Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Papa Francisko Jubilei ya Miaka 50 ya "Ordo virginum": Unabii asili ya wito wao; Mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma, upendo na mshikamano na maskini. Ujumbe wa Papa Francisko Jubilei ya Miaka 50 ya "Ordo virginum": Unabii asili ya wito wao; Mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma, upendo na mshikamano na maskini. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Wanawake Waliowekwa Wakfu:

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Jubilei ya Miaka 50 tangu Kuchapishwa kwa Ibada ya Kuwaweka Wakfu Wanawake; anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wanawake waliowekwa wakfu ndani ya Kanisa. Anawataka waendeleze asili ya unabii wa wito wao; wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo; faraja na huruma kwa maskini na wote wasiopendwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 31 Mei 1970, Miaka 50 iliyopita, Mtakatifu Paulo VI aliliagiza Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kupitia na kufanya marekebisho katika Ibada ya Madhehebu ya Kuwaweka wanawake wakfu kwa ajili ya Mungu na Kanisa: “The New Rite of Consecration of Virgins”. Tukio hili la kihistoria, limeahirishwa kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni tukio ambalo lilikuwa limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Jubilei ya Miaka 50 tangu Kuchapishwa kwa Ibada ya Kuwaweka wanawake wakfu; anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wanawake waliowekwa wakfu ndani ya Kanisa. Anawataka waendeleze asili ya unabii wa wito wao; wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo; faraja na huruma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wanawake waliowekwa wakfu watambue kwamba, wao ni wachumba waaminifu wa Kristo Yesu katika maisha na wito wao.

Baba Mtakatifu anasema, marekebisho yaliyofanywa kwenye Madhehebu ya Ibada ya kuwaweka wanawake wakfu na “Ordo fidelium” yamerejesha tena ile Jumuiya ya Kikanisa kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa kama zinavyofafanuliwa kwenye Mwongozo wa “Ecclesiae Sponsae Imago” uliochapishwa kunako mwaka 2018. Wito wa maisha ya wanawake waliowekwa wakfu ni alama ya utajiri wa zawadi na karama za Roho Mtakatifu, ambazo Kristo Mfufuka anapenda kulijalia Kanisa lake, ili kuyafanya yote mapya. Ni alama ya matumaini inayowataka wanawake waliowekwa wakfu kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu ambaye hata leo hii, anaamsha ndani ya watu kiu ya kutaka kujiweka wakfu katika nadhiri ya usafi kamili na kuendelea kuishi katika jamii na tamaduni; kwa kujiaminisha kwa Kanisa mahalia mintarafu maisha ya wakfu katika asili yake, lakini ambayo kwa sasa yamepyaishwa zaidi.

Kwa wanawake waliowekwa wakfu na kusindikizwa na Maaskofu mahalia katika maisha na utume wao, wamekuwa na mchango maalum kwa Makanisa mahalia. Maaskofu wamekuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa kuwasaidia wanawake wanaotaka kujiweka wakfu kufanya mang’amuzi ya kina pamoja na kuendelea kuwapatia majiundo ya awali na endelevu. Zawadi ya wito huu ni kielelezo cha umoja wa Kanisa unaojidhihirisha kwa wanawake kumwilisha udada wao katika maisha. Jubilei ya Miaka 50 tangu kufanyika kwa marekebisho haya ni nafasi ya kuendelea kujizatiti katika unabii ambao ni asili ya wito wao. Wakumbuke kwamba, wameitwa si kutokana na juhudi zao binafsi, bali ni kwa njia ya huruma ya Mungu, ili maisha yao, yaweze kuakisi Uso wa Kanisa, Mchumba wa Kristo Yesu. Kanisa ni bikira hata kama bado watoto wake wanaogelea katika dimbwi la dhambi; linaendelea kutunza imani na kuzaa maisha mapya, ili kusaidia ukuaji na ukomavu wa utu mpya!

Baba Mtakatifu anawakumbusha wanawake waliowekwa wakfu kwa ajili ya Mungu na Kanisa, kuwa wanapaswa kuonesha umoja unaobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa na kwamba, wanapaswa kujisadaka kwa kujiaminisha kwa Kristo, tayari kumkaribisha katika maisha yao. Kwa hakika, Kristo Yesu hatachelewa kuwaendea. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kujizatiti kila kukicha katika hija ya maisha yao Kikanisa. Kwa njia hii, watafanikiwa kuwa ni nyota angavu zinazouongoza ulimwengu katika safari hii. Wanawake waliowekwa wakfu wanahimizwa kujisomea na kutafakari Mwongozo wa Madhehebu ya kuwaweka wakfu, ili kutambua maana ya wito wao, tayari kufanya mang’amuzi ya wito wao ambao ni kielelezo cha upendo na nguvu ya Mungu inayomwongoa mwanadamu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Neno la Mungu, Kristo Yesu anawaalika kumwonesha upendo wa dhati.

Baba Mtakatifu anawataka wanawake waliowekwa wakfu kwa ajili ya Mungu na Kanisa kuendelea kujizatiti ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Walisaidie Kanisa kuwapenda na kuwahudia maskini wa kiroho na kimwili. Waoneshe ukaribu wa Kiinjili kwa wagonjwa mbali mbali; kwa vijana na wazee pamoja na wale wote wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watu ambao wanaweza kusukumwa pembezoni mwa jamii wakati wowote ule! Wawe ni wanawake wenye huruma na wataalam katika utu, chemchemi ya mapinduzi ya upendo na upole. Huu ni muda wa kufyekelea mbali ukosefu wa usawa; kwa kuganga na kuponya majeraha ya ukosefu wa haki yanayotishia ustawi, maendeleo na mafao ya familia kubwa ya binadamu.

Wanawake waliowekwa wakfu, wajitahidi kusoma alama za nyakati na kusimama imara ili kupambana na mazingira hasa kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Waguswe na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu. Wadumu katika kutangaza na kushuhudia Injili ambayo ni utimilifu wa maisha kwa watu wote. Wajitahidi kuishi kikamilifu nadhiri ya usafi wa moyo kwa uhuru kamili “Castalibertas” kwa kuendelea kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii, kama kielelezo cha upendo wa Kanisa, mchumba wake Kristo; Bikira na Mama; Dada na rafiki wa wote. Kwa ukarimu wao, wajenge na kuimarisha mtandao wa mafungamano ya kijamii, ili kujenga ujirani mwema, kwa kuondokana na upweke hasi na tabia ya watu kutojulikana. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaonya wanawake waliowekwa wakfu kuepukana na umbea na majungu. Wawe na hekima, busara na amana; wajenge nguvu ya upendo ili kuondokana na kiburi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, amewatakia wote heri, baraka na furaha ya Injili kutoka kwa Roho Mtakatifu. Kama alama ya Kanisa, Mchumba wa Kristo, wawe daima ni wanawake wenye furaha, wakiendelea kufuata mfano wa Bikira Maria wa Utenzi wa “Magnificat, Mama wa Injili hai!

Papa: Mabikira

 

 

02 June 2020, 13:41