Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewaambia mahujaji wa hija ya 42 kutoka Macerata hadi Loreto kwamba, wao ni mahujaji wa Bikira Maria, nyota ya matumaini mapya! Baba Mtakatifu Francisko amewaambia mahujaji wa hija ya 42 kutoka Macerata hadi Loreto kwamba, wao ni mahujaji wa Bikira Maria, nyota ya matumaini mapya! 

Papa Francisko: Mahujaji wa Bikira Maria, Nyota ya Matumaini

Baba Mtakatifu Francisko amewashauri mahujaji kumsihi Bikira Maria ili aweze kuwaombea kwa Kristo Yesu, ujasiri wa kukabiliana na matatizo na changamoto mamboleo. Wao ni mahujaji wa Bikira Maria, chemchemi ya matumaini. Papa amekuwa akishiriki hija kutoka Macerata hadi kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto kwa njia ya simu. Hija hii ilianzishwa kunako mwaka 1978.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa kuzingatia itifaki dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Hija ya 42 kutoka Macerata hadi kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, nchini Italia kwa mwaka 2020 yamefanyika kwa njia ya mtandao. Tukio hili limerushwa mubashara na Kituo cha Televisheni cha Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, TV2000. Baba Mtakatifu Francisko amezungumza mubashara na mahujaji hawa kwa njia ya simu kutoka mjini Vatican. Mahujaji walikuwa wamekusanyika nje ya Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, Jumamosi tarehe 13 Juni 2020. Baba Mtakatifu amesema kwamba, Bikira Maria ni Mama wa matumaini, anayewasaidia waamini kuangalia mbali zaidi, huku wakiwa na matumaini, hususan katika kipindi hiki cha janga kubwa la ugonjwa Virusi vya Corona, COVID-19.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na matumaini. Amewahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Amewaomba kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Amewataka pia kuwa na ujasiri kwa sababu kipindi kinachofuatia baada ya janga la Corona, COVID-19 hakitakuwa rahisi sana! Lakini kwa njia ya imani, matumaini na mapendo, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Katika hija hii kwa njia ya mtandao, Baba Mtakatifu amewashauri mahujaji kumsihi Bikira Maria ili aweze kuwaombea kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ujasiri wa kukabiliana na matatizo na changamoto mamboleo. Amewashukuru wote walioshiriki ili kuhakikisha kwamba, tukio hili linafanikiwa katika ubora wake hata kama ni kwa njia ya mtandao na uwakilishi wa vijana wachache tu!

Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, wao ni mahujaji wa Bikira Maria, chemchemi ya matumaini. Baba Mtakatifu tangu mwaka 2013 amekuwa akishiriki hija kutoka Macerata hadi kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto kwa njia ya simu. Hija hii ilianzishwa kunako mwaka 1978. Askofu Nazzareno Marconi wa Jimbo Katoliki la Macerata, Italia amebariki Mwenge wa Amani ambao umepelekwa moja kwa moja kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto ambako kumefanyika Ibada ya: Sala, Liturujia ya Neno la Mungu, Maombi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Rozari Takatifu pamoja na nyimbo na hatimaye, kuhitimishwa kwa baraka ya Sakramenti kuu, iliyotolewa na Askofu mkuu Fabio Dal Cin wa Jimbo kuu la Loreto, Italia.

Papa: Loreto

 

15 June 2020, 13:36