Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza Maaskofu Katoliki Marekani kwa msimamo wao wa kichungaji katika muktadha wa machafuko ya kijamii yanayoendelea nchini Marekani. Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza Maaskofu Katoliki Marekani kwa msimamo wao wa kichungaji katika muktadha wa machafuko ya kijamii yanayoendelea nchini Marekani.  (AFP or licensors)

Papa: Awapongeza Maaskofu USA kwa Msimamo Wao wa Kichungaji

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Juni 2020 amewasiliana kwa njia ya simu na Askofu mkuu Josè H. Gomez, wa Jimbo kuu la Los Angeles na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, ili kuwapongeza kwa msimamo wao wa kichungaji waliouonesha katika kukabiliana na machafuko ya kijamii nchini Marekani. Ameonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, Jumatano, tarehe 3 Juni 2020, wakati wa salam na matashi mema kwa waamini, mahujaji na wageni mbali mbali, amesema kwamba, anaendelea kufuatilia kwa umakini na wasi wasi mkubwa machafuko ya kijamii yanayoendelea kujitokeza huko nchini Marekani kwa muda wa siku kadhaa sasa. Machafuko haya yamesababishwa na mauaji ya kikatili dhidi ya Bwana George Floyd. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Juni 2020 amewasiliana kwa njia ya simu na Askofu mkuu Josè H. Gomez, wa Jimbo kuu la Los Angeles na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, ili kuwapongeza kwa msimamo wao wa kichungaji waliouonesha katika kukabiliana na machafuko ya kijamii nchini Marekani.

Baba Mtakatifu ameonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa watu wa Mungu nchini Marekani, hasa katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha ya nchi yao. Askofu mkuu Gomez ameshirikishana na Maaskofu wenzake, ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ili waendelee kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu amewahakikishia watu wa Mungu nchini Marekani uwepo wake endelevu kwa njia ya sala. Amesema, kwa namna ya pekee, anapenda kumwombea Askofu Bernard A. Hebda pamoja na Kanisa mahalia la Mtakatifu Paulo na Jimbo la Minneapolis katika ujumla wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, limemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wake wakati wa Katekesi aliyoitoa Jumatano, tarehe 3 Juni 2020. Maaskofu kwa upande wao, wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko sala na sadaka zao kwa ajili ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anasema, ubaguzi wa aina yoyote ile ni jambo ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa wala kufumbiwa macho kwa kisingizio cha kulinda utakatifu wa maisha. Lakini, pia, watu wanapaswa kutambua kwamba, ghasia na vurugu za hivi karibuni, zimepelekea watu wengi kujeruhiwa pamoja na uharibifu mkubwa wa mali. Mambo mengi yanapotea kutokana na vita pamoja na ghasia. Baba Mtakatifu anapenda kuungana na Kanisa la Mtakatifu Paulo na familia ya Mungu mjini Minneapolis pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Marekani kwa ajili ya kumkumbuka na kuiombea roho ya Marehemu George Floyd pamoja na wale wote waliopoteza maisha kutokana na dhambi ya ubaguzi, ili waweze kupata faraja na maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu amewaombea ndugu, jamaa na marafiki wa George Floyd, faraja, amani na utulivu wa ndani. Ameliombea taifa la Marekani liweze kujikita katika upatanisho wa kitaifa, ili hatimaye, amani iweze kutawala. Baba Mtakatifu anasema, kwa maombezi ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika, awaombee wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushughulikia, haki na amani, ili viweze kutawala tena nchini Marekani na ulimwenguni kote!

Papa: Maaskofu USA
04 June 2020, 13:48