Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asema, ubaguzi ni dhambi kubwa, lakini vurugu na ghasia ni hatari kwa maisha na mali za watu! Kuna haja ya kujikita katika upatanisho wa kitaifa nchini Marekani. Baba Mtakatifu Francisko asema, ubaguzi ni dhambi kubwa, lakini vurugu na ghasia ni hatari kwa maisha na mali za watu! Kuna haja ya kujikita katika upatanisho wa kitaifa nchini Marekani.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Ubaguzi ni Dhambi Kubwa! Vurugu ni Hatari!

Machafuko haya yamesababishwa na mauaji ya kikatiliki dhidi ya Bwana George Floyd. Baba Mtakatifu anasema, ubaguzi wa aina yoyote ile ni jambo ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa wala kufumbiwa macho kwa kisingizio cha kulinda utakatifu wa maisha. Lakini, pia, watu wanapaswa kutambua kwamba, ghasia na vurugu za hivi karibuni, zimepelekea maafa makubwa kwa watu na mali .

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uwezekano wa kuishi pamoja kati ya Mataifa mbali mbali unategemezwa na misingi ileile ambayo ingekuwa ni miongozo ya uhusiano kati ya binadamu: ukweli, haki, mshikamano wa kweli kimatendo na uhuru. Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu kanuni za kikatiba juu ya jamii ya kimataifa yanasema kwamba, mahusiano kati ya watu na jumuiya za kisiasa yanaratibiwa kimantiki, kihaki, kisheria na kwa maafikiano bila vurugu au vita wala aina yoyote ya ubaguzi, vitisho na udanganyifu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi wa rangi na maamuzi mbele kwa kutambua kwamba, kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, Jumatano, tarehe 3 Juni 2020, wakati wa salam na matashi mema kwa waamini, mahujaji na wageni mbali mbali, amesema kwamba, anaendelea kufuatilia kwa umakini na wasi wasi mkubwa machafuko ya kijamii yanayoendelea kujitokeza huko nchini Marekani kwa muda wa siku kadhaa sasa. Machafuko haya yamesababishwa na mauaji ya kikatili dhidi ya Bwana George Floyd.

Baba Mtakatifu anasema, ubaguzi wa aina yoyote ile ni jambo ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa wala kufumbiwa macho kwa kisingizio cha kulinda utakatifu wa maisha. Lakini, pia, watu wanapaswa kutambua kwamba, ghasia na vurugu za hivi karibuni, zimepelekea watu wengi kujeruhiwa pamoja na uharibifu mkubwa wa mali. Mambo mengi yanapotea kutokana na vita pamoja na ghasia. Baba Mtakatifu anapenda kuungana na Kanisa la Mtakatifu Paulo na familia ya Mungu mjini Minneapolis pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Marekani kwa ajili ya kumkumbuka na kuiombea roho ya Marehemu George Floyd pamoja na wale wote waliopoteza maisha kutokana na dhambi ya ubaguzi, ili waweze kupata faraja na maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu amewaombea ndugu, jamaa na marafiki wa George Floyd, faraja, amani na utulivu wa ndani. Ameliombea taifa la Marekani liweze kujikita katika upatanisho wa kitaifa, ili hatimaye, amani iweze kutawala. Baba Mtakatifu anasema, kwa maombezi ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika, awaombee wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushughulikia, haki na amani, ili viweze kutawala tena nchini Marekani na ulimwenguni kote!

Wakati huo huo, Askofu mkuu Wilton D. Gregory wa Jimbo kuu la Washington, DC., nchini Marekani, anasema kwamba, amesikitishwa sana na kitendo cha Rais Donald Trump wa Marekani kutumia Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Kitaifa, kutaka kujijenga kisiasa. Si haki kwa Rais Trump kutumia Kanisa Katoliki kwa ajili ya mafao binafsi kisiasa, huku akitambua fika kwamba, anavunja haki msingi za binadamu. Kanisa linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, hata wale ambao hawawezi “kupikika chungu kimoja”. Mtakatifu Yohane Paulo II ni kiongozi aliyejipambanua kwa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki msingi za binadamu; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kwa hakika Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha amana, utajiri na ushuhuda mkubwa kuhusu tunu hizi msingi katika maisha ya binadamu.

Askofu mkuu Wilton D. Gregory wa Jimbo kuu la Washington, DC., nchini Marekani, anasema kwa hakika, Mtakatifu Yohane Paulo II hasingetumia mabomu ya machozi na silaha kali kwa ajili ya “kuwashikisha” adabu au kutaka kuwanyamazisha watu waliokuwa wanaandamana. Inasikitisha kwa Rais Trump kutumia Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II Kimataifa, mahali pa sana, amani na utulivu kwa ajili ya kujijenga kisiasa.

Papa: Vurugu nchini Marekani
03 June 2020, 14:12