Tafuta

Vatican News
Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria ni chemchemi ya faraja, imani na matumaini. Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria ni chemchemi ya faraja, imani na matumaini.  (AFP or licensors)

Moyo Safi wa Bikira Maria: Upendo, Faraja na Matumaini kwa wote!

Sikukuu ya Moyo Safi wa Bikira Maria, ilianzishwa mwaka 1944. Hii ni Ibada inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Watakatifu na waungama imani, wakaiendeleza Ibada hii kwa ari na moyo mkuu zaidi. Mtakatifu Eudes 1601-1680: Alikuza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu na Moyo Safi wa Bikira Maria, Mama wa Yesu. Kunako mwaka 1668 Ibada ikaadhimishwa nchini Ufaransa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Luka anabainisha kwa kina na mapana mambo msingi katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka. Yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake". LK 2:19. Simeoni: Upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Lk.2:35. Uchungu mkubwa ni kumwona Mkombozi wa ulimwengu, akiyamimina maisha yake, sawa na mkuki uliopenya katika undani wa maisha ya Bikira Maria, akabaki akiwa ameshika tama, kama anavyooneshwa kwenye michoro kadhaa katika Mapokeo ya Kanisa ya Mashariki. Chini ya Msalaba, Kristo Yesu aliweza kuonana mubashara na Mama yake na hivyo kumkirimia kiwango cha hali ya juu kabisa cha matumaini. Ni katika muktadha huu, Bikira Maria aliweza kuguswa na mateso makali hadi kifo cha aibu alichokumbana nacho Kristo Yesu! Kimsingi, mateso na kifo ni changamoto pevu katika maisha ya mwanadamu, sembuse kwa Mama?

Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo hata kwa wanafunzi wa Yesu lilikuwa ni kashfa kubwa sana ndiyo maana alipokuwa anatangaza kuhusu kuteswa, kufa na kufufuka kwake, Mtakatifu Petro, Mtume, akamvuta kando na kumwelezea kwamba, haya kamwe hayataweza kumpata hata kidogo! Lakini, badala yake, Kristo Yesu akamwambia Petro “Nenda nyuma yangu, Shetani”. Lilikuwa ni jambo la kushangaza sana kuona Masiha wa Bwana, akiteseka na hata kufa Msalabani, kwani wao walitegemea kumwona Masiha wa kisiasa na mwenye nguvu za kijeshi. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa wale wanafunzi wa Emau waliokuwa na matumaini kwamba, Kristo Yesu ndiye atakaye mkomboa Israeli, lakini kwa bahati mbaya, ameishia kuteswa, kutundikwa Msalabani na kufa kifo cha aibu. Matumaini ya kumwona Kristo Yesu akiwakomboa, yakatoweka kama umande wa asubuhi. Huu ndio mwelekeo wa kibinadamu kwamba, hakuna ukombozi unaoweza kububujika kutoka katika mateso na kifo cha aibu kama hiki.

Bikira Maria akiwa chini ya Msalaba aliyatafakari yote haya na kujiuliza, kulikoni hata Mkombozi wa ulimwengu kuteswa, kufa na kuzikwa? Mwinjili Luka tangu mwanzo alikwisha kusema kuhusu Bikira Maria “Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi” Lk. 2: 34-35. Upanga wenye makali kuwili, ukapenya katika sakafu ya moyo wa Bikira Maria. Upanga huu, kadiri ya Waraka kwa Waebrania ni “Neno la Mungu”. Bikira Maria chini ya Msalaba akayatafakari yote haya na kuyahifadhi katika moyo wake, kama kito cha thamani kubwa. Neno la Kigiriki lililotumika ni “symballo” yaani, Bikira Maria katika hali na mazingira haya, alijitahidi kuunganisha maneno na matendo yaliyokuwa mbele ya macho yake. Bikira Maria alikuwa chini ya Msalaba na juu ya Msalaba kulikuwa kumeandikwa anuani ifuatayo “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi” Lk. 23: 38. Kristo Yesu ni Mfalme aliyetundikwa Msalabani, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Padre Marko Ivan Rupnik anakaza kusema, ili mwamini kuweza kufikia hatima hii, anahitaji nguvu na msaada wa Roho Mtakatifu. Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni zawadi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, jambo linaloweza kueleweka tu kwa njia ya kiri ya imani.

Mama Kanisa baada ya kuadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jumamosi inayofuatia, anaadhimisha Sikukuu ya Moyo Safi wa Bikira Maria, iliyoanzishwa kunako mwaka 1944, ingawa Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria, imekuwemo katika maisha na utume wa Kanisa tangu awali sana. Hii ni Ibada inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Watakatifu na waungama imani, wakaiendeleza Ibada hii kwa ari na moyo mkuu zaidi, kiasi hata Mababa wa Kanisa wakaivalia njuga na kuitangaza kwa ajili ya Kanisa zima. Mtakatifu Yohane Eudes aliyeishi kati ya Mwaka 1601 hadi mwaka 1680 katika tafakari zake, alipenda kuunganisha Moyo Mtakatifu wa Yesu na Moyo Safi wa Bikira Maria, Mama wa Yesu. Kunako mwaka 1668 Ibada hii ikaanza kuadhimishwa nchini Ufaransa. Tarehe 13 Julai 1917, Bikira Maria aliwatokea Watoto wa Fatima, wakati walimwengu walipokuwa wanateseka kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Bikira Maria akawapatia ujumbe wa matumaini uliokuwa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika: toba, wongofu wa ndani pamoja na sala na kwamba, Mwenyezi Mungu daima anatembea katika historia ya maisha ya watu wake, mwaliko kwa waamini kumtumainia Kristo Yesu kwani yeye ameushinda ulimwengu. Kunako mwaka 1942 Papa Pio XII akaliweka Kanisa na watu wote wa Mungu nchini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria, akimwomba, aweze kuliombea Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, amani ya kudumu kutokana na vitisho vya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kunako mwaka 1944 Papa Pio XII akaeneza Ibada hii kwa Kanisa la Ulimwengu. Ibada hii ni chemchemi ya utakatifu, uchaji na matumaini ya watu wa Mungu waliokombolewa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao wokovu. Lengo la Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria ni kuombea amani duniani, uhuru wa Kanisa na wadhambi waweze kupata nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu. Kwa njia ya Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria, waamini waimarishwe katika imani na fadhila mbali mbali za Kikristo kwa njia ya neema ya Mungu.

Wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, Mtakatifu Paulo VI alikwenda kuhiji mjini Fatima nchini Ureno. Lakini, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na uhusiano na ibada ya pekee kabisa kwa Bikira Maria wa Fatima katika maisha na utume wake, kiasi cha kujikabidhi kwa huyu Mama. Kwa namna ya pekee kabisa, waamini wanaalikwa kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili; ili kujiachilia wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kujazwa na upendo wake usiokuwa na kifani. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alitembelea madhabahu haya kunako mwaka 2010. Huyu ndiye aliyefafanua kuhusu siri za Fatima na kuziweka hadharani. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kusoma ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima katika mwanga wa historia ya ukombozi.

Ujumbe huu uwe ni changamoto na mwaliko wa kuzama zaidi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika toba, wongofu wa ndani na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Lugha aliyotumia Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ilikuwa ni lugha ya upendo inayoeleweka na kufahamika na wengi hivyo, waamini wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Bikira Maria ameendelea kupewa kipaumbele cha pekee hata wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa na Ibada ya pekee sana kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kabla na baada ya hija zake za kitume, daima amekimbilia ulinzi na tunza ya Mama wa Mungu katika hija zake za kitume. Anawataka waamini kukuza na kudumisha Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Waamini wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao.

Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia wa Rozari Takatifu, amebarikiwa kuliko wanawake wote, ni sura ya Kanisa iliyovishwa mwanga wa Pasaka; Yeye ni heshima ya watu wa Mungu; mshindi dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo! Watoto wa Fatima wawe ni mfano bora wa kujiaminisha kwa kukimbilia: ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, anayewanyanyua kwa kuwashika mkono. Ni Mama anayewafunda kukua na kukomaa katika upendo kwa Kristo na umoja wa kidugu! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwangalia na kumwomba Bikira, ili hatimaye, kumwachia nafasi pia ili aweze kuwaangalia, kwani anawapenda kama Mama ili waweze kujifunza kuwa wanyenyekevu na wajasiri katika kufuasa Neno la Mungu, Kumpokea Mwanaye mpendwa Yesu Kristo; kwa njia ya urafiki, waweze kuwapenda pia jirani zao kadiri ya kipimo cha Moyo Mtakatifu wa Yesu ambao ni chemchemi ya: maisha, matumaini na amani! Uhusiano mwema na Bikira Maria uwasaidie waamini kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mama Kanisa, kwani wote ni Mama, kwani lile linaloweza kusemwa kwa Bikira Maria linaweza pia kusemwa kwa Kanisa na moyo wa binadamu, kama anavyofafanua Abate Isaac wa nyota!

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wao ni chemchemi ya uhai na bila kuwa na uhusiano wa kimwana na Bikira Maria, mwamini atajisikia kuwa yatima moyoni mwake! Bikira Maria awe ni kimbilio la Mapadre hasa katika nyakati ngumu za maisha na utume wao, ili waweze kupata ulinzi na tunza ya Mama Bikira Maria, daima wajitahidi kuzituliza nafsi zao na kuzinyamazisha kama mtoto aliyenyoshwa kifuani mwa mama yake. Bikira Maria ni shuhuda wa unabii wa upendo wa huruma ya Mungu; mwalimu mahiri wa Habari Njema ya Mwana wa Mungu, alama ya moto wa Roho Mtakatifu. Huku bondeni kwenye furaha na machozi, Bikira Maria awafundishe watoto wake ukweli ambao Baba wa milele, anapenda kuwafunulia wadogo na wanyenyekevu wa moyo, watu wasiokuwa na makuu. Bikira Maria awaoneshe ulinzi na tunza ya mkono wenye nguvu! Moyo wake safi usiokuwa na doa uwe ni kimbilio la wadhambi, njia inayowaelekeza kwa Mwenyezi Mungu.

Moyo Safi wa Bikira Maria

 

 

22 June 2020, 14:22