Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ameandika dibaji kwenye kitabu cha "Umoja na Matumaini: Ushuhuda wa imani katika nyakati za janga la Virusi Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko ameandika dibaji kwenye kitabu cha "Umoja na Matumaini: Ushuhuda wa imani katika nyakati za janga la Virusi Corona, COVID-19. 

Papa Francisko Tafakari Kuhusu COVID-19: Changamoto, Matatizo na Imani

Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji anasema, Kitabu cha “Umoja na Matumaini, Ushuhuda wa imani katika nyakati za janga la Virusi vya Corona, COVID-19”. Ni mkusanyiko wa shuhuda mbalimbali za Kikristo za jinsi ya kutangaza na kushuhudia imani wakati wa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona-Covid-19. Janga hili limewashutua watu wengi sana duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameandika dibaji kwenye kitabu kilichotungwa na Kardinali Walter Kasper, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, akishirikiana na Padre George Augustin kutoka Shirika la Wapallottin lililoanzishwa na Padre Vicent Mary Pallotti. Kitabu hiki ambacho kimeandikwa kwa lugha ya Kijerumani na Kiitalia kinajulikana kama "Comunione e speranza, testimoniare la fede al tempo del Coronavirus" yaani “Umoja na Matumaini, Ushuhuda wa imani katika nyakati za janga la Virusi vya Corona, COVID-19”. Padre George Augustin kunamo mwaka 2005 alianzisha Taasisi ya Kardinali Walter Kasper: “Kardinal Walter Kasper Institut”. Hii ni taasisi inayojishughulisha kisayansi na masuala ya taalimungu, uekumene na tasaufi.

Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji anasema, Kitabu cha “Umoja na Matumaini, Ushuhuda wa imani katika nyakati za janga la Virusi vya Corona, COVID-19”, ni mkusanyiko wa shuhuda mbalimbali za Kikristo za jinsi ya kutangaza na kushuhudia imani wakati wa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona-Covid-19. Hili ni janga ambalo limewashtua watu wengi kama dhoruba kali, kiasi cha kugusa na kubadili mambo mengi katika maisha sehemu mbali mbali za dunia. Ni dhoruba ambayo imetikisa maisha ya kifamilia, kikazi na hadhara. Watu wengi bado wanaendelea kuwalilia na kuwaombolezea ndugu, jamaa na marafiki zao waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Kuna mamilioni ya watu ambao wameathirika vibaya sana kiuchumi na wengine wapoteza fursa za ajira.

Maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2020 kiini cha maisha ya Wakristo, yamegubikwa na upweke, majonzi pamoja na athari kubwa za: kiroho, kimwili na kijamii ambazo zimesababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Waamini wengi wameshindwa kuchota huruma, upendo na baraka za Mwenyezi Mungu kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na ile ya Upatanisho pamoja na Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Hata katika muktadha huu, Mwenyezi Mungu bado ameendelea kuwa na waja wake, changamoto na mwaliko ni kuendelea kushikamana katika sala, kwani kwa hakika, atawanyooshea mkono wake na kuwatia shime, wasiogope kwani Kristo Mfufuka yuko daima pamoja nao! Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limeufunua udhaifu wa binadamu, dhamiri nyofu na umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kama ndugu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, janga hili limezua maswali tete ambayo ni msingi, mipango na miradi mbali mbali ambayo mwanadamu alikuwa amelenga kuitekeleza katika maisha yake. Janga la Corona, COVID-19 linatoa changamoto ya maswali msingi kuhusu furaha ya kweli, amana na utajiri wa imani ya Kikristo. Haya ni mambo tete yanayotakiwa kufanyiwa tafakari ya kina ili kuangalia ni mahali gani ambapo, waamini wanakita zaidi mizizi ya maisha yao, ili kukabiliana na dhoruba kali ya janga la Virusi vya Corona-COVID-19. Waamini wanakumbushwa kwamba, kuna mambo msingi ambayo wamesahau kuyapatia kipaumbele cha kwanza na kumbe, huu ni wakati wa kuangalia mambo msingi na yale mambo ambayo yanaonekana kuwa na mvuto lakini si yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee.

Baba Mtakatifu anakaza kusema kwamba, hiki ni kipindi cha majaribu yanayopaswa kupewa maamuzi mazito katika maisha, ili kupyaisha maisha, mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye faraja na hatima ya maisha ya waja wake. Mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu; umuhimu wa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani katika hali na mwamko mpya ni kati ya mambo mazito yaliyoibuliwa kutokana na janga la Virusi vya Corona-COVID-19. Ni wakati wa kusimama kidete kupambana na ukosefu wa misingi ya haki sehemu mbali mbali za dunia, ili hatimaye, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi”.

Kwa hakika ulimwengu mamboleo unachechemea sana kwa maradhi. Katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, waamini wamesikiliza ujumbe wa Kristo Mfufuka, aliyeshinda dhambi na mauti! Kumbe, waamini wanapaswa “kutoka kifua mbele” na kamwe wasikubali “kupigishwa magoti” na Virusi vya Corona, COVID-19. Fumbo la Pasaka ni kiini na chemchemi ya matumaini, imani na ujasiri; mambo yanayoimarisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na chuki pamoja na uhasama; kwa kutambua kwamba, wote kwa pamoja, wanaunda familia kubwa ya binadamu, inayopaswa kushikamana, kusaidiana na kubebeana mizigo kama kielelezo cha faraja. Hatari ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, iwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza umuhimu wa “kuambukizana” fadhila ya upendo, kwa kusaidiana.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii katika dibaji ya kitabu cha: “Umoja na Matumaini, Ushuhuda wa imani katika nyakati za janga la Virusi vya Corona, COVID-19” kukiri kwamba, ameshuhudia alama za sadaka na majitoleo yaliyoshuhudiwa na madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya, wakleri na watawa. Ushuhuda wao katika majuma yote hayo ni nguvu iliyokuwa inabubujika kutoka katika amana na utajiri wa imani. Waamini walishindwa kuadhimisha Fumbo la Pasaka hadharani na matokeo yake, waamini wengi wakajikuta wakiwa wanaelemewa na ukame wa Ekaristi Takatifu. Lakini, waamini wamejifunza na kugundua uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake, wanapokutanika kwa ajili ya jina lake. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa njia ya vyombo vya habari na mawasiliano yalikuwa ni kwa ajili ya dharura peke yake, ingawa watu wengi wanamshukuru Mungu kwa sadaka na majitoleo makubwa yaliyooneshwa na wadau wa tasnia ya mawasiliano ya kijamii.

Lakini, maadhimisho haya hayawezi hata kidogo kuchukua nafasi ya uwepo na ushiriki mkamilifu wa waamini katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu! Kumbe, huu ni wakati muafaka wa kuanza kurejea tena katika sheria, kanuni na taratibu za maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Uwepo wa Kristo Mfufuka katika Neno na Sakramenti zake ni chemchemi ya nguvu  na faraja ya imani itakayowasaidia waamini kukabiliana na matatizo na changamoto mamboleo baada ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19 kupita. Ni matumaini na imani thabiti ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, tafakari za kitaalimungu zilizowekwa kwenye kitabu hiki, zitawasaidia wasomi kuendelea kufanya tafakari ya kina, zitasaidia kuibua matumaini na mshikamano mpya. Kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Yesu anaendelea kuandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau, ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo. Kwa njia ya Neno lake na wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi, atawaambia tena “Msiogope, Mimi nimeshinda mauti!

Papa: Corona-COVID-19

 

 

30 July 2020, 14:08