Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kuhusu Fumbo la Kifo, ili kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kifo chema! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kuhusu Fumbo la Kifo, ili kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kifo chema! 

Papa Francisko: Tafakari Kuhusu Fumbo la Kifo Kwa Mwanadamu!

Monsinyo Georg Ratzinger alizaliwa tarehe 15 Januari 1924. Baada ya mahangaiko makubwa katika malezi na majiundo yake ya Kikasisi, kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kunako tarehe 29 Juni 1951, akiwa ameambatana na mdogo wake, Papa Mstaafu Benedikto XVI, wakapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Monsinyo Georg Ratzinger amefariki dunia tarehe 1 Julai 2020.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu.

Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anaomboleza kifo cha kaka yake mkubwa Monsinyo Georg Ratzinger kilichotokea Jumatano tarehe 1 Julai 2020 huko nchini Ujerumani, akiwa na umri wa miaka 96. Ni hivi karibuni tu, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alikwenda nyumbani kwao kumtembelea na kumfariji katika uzee na mahangaiko yake kutokana na hali yake ya afya kuanza kudhohofu zaidi. Monsinyo Georg Ratzinger alizaliwa tarehe 15 Januari 1924. Baada ya mahangaiko makubwa katika malezi na majiundo yake ya Kikasisi, kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kunako tarehe 29 Juni 1951, akiwa ameambatana na mdogo wake, Papa Mstaafu Benedikto XVI, wakapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Monsinyo Georg Ratzinger alibahatika kuwa na kipaji cha muziki, kilichomwezesha kuzunguka sehemu mbali mbali za dunia ili kuwashirikisha watu wa Mungu, sala hii inayovuka mipaka ya lugha. Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, “Qui bene cantat bis orat” yaani “anayeimba vyema, anasali mara mbili”. Katika familia ya Ratzinger, wote walikuwa ni wapenzi wa muziki. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI pamoja na kaka yake mkubwa Georg Ratzinger, katika maisha yao, wamekuwa ni marafiki sana. Monsinyo George Ratzinger aliwahi kusema kwamba, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwake, alikuwa ni mwandani wake wa safari katika maisha na kiongozi anayetegemewa. Kwake amekuwa ni dira na mwongozo wake wa maisha; mtu mwaminifu na mkweli katika maamuzi yake! Daima amejitahidi kumwonesha njia ya kupitia hata katika nyakati ngumu na zenye changamoto pevu! Ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kupata fununu za nia ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kutaka kung’atuka madarakani kutokana na umri na afya yake kuanza kuingia kwenye mgogoro. Katika uzee wake, Baba Mtakatifu Mstaafu anataka amani na utulivu wa ndani. Hata katika uzee wake na afya yake kuanza kudhohofu zaidi kutokana na upofu na ugonjwa wa miguu, lakini bado, alijitahidi na kuhakikisha kwamba, mara kwa mara anamtembelea mdogo wake, yaani Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI.

Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima”. Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao! Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi! Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na  kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ameganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu!

Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton”. Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kumi” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka”. Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza. Baba Mtakatifu anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbu kumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili waweze kuwajalia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao!

Kifo kitakuja tu kwa wakati wake, kinaweza kuwahi au kuchelewa, lakini mwanadamu akumbuke kwamba, iko siku atakufa tu na hivyo kuungana na wahenga kwenye usingizi wa amani. Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kuitupa mkono duni, Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo!

Papa: Fumbo la Kifo

 

 

02 July 2020, 13:36