Tafuta

Siku ya Uhuru wa Kidhamiri kwa Mara ya kwanza imeadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 5 Aprili 2020: Papa Francisko: Uhuru wa Kidhamiri Unapaswa kulindwa na wote! Siku ya Uhuru wa Kidhamiri kwa Mara ya kwanza imeadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 5 Aprili 2020: Papa Francisko: Uhuru wa Kidhamiri Unapaswa kulindwa na wote! 

Papa Francisko: Uhuru wa Dhamiri Unapaswa Kulindwa na Wote!

Jumuiya ya Kimataifa hivi karibuni imeadhimisha Siku ya Uhuru wa Kidhamiri Kimataifa. Hii ni siku ambayo inapata chimbuko lake kutoka kwenye ushuhuda wa Aristed de Sousa Mendes, Mwanadiplomasia kutoka Hispania. Alifuata dhamiri nyofu, akasimama kidete kulinda, kutetea na kuokoa maisha ya maelfu ya Wayahudi na wale wote waliokuwa wanateswa na kunyanyaswa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwanadamu anayo sheria moyoni mwake iliyoandikwa na Mwenyezi Mungu. Dhamiri yake ndio kiini cha ndani sana na siri kubwa ya mwanadamu, ndipo patakatifu ambamo yumo peke yake pamoja na Mwenyezi Mungu; ambamo sauti yake yasikika. Dhamiri adilifu iliyo moyoni mwa mtu yaamuru, wakati ufaao, kutenda mema na kuepuka mabaya. Yahukumu pia uchaguzi mmoja mmoja, ikithibitisha ulio mzuri na kulaumu ule mbaya. Hushuhudia mamlaka ya kweli kuhusu uzuri wa juu kabisa ambako mwanadamu avutiwa; na huzipokea amri. Anaposikiliza dhamiri yake, mtu mwenye busara aweza kumsikia Mungu anaposema. Mama Kanisa anatafsiri dhamiri kuwa ni hukumu ya akili ambamo mwanadamu hutambua sifa adilifu ya tendo halisi analoelekea kulitenda, angali akilifanya au amekwisha kulitekeleza. Katika yote asemayo na atendayo, mwanadamu hana budi kufuata kiaminifu anachojua kuwa ni haki na sahihi. Mwanadamu hufahamu na kutambua maagizo ya sheria ya Mungu kwa hukumu ya dhamiri yake. Hadhi ya binadamu yadokeza na kudai unyofu wa dhamiri adilifu.

Dhamiri yamwezesha mtu kuchukua madaraka ya matendo yaliyotekelezwa. Mtu ana haki ya kutenda katika dhamiri na uhuru ili afanye mwenyewe maamuzi adilifu. Mtu asishurutishwe kutenda kinyume cha dhamiri yake. Wala asizuiwe kutenda kadiri ya dhamiri yake, hususan katika mambo ya kidini. Rej. KKK. 1776 – 1802. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Jumuiya ya Kimataifa, wazo la kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Kidhamiri Kimataifa, lilitolewa tarehe 25 Julai 2019 kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Kwa mara ya kwanza Siku hii imeadhimisha tarehe 5 Aprili 2020, kwa kutafakari kuhusu amani duniani, kwa kuzingatia uhuru wa dhamiri na uwajibikaji kwa ajili ya mafao mapana zaidi ya binadamu. Kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na Maskini, ili kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto zinazoibuliwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ni wakati wa kufunda dhamiri, ili ziweze kuwa nyofu, kwa kuzingatia tunu, kanuni maadili na utu wema. Na kwa njia hii, watu watawajibika na kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni wakati wa kuamsha dhamiri zilizolala au kusinzia kwa kusimama kidete ili kutokubali mtu kuchezea dhamiri yako, kwani hapa ni mahali patakatifu sana. Ni wakati wa kuwajibika barabara kwa kuzingatia dhamiri nyofu, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 17 Juni 2020 mara baada ya Katekesi yake amesema hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa kwa mara ya kwanza imeadhimisha Siku ya Uhuru wa Kidhamiri Kimataifa. Hii ni siku ambayo inapata chimbuko lake kutoka kwenye ushuhuda wa Aristed de Sousa Mendes, Mwanadiplomasia kutoka Hispania.

Katika kipindi cha takribani miaka themanini iliyopita, aliamua kufuata dhamiri nyofu, akasimama kidete kulinda, kutetea na kuokoa maisha ya maelfu ya Wayahudi na wale wote waliokuwa wanateswa na kunyanyaswa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, uhuru wa kidhamiri utaheshimiwa, kila sehemu na kwamba, kila Mkristo atoe ushuhuda wa uhalisia wa maisha yake kwa kufuata dhamiri nyofu inayoangazwa na Neno la Mungu.

Papa: Dhamiri
17 June 2020, 12:25