Tafuta

Vatican News
Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya Kuombea Toba, Wongofu wa Ndani na Utakatifu wa Mapadre; mambo msingi katika maisha na utume wa kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya Kuombea Toba, Wongofu wa Ndani na Utakatifu wa Mapadre; mambo msingi katika maisha na utume wa kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu.  (Vatican Media)

Moyo Mtakatifu wa Yesu: Utakatifu wa Mapadre katika Utume wa Kanisa

Daraja Takatifu ya Upadre ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa, kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli, Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza. Utakatifu wa Mapadre ni muhimu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002 akatenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa maisha ya Mapadre Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wakleri kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Papa Pio XII, “Haurietis acqua” wa Mwaka 1956 kuhusu “Moyo Mtakatifu wa Yesu kiini cha huruma ya Mungu”. Ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejifanya kuwa mdogo ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta maisha na uzima wa milele! Utakatifu wa Mapadre ni hitaji muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Ukweli huu wa imani katika maisha na utume wa Mama Kanisa, unagusa hata maisha ya waamini walei ambao usiku na mchana wanatafuta utakatifu wao kwa kutambua au kwa kutokujua kutoka kwa mtu wa Mungu. Waamini wanamwona Padre kuwa ni mshauri wa maisha ya kiroho, mpatanishi wa amani; mtu mwenye hekima na busara. Ni kiongozi salama ambaye watu wa Mungu wanaweza kujiaminisha kwake nyakati ngumu na wakati wa majaribu ya maisha, ili kuonja na hatimaye kupata faraja na usalama wao! Hivi karibuni, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri limechapisha mwongozo wa malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”.  Haya ni matunda ya changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa, kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli, Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia!

Mwongozo huu ni matunda ya ushirikiano mkubwa kutoka katika Sektretarieti kuu ya Vatican, kazi iliyoanza kunako mwaka 2014. Mwongozo unatoa kwa muhtasari: sheria, kanuni na mambo msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unabainisha wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; Waratibu wa Seminari kitaifa na kimataifa pamoja na mwongozo wa malezi ya mseminari moja moja. Kwa kuzingatia umuhimu wa malezi na majiundo ya Kikasisi katika ulimwengu mamboleo wenye changamoto nyingi. Mwongozo wa “Zawadi ya Wito wa Kipadre” unapembua kwa kina na mapana: kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Yaani Wakleri wanapaswa kuunganika na Kristo Yesu ili kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa roho za watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Wito wa Daraja takatifu ni zawadi inayoleta furaha na kumkirimia mtu nguvu ya kusonga mbele kwa ujasiri mkubwa!

Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu. Malezi kiroho: yanafumbatwa katika tafakari ya Neno la Mungu; Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Maisha ya Sala na Ibada pamoja na kuwa na mahusiano ya karibu na Padre mlezi wa maisha ya kiroho pamoja na kukuza kwa kina na mapana Mashauri ya kiroho. Malezi: kiakili ni kumwezesha jandokasisi kuwa mahiri katika falsafa na taalimungu ili kupambana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika masuala ya kitamaduni kwa kutoa malezi ya kina kwa milango yote ya fahamu za binadamu! Majiundo haya yazingatie pia utamaduni na historia ya nchi husika. Malezi ya kichungaji ni mambo yanayomwezesha Padre kuwajibika na kutoa huduma makini zaidi kwa familia ya Mungu kwa njia ya upendo wa shughuli za kichungaji. Kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kuamua na kutenda; kwa kuwaheshimu na kuwajali watu; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kusimamia tunu msingi za maisha ya Kikristo, daima akionesha ari na utume wa Kimissionari.

Mwongozo unafafanua kuhusu: mihimili mikuu ya malezi kwa kuzingatia kwamba: mlezi mkuu ni Fumbo la Utatu Mtakatifu, Askofu mahalia, Mapadre, Waseminari wenyewe, Jumuiya ya walezi yaani Majaalimu na wataalam mbali mbali wanaoalikwa ili kusaidia kutoa malezi kwa majandokasisi. Familia na Parokia pia zinahusika kikamilifu katika malezi ya majandokasisi. Watawa na waamini walei wanaweza pia kuhusishwa katika malezi ya Mapadre wa baadaye. Makundi yote haya ni muhimu sana katika malezi endelevu na fungamani ya Wakleri katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, anapenda kuwakumbusha wakleri wenzake kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu, wao kwanza ni waamini waliobatizwa kwa Maji na Roho Mtakatifu. Utambulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa.

Kwa namna ya pekee, wao ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Kutokana na uzoefu na mang’amuzi ya maisha, wakleri kwa namna ya pekee ni viongozi wa Jumuiya ya waamini katika safari ya maisha yao ya kiroho; dhamana wanayoitekeleza kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma ya mapendo kwa ajili ya kuwasindikiza waamini katika maisha yao kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa katika ujumla wake. Kwa njia hizi, waamini wote wanaweza kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao anasema Kardinali Beniamino Stella.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ya Mungu kwa namna ya pekee kabisa, inaadhimishwa kwenye Sakramenti ya Upatanisho, ambapo Mwenyezi Mungu anamkumbatia mdhambi na kumpatia tena neema ya kutubu na kumwongokea, tayari kuendelea na safari ya maisha ya kiroho. Huruma na upendo wa Mungu unajionesha katika maisha ya watu kwa kuwasaidia kutubu na kuongoka, ili hatimaye, kushirikiana na Mwenyezi Mungu kama vyombo na mashuhuda wake. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ameweza kuupatanisha ulimwengu wote pamoja naye na kwa Sakramenti ya Upatanisho, Mungu anachukua hatua ya kwanza ili kuonesha upendo kwa mdhambi, kama ilivyo kwa Mama Kanisa kuanza kwa ushupavu kuwaendea na kuwatafuta walioanguka na kutopea dhambini, waliotengwa na kuwakaribisha tena ili kuwaonjesha mang’amuzi ya huruma na upendo wa Mungu, ambayo ni matunda ya nguvu ya Baba isiyokuwa na kikomo!

Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao,  waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo! Kwa njia ya Sakramenti za Huruma ya Mungu, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaganga, kuwaponya na kuwasamehe watu wake dhambi zao. Katika kipindi hiki kigumu katika historia ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, kuna haja ya kugundua tena thamani ya ukimya katika maisha; fumbo la mateso na kifo katika maisha ya mwanadamu; umuhimu wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu hata katika mazingira ya kifamilia kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, Alhamisi Kuu ya Mwaka 2020 amesema kwamba,  Kristo Yesu kama kielelezo cha upendo mkuu kwa waja wake, aliamua kubaki kati yao kwa njia ya uwepo wake endelevu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kwa kushiriki kikamilifu, Mwili na Damu yake Azizi, waamini wanapata chakula kinachowapatia nguvu ya kwenda mbinguni.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha uwepo wa Kristo kati pamoja na wafuasi wake. Baba Mtakatifu anasema, huduma ya upendo inayotolewa kwa unyenyekevu ni kibali cha kuingilia mbinguni. Katika mahojiano kati ya Kristo Yesu na Mtakatifu Petro, Yesu anawakumbusha waja wake kwamba, hawana budi kumpatia nafasi ya kuwahudumia kwanza, kwani Kristo Yesu amejitambulisha kuwa ni Mtumishi mwaminifu wa Mungu, anayependa pia kuwahudumia wanadamu. Dhana hii ya huduma inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu si rahisi sana kuweza kueleweka, lakini hili ni sharti muhimu la kuweza kuingia katika Ufalme wa mbinguni. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wakleri wote, tangu yule mdogo kabisa ambaye amepewa Daraja Takatifu hivi karibuni hadi Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mapadre wamepakwa mafuta ili kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kuwahudumia watu wa Mungu kwa unyenyekevu!

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume anawahimiza waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kumwabudu Mungu katika: ukimya, sala na huduma kwa jirani. Mama Kanisa ana amini na kufundisha kwamba, uzima wa waamini hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakisha bomolewa, waamini wanakirimiwa makao ya milele mbinguni. Kumbe, mauti na kifo, kamwe hakiwezi kubomoa mahusiano na mafungamano ya waamini, bali yanaimarishwa zaidi katika muungano na watakatifu. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni muda muafaka wa kuwakumbuka na kuwaombea wakleri wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu wakati wa kipeo cha janga la maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna umati mkubwa wa wakleri ambao wameambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19 na wengi wao wamefariki dunia. Wote hawa wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa amani!

Moyo Mtakatifu wa Yesu 2020

 

 

19 June 2020, 14:16