Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu amebariki Pallio Takatifu 54 watakazovishwa Maaskofu wakuu walioteuliwa katika kipindi cha mwaka 2019-2020 Baba Mtakatifu amebariki Pallio Takatifu 54 watakazovishwa Maaskofu wakuu walioteuliwa katika kipindi cha mwaka 2019-2020  (Vatican Media)

Maaskofu Wakuu Wapya 54 Wapewa Pallio Takatifu: Ruwaichi, DSM!

Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu amebariki Pallio Takatifu 54 watakazovishwa: Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali. Maaskofu wakuu kutoka Barani Afrika ni 13 kati yao ni: Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, tarehe 29 Juni 2020 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa: Dekano wa Baraza la Makardinali pamoja na Maaskofu wakuu walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2019-2020. Pallio takatifu  ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu amebariki Pallio Takatifu 54 watakazovishwa: Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali. Maaskofu wakuu kutoka Barani Afrika ni 13 kati yao ni: Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama wa Jimbo Kuu Abuja, Nigeria.

Wengine ni: Askofu mkuu Nicodème Anani Barrigah-Benissan wa Jimbo kuu la Lomè, Togo. Askofu mkuu Ernest Ngboko Ngombe, wa Jimbo kuu la Mbandaka-Bikoro, Jamhuri ya Watu wa Congo. Askofu mkuu Gabriel Sayaogo wa Jimbo kuu Koupèla, Burkina Faso. Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin Mulla wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini. Askofu mkuu Andrew Nkea Fuanya wa Jimbo kuu la Bamenda, Cameroon. Askofu mkuu Matthew Ishaya Audu wa Jimbo kuu la Jos, Nigeria. Katika kundi hili wamo pia Askofu mkuu Jean-Patrick Iba-ba wa Jimbo kuu la Libreville, Gabon. Askofu mkuu Zolite Peter Mpambani wa Jimbo kuu la  Bloemfontein, Afrika ya Kusini. Askofu mkuu Lambert Bainomugisha wa Jimbo kuu la Mbarara, Uganda. Askofu mkuu Miguel Angel Olaverri Arroniz wa Jimbo kuu la Pointe-Noire, Jamhuri ya Watu wa Congo pamoja na Askofu mkuu Victor Abagna Mossa wa Jimbo kuu la Owando, Jamhuri ya Watu wa Congo.

Pallio Takatifu

 

29 June 2020, 14:38