, kila mwamini ni udongo ambao unaweza kuipokea mbegu ya Neno la Mungu na wala hakuna mtu anayetengwa na upendo huu wa Mungu. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza, Je, wao ni aina gani ya udongo? Je, wanafanana na udongo wa njia panda, udongo penye miamba au udongo penye miiba. Ikiwa kama waamini wanataka, wanaweza kuongoka na kuwa ni udongo mzuri unaoshughulikia kwa makini, ili uweze kusaidia mbegu za Neno la Mungu kuota na kuendelea kukua.

Neno la Mungu limekwisha kupandikizwa katika sakafu ya nyoyo za waamini, lakini ili ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, waamini wanapaswa kuchakarika usiku na mchana, kwa kulipokea Neno la Mungu na kuliheshimu. Waamini wawe waangalifu wasipoteze hata kidogo dira na mwelekeo wa maisha, kwani wahenga wanasema “Miruzi mingi humpoteza mbwa”. Hii inatokana na ukweli kwamba, waamini wanashindwa kutofautisha sauti na maneno mengi wanayoyasikia. Lakini, Neno la Mungu, ni Neno la pekee linalowaweka huru. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko alimgeukia Bikira Maria, ambaye katika maisha na utume wake amebaki kuwa ni udongo mzuri, awasaidie waamini kwa maombezi, ulinzi na tunza yake ya kimama, ili waweze kuwa ni udongo ambao uko wazi, bila ya miiba wala mawe, ili hatimaye, waweze kuzaa matunda bora kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa: Mpanzi

 

 

12 July 2020, 14:01