Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, amewakumbuka watakatifu, wafiadini na waungama imani, waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, amewakumbuka watakatifu, wafiadini na waungama imani, waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. 

Papa Francisko: Utu na Heshima kwa Wakazi wa Mji wa Roma!

Baba Mtakatifu kwa maombezi ya Watakatifu Petro na Paulo, amewaombea wananchi wote wa mji wa Roma ili waweze kuishi maisha yanayozingatia: utu na heshima ya binadamu, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili. Ni katika muktadha wa ushuhuda wa imani, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake: Ushuhuda katika matendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 29 Juni 2020, akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, walioyamimina maisha yao kama sadaka safi na ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika mahubiri yake, amekazia mambo makuu mawili yaani: Umoja unaofumbatwa katika upendo na utofauti; katika mateso, sala na ushuhuda wa imani; Amebariki Pallio Takatifu 54 watakazovishwa Maaskofu wakuu walioteuliwa kati ya Mwaka 2019-2020, kama alama ya Kristo Mchungaji mwema; alama ya umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Pili, ni Unabii unaosimikwa katika ushuhuda wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha upendo kwa Mungu; unaoleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 ametafakari kuhusu Mtume Petro na Paulo, Wasimamizi wa Mji wa Roma. Uwanja wa Kanisa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni mahali ambapo inasadikiwa kwamba, Mtakatifu Petro aliuwawa kikatili na kuzikwa katika eneo hili. Safari ya maisha ya Mtakatifu Petro inaweza kuwa ni dira kwa maisha ya waamini, kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya Mungu aliye hai! Hata kwa Mtakatifu Paulo, Mtume wa Mataifa, alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; akaona yote kuwa si mali kitu, ili kumpata na kumwambata Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwa namna ya pekee aliwasalimia watu wa Mungu wanaoishi na kufanya shughuli zao mbali mbali mjini Roma, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Wasimamizi wa mji wa Roma. Baba Mtakatifu kwa maombezi ya Watakatifu Petro na Paulo, amewaombea wananchi wote wa mji wa Roma ili waweze kuishi maisha yanayozingatia: utu na heshima ya binadamu, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili. Ni katika muktadha wa ushuhuda wa imani, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, Baba Mtakatifu amewakumbuka: watakatifu, mashuhuda na waungama imani, walioteswa, wakauwawa kikatili na wengine kuchomwa moto kwa mashtaka ya uwongo.

Hivi ndivyo ilivyotokea kwenye madhulumu ya Mfalme Nero, tarehe 19 Julai 64 alipoteketekeza mji wa Roma kwa moto pamoja na kuwachoma Wakristo, wengi wao wakiwa bado hai na wakaendelea kuungua taratibu kwa ajili ya kutoa mwanga kwa mji wa Roma. Ndiyo maana, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 30 Juni, anawakumbuka wafiadini wa kwanza wa Kanisa la Roma. Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni mahali patakatifu sana, kwa ni hapa anasema Baba Mtakatifu ni mahali ambapo palilowanishwa kwa damu ya mashuhuda na waungama imani. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa watu wa Mungu kutoka Canada, Venezuela, Colombia na sehemu mbali mbali za dunia, waliokuwa wamebeba bendera za nchi zao. Hija ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwenye makaburi ya watakatifu Petro na Paulo, Mitume, isaidie kuimarisha imani na ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Baba Mtakatifu amesema kwa kawaida katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, Patriaki Bartolomeo wa kwanza, huwa anatumwa ujumbe kwa ajili ya kushiriki maadhimisho haya. Lakini mwaka 2020 imeshindikana kutokana na hofu ya maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona. Hata hivyo, Baba Mtakatifu amemtumia salam na matashi mema, Patriaki Bartlomeo wa kwanza, huku akiwa na matumaini kwamba, wataweza kurejesha tena utamaduni na mapokeo ya kutembelea hivi karibuni.

Papa Mashuhuda wa Imani

 

 

30 June 2020, 13:05