Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asema, Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni shuhuda jasiri wa Injili, awasaidie waamini kusimama kidete kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili! Baba Mtakatifu Francisko asema, Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni shuhuda jasiri wa Injili, awasaidie waamini kusimama kidete kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili!  (Vatican Media)

Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji: Ujasiri wa Kiinjili!

Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji, aliyebahatika kumtangulia Kristo Yesu, ili kumwandalia njia, awasaidie kuwa mashuhuda jasiri wa Injili, kwa kuvunjilia mbali tofauti, ili kujenga na kudumisha maridhiano na urafiki nguzo msingi na inayoaminika katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala, Jumatano tarehe 24 Juni 2020, amedadavua kuhusu sala ya Mfalme Daudi. Amesema, sala ni ufunguo na ngazi ya kupandia kwenda mbinguni. Mfalme Daudi anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kugeuza: mateso, furaha, mahangaiko na machungu ya maisha; wasi wasi na matumaini kuwa ni chemchemi ya sala zao. Ni katika muktadha huu, maisha yanageuka kuwa ni kielelezo makini cha sala ambayo inageuka kuwa maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiaminisha mbele ya Kristo Yesu, Mchungaji mwema, Mpole na Mnyenyekevu wa moyo, anayewakirimia waja wake: faraja, huruma na msamaha wa dhambi, ili aweze kuwasindikiza kwenye chemchemi ya furaha na utukufu wa Baba yake wa mbinguni.  Kwa wananchi wengi Barani Ulaya na Marekani, wameanza likizo ya kipindi cha kiangazi kwa mwaka 2020.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, muda huu utawawezesha watu kupata amani na utulivu wa ndani. Ni fursa ya kuweza kutafakari kazi ya uumbaji, iliyofanywa na Mungu muumbaji Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Juni, anaadhimisha Siku kuu ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Huyu ni Mtakatifu pekee, ambaye Mama Kanisa anaadhimisha Siku yake ya kuzaliwa. Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji, aliyebahatika kumtangulia Kristo Yesu, ili kumwandalia njia, awasaidie kuwa mashuhuda jasiri wa Injili, kwa kuvunjilia mbali tofauti, ili kujenga na kudumisha maridhiano na urafiki nguzo msingi na inayoaminika katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Tangu tumboni mwa Mama yake Elizabeth, Yohane Mbatizaji alikuwa ni mtangulizi wa Yesu, akaonesha kwamba, hakuna jambo lisilowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hiki ni kielelezo makini cha uhusiano wa kina kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu, kwa njia ya Roho Mtakatifu. Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyefunga Agano la Kale, akawa daraja ya Agano Jipya, aliyemwandalia njia na hatimaye, wakati ulipowadia akamtambulisha Yesu kuwa ni Masiha, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Watu wengi walimfananisha Yohane Mbatizaji na Nabii Elia aliyewatakasa Waisraeli kutoka katika ibada ya kuabudu miungu na kuwarejesha tena katika imani ya kweli iliyokita mizizi yake kwa Mwenyezi Mungu aliye hai, yaani Mungu wa Abramu, Isaka na Yakobo. Yohane Mbatizaji alihubiri juu ya uwepo wa Masiha ambaye atajifunua kwao. Yohane Mbatizaji aliwataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa.

Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu akamshukia Kristo Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Yesu Kristo ni Masiha wa Bwana. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, tukio hili lilimshangaza sana Yohane Mbatizaji, kumwona Yesu akiwa kati kati ya kundi kubwa la wadhambi kama wao, lakini kwa ajili yao, ili aweze kubatizwa na kutekeleza haki yote sanjari na mpango wa wokovu wa Mungu. Yesu Kristo anajionesha kama Mwana kondoo wa Mungu anayeichukua na kuondoa dhambi ya ulimwengu. Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha kuwa Kristo Yesu ndiye Mwana kondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Yesu! Hawa ndio akina Simone aitwaye Petro, na Andrea nduguye, Yakobo na ndugu yake Yohane, wote hawa walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya kama ilivyokuwa kwa Yesu.

Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyetangaza na kusimamia ukweli, aliyekatwa kichwa na wafuasi wake waliposikia wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika kwa heshima! Hivi ndivyo nyota angavu ya Yohane Mbatizaji, ilivyozimika baada ya kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Yohane Mbatizaji, kati ya watu maarufu wa Agano Jipya, anaishia kukatwa kichwa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kifodini ni huduma, utume na zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifodini ni kielelezo cha ukatili wa binadamu dhidi ya watu waaminifu.

Papa: Yohane Mbatizaji
25 June 2020, 13:40