Tafuta

Papa Francisko. Matakwa ya Kiinjili ni pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza pamoja na kuvumilia mateso na madhulumu kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Papa Francisko. Matakwa ya Kiinjili ni pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza pamoja na kuvumilia mateso na madhulumu kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. 

Papa Francisko: Matakwa ya Kiinjili: Sadaka na Uvumilivu wa Mateso!

Kristo Yesu katika Injili ya Mathayo, 10: 37-42, anawataka wanafunzi wake, kujizatiti zaidi kutekeleza matakwa ya Kiinjili hata pale wanapotakiwa kutoa sadaka kubwa pamoja na kuvumilia mateso. Jambo la kwanza kwa wafuasi wake ni kuhakikisha kwamba, wanatoa upendo wa dhati kwa Kristo Yesu, kama kipaumbele chao cha kwanza kushinda hata upendo kwa wazazi, ndugu na jamaa zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 27 Juni 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema, Kristo Yesu katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo, 10: 37-42, anawataka wanafunzi wake, kujizatiti zaidi kutekeleza matakwa ya Kiinjili hata pale wanapotakiwa kutoa sadaka kubwa pamoja na kuvumilia mateso. Jambo la kwanza kwa wafuasi wa Kristo ni kuhakikisha kwamba, wanatoa upendo wa dhati kwa Kristo Yesu, kama kipaumbele chao cha kwanza kushinda hata upendo kwa wazazi, ndugu na jamaa zao. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kwa masharti haya, si kwamba, Kristo Yesu, hathamini upendo kwa wazazi na watoto, bali anataka kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anakuwa ni dira na mwongozo wao wa maisha, vinginevyo wanaweza kuyumba na kupotea njia. Hata leo hii, rushwa, upendeleo wa ukabila na undugu bado ni changamoto kubwa katika misingi ya utawala bora.

Katika muktadha huu, kila mtu anao mfano halisi ambao anaweza kushirikisha katika tafakari hii. Wakati mwingine, vipaumbele, mahusiano na mafungamano ya kifamilia yanagumisha maamuzi ya Kiinjili. Lakini, pale ambapo upendo kwa wazazi na watoto umetakaswa kwa njia ya upendo unaobubujika kwa Kristo, hapo upendo huo unaweza kuzaa matunda mema ndani na nje ya familia yenyewe. Kuna baadhi ya watu wanaoikataa Amri ya Mungu ili kushika mapokeo yao! Lakini watu wanapaswa kuwaheshimu wazazi wao kwa kuhakikisha kwamba, wanapatia mahitaji yao msingi, vinginevyo wanatangua Neno la Mungu pamoja na mapokeo yao. Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuchukua misalaba yao na kufuata nyayo zake katika njia ile atakayopitia, bila kutafuta njia ya mkato. Upendo wa kweli una gharama na wakati mwingine gharama hii inalipwa na yule anayependa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kubeba Misalaba ya maisha yao kwa kusaidiana na Kristo Yesu.

Kwa njia hii, hawataweza kuogopa kwani Yesu, daima yuko pembeni mwao ili kuwasaidia wakati wa majaribu makubwa katika maisha, ili kuwakirimia ujasiri na nguvu ya kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mtu hawezi “kufua dafu kwa kujirusha chini kama gunia la Mahindi”, au kwa kuwa na woga usiokuwa na mashiko hata kidogo au kwa kuelemewa na ubinafsi, ili kuokoa maisha yake! Hata leo kuna kuna umati mkubwa wa watu unaowasaidia jirani zao, kubeba vyema misalaba yao Katika hali na mazingira kama haya, Kristo Yesu anasema “mwenye kuiona nafsi yake, ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafasi yake kwa Kristo Yesu ataiona”. Hii ndiyo changamoto ya Kiinjili. Lakini hata katika hili, bado kuna mifano lukuki. Utimilifu wa maisha na furaha ya kweli inapata chimbuko lake katika Injili na kati ya jirani, kwa kuwakunjulia mikono ya wema, kwa kuwakaribisha na kuwatakia mema.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni kwa kutekeleza haya, waamini wanaweza hata wao kuonja wema na shukrani kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu katika Injili anawakumbusha waja wake kwamba, mtu yeyote anayewapokea wao, anampokea pia Yeye; naye anayempokea Yesu anampokea pia Baba yake wa mbinguni, aliyemtuma. Kwa mtu yeyote atakayewatendea haki na ukarimu atapata pia thawabu yake. Ukarimu wa Mwenyezi Mungu unaangalia hata yale mambo madogo madogo yanayotendwa kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani. Huu ni utambuzi ambao unaambukizana na hivyo kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na moyo wa shukrani kwa watu wanaowahudumia, ili kuweza kupata mahitaji yao msingi. Watu wajenge utamaduni na moyo wa shukrani na kamwe wasidhani kwamba, huduma wanayopata ni haki yao.

Moyo wa shukrani ni kielelezo cha malezi bora na ni sehemu ya utambulisho na vinasaba vya maisha ya Mkristo. Ni alama ya kawaida, lakini inapata chimbuko lake katika Ufalme wa Mungu ambao unasimikwa katika upendo wenye sadaka na moyo wa shukrani. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amesema, Bikira Maria alimpenda sana Mwanaye Kristo Yesu, kuliko hata maisha yake na kuthubutu kumfuata katika Njia yake ya Msalaba, asaidie kuwaombea waamini mbele ya Mwenyezi Mungu ili wawe na moyo ulio tayari kwa kuliachia Neno la Mungu ili liweze kuhukumu matendo na maamuzi yao.

Papa: Ukarimu
28 June 2020, 13:55