Tafuta

Vatican News
Tarehe 26 Juni 2020 ni Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya! Tarehe 26 Juni 2020 ni Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya!  (AFP or licensors)

Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya ni Hatari!

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni, inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani. Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupambana na dawa za kulevya na uhalifu, "UNODC” inasema, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku hii kwa mwaka 2020 ni “Tunahitaji maarifa zaidi ili kutoa huduma bora”. Biashara hii ni hatari sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu mwaka 1989, Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni, inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani. Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupambana na dawa za kulevya na uhalifu, “United Nations Office on Drugs and Crime, UNODC” inasema, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku hii kwa mwaka 2020 ni “Tunahitaji maarifa zaidi ili kutoa huduma bora”. Lengo ni kusaidia maboresho ya uelewa mpana zaidi wa mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kupambana na biashara hii ambayo ina madhara makubwa katika afya, utawala bora, ulinzi na usalama wa raia na mali zao! Ikumbukwe kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake ni kikwazo kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa afya, maisha na jamii katika ujumla wake, changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe ili kupambana dhidi ya uzalishaji, uchakataji, usambazi na matumizi haramu ya dawa hizi sehemu mbali mbali za dunia.

Ni dhamana pevu kwa serikali kuhakikisha kwamba, zinapambana kufa na kupona na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa kuwashughulikia kisheria wale wote wanaoendelea kupandikiza kifo miongoni mwa vijana! Matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa njia ya mitandao ni hatari inayoendelea kujionesha kila kukicha na kwamba, vijana ndio wanaotumbukizwa kwa urahisi katika janga hili, kiasi cha kupoteza maana ya maisha. Kutokana na changamoto hizi, Mama Kanisa anapenda kujipambanua katika masuala haya, ili kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili kwamba, binadamu na mahitaji yake msingi apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Utu wa binadamu ndiyo msingi wa Injili ya huruma ya Mungu. Ni kutokana na msingi huu, wakristo wanapaswa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji ili kusaidia mchakato wa kuzuia, kuganga na kuponya magonjwa yanayotokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, Kanisa linataka kumweka binadamu kuwa ni kiini cha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Mama Kanisa ataendelea kushirikiana na kushikamana na wadau sehemu mbali mbali za dunia katika kuelimisha, kuzuia, kurekebisha na kuwaponya waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu. Ushindi dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya unafumbatwa kwa namna ya pekee katika umoja na mshikamano kati ya taasisi, familia na sekta ya elimu katika ujumla wake.

Dawa za Kulevya 2020
26 June 2020, 14:13