Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sherehe ya Watakatifu Petro Paulo miamba wa imani amewataka waamini kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sherehe ya Watakatifu Petro Paulo miamba wa imani amewataka waamini kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.  (AFP or licensors)

Papa: Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Mashuhuda wa Imani

Akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 ametafakari kuhusu Mtume Petro na Paulo, Wasimamizi wa Mji wa Roma. Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni mahali ambapo inasadikiwa kwamba, Mtakatifu Petro aliuwawa na kuzikwa katika eneo hili. Safari ya maisha ya Mtakatifu Petro yanaweza kuwa ni dira ya maisha kwa wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuhitimisha maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume ambamo amefafanua kuhusu umoja na unabii, amewaongoza waamini kwa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana. Akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 ametafakari kuhusu Mtume Petro na Paulo, Wasimamizi wa Mji wa Roma. Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni mahali ambapo inasadikiwa kwamba, Mtakatifu Petro aliuwawa kikatili na kuzikwa katika eneo hili. Safari ya maisha ya Mtakatifu Petro inaweza kuwa ni dira kwa maisha ya waamini, kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya Mungu aliye hai! Baba Mtakatifu anasema, Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa Imani inatoa mwelekeo tofauti kabisa, yaani miaka kadhaa kabla ya Mtakatifu Petro hajaokolewa kutoka kwenye kifo!

Yakobo alikuwa ameuwawa, Mtume Petro alikuwa ametupwa gerezani, lakini Kanisa likawa linamwomba Mwenyezi Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Mara Malaika wa Bwana akasimama na kumwokoa kutoka kifungoni. Jambo la kujiuliza, ilikuaje, Mtakatifu Petro akaweza kuokolewa kutoka gerezani, lakini baadaye, akakumbana na mkono Herode? Hija ya maisha ya Mtakatifu Petro hapa ulimwenguni ni mwanga angavu unaoweza kuwaangazia hata waamini katika maisha yao. Mtakatifu Petro alibahatika kupata upendeleo na neema ya pekee kutoka kwa Kristo Yesu, akamwokoa kutoka katika taabu mbali mbali na ndivyo Mwenyezi Mungu anavyofanya kwa kila mwamini. Inasikitisha kuona kwamba, waamini wanamkimbilia Mwenyezi Mungu wanapokuwa katika shida na mahangaiko makubwa. Lakini, Mwenyezi Mungu anaona mbali zaidi na anawataka waja wake kupiga hatua kubwa zaidi, si tu kwa kutafuta zawadi, neema na baraka zake, bali kumtafuta Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Katika muktadha huu, waamini wawe na ujasiri wa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, huku wakimtolea shida na matatizo yao mbali mbali ya maisha, ili hatimaye, aweze kuwapatia neema kubwa zaidi ya kuweza kusadaka maisha yao, kwa kuyageuza kuwa ni zawadi kwa ajili ya wengine. Baba Mtakatifu anasema, changamoto hii, inawahusu na kuwagusa watu wote; wazazi wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya watoto wao; watoto wajitoe bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wazazi wao ambao ni wazee. Vivyo hivyo sadaka ya maisha inapaswa kujionesha kwa wanandoa pamoja na watawa. Sadaka hii ishuhudiwe sehemu mbali mbali, yaani: nyumbani, maeneo ya kazi na kwa jirani wenye uhitaji mkubwa zaidi. Mwenyezi Mungu anawataka waja wake, kukua na kukomaa katika sadaka ya maisha na kwa njia hii, wataweza kukomaa na kuwa watu wazima zaidi. Mtakatifu Petro hakubahatika kuwa shujaa wa imani kwa sababu aliokolewa kutoka gerezani, lakini kwa sababu aliweza kusadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Zawadi ya maisha yake imeugeuza Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuwa ni uwanja wa matumaini. Kumbe, waamini wanapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema na baraka si kwa ajili ya wakati huo huo, bali neema ya maisha. Mtakatifu Petro aliweza kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Na Kristo Yesu anamwambia Heri wewe Simoni Bar-yona, kwa maneno mengine ni kusema, heri wewe Petro ulibahatika kuwa na furaha katika maisha! Yaani kumtambua Kristo Yesu, kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Kumbe, haitoshi kwa mwamini kufahamu kwamba, Kristo Yesu alikuwa mtu maarufu sana katika historia, aliyetenda miujiza mingi, bali jinsi ambavyo mwamini anamtambua Yesu katika undani wa maisha yake. Ni katika utambuzi huu, Kristo Yesu anampatia Mtakatifu Petro dhamana kwamba, juu ya mwamba huu, atalijenga Kanisa lake. Ni mtu aliyekuwa na imani thabiti na aliyeaminika!

Hata katika dhamana hii, bado Mtakatifu Petro aliendelea kuandamwa na udhaifu wake wa kibinadamu, kiasi cha kufanya makosa, hadi kudiriki kumkana Yesu mara tatu! Mtakatifu Petro, alijitahidi kujenga maisha yake juu ya Kristo Yesu na wala hakujimwambafai kutokana na nguvu zake mwenyewe. Kumbe, Kwa Petro Mtume, Yesu akawa ni mwamba thabiti uliomtegemeza Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuchunguza hali ya maisha yao na hivyo kujiangalia ni wapi ambapo wamejielekeza na kujiaminisha zaidi. Je, ni watu wanaojifariji wao na mahitaji yao binafsi? Au wanatambua kwamba, kwa hakika wanamhitaji Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia neema ya kuwa ni zawadi kwa wengine. Waamini wanapaswa kujiuliza, Je, wanajenga namna gani maisha yao, kwa kujiamini wao wenyewe au wanamtegemea Mungu aliye hai? Bikira Maria aliyejiaminisha kwa Mwenyezi Mungu awasaidie waamini kumwilisha hali ya kujiaminisha kwa Mungu, kila siku ya maisha yao!

Papa: Petro na Paulo

 

 

29 June 2020, 14:00