Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa tarehe 25 Juni 2020 imeadhimisha Siku ya Mabaharia Duniani: Papa Francisko amewatumia ujumbe wa matumaini na faraja! Jumuiya ya Kimataifa tarehe 25 Juni 2020 imeadhimisha Siku ya Mabaharia Duniani: Papa Francisko amewatumia ujumbe wa matumaini na faraja!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Siku ya Mabaharia Duniani: Faraja na Matumaini!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha Siku ya Mabaharia Duniani anasema, mabaharia pamoja na wavuvi ni kati ya wafanyakazi mashuhuri, wanaosaidia kusongesha mbele gurudumu la maendeleo fungamani duniani. Katika maadhimisho haya, anapenda kuwatumia salam na matashi mema, yanayofumbatwa katika matumaini na faraja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha Siku ya Mabaharia Duniani anasema, mabaharia pamoja na wavuvi ni kati ya wafanyakazi mashuhuri, wanaosaidia kusongesha mbele gurudumu la maendeleo duniani. Katika maadhimisho haya, anapenda kuwatumia salam na matashi mema, yanayofumbatwa katika matumaini na faraja. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres katika maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Juni, anasema, Mabaharia ni kati ya mashujaa wasiokumbukwa sana na Jumuiya ya Kimataifa, licha ya mchango wao mkubwa katika medani mbali mbali za maisha. Hawa ni watu wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwa weledi mkubwa, nidhamu na sadaka kubwa ya maisha, ili kuhakikisha kwamba, bidhaa muhimu zinawafikia walengwa kwa wakati muafaka. Hata katika kipindi hiki cha janga kubwa la maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mabaharia bado wameendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu. Wameendelea kukabiliana na matatizo na changamoto nyingi, kiasi hata cha kuwakatisha tamaa. Mwaka 2020, Jumuiya ya Kimataifa inapenda kuwashukuru na kuwapongeza kwa mchango wao mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Wakati huo huo, Shirika la Kazi Duniani, ILO, limezitaka mamlaka za serikali, uhamiaji, afya na masuala ya bahari kushirikiana na kushikamana ili kutambua kwamba mabaharia ni wafanyakazi muhimu ambao wanahakikisha kuendelea kwa biashara na usafirishwaji wa dawa muhimu, vifaa vya ulinzi na usalama, chakula na bidhaa nyingine muhimu zinazohitajika katika mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hii ni changamoto kwa Serikali mbali mbali kuhakikisha kwamba zinaridhia Mkataba wa Ajira za Usafiri wa Bahari wa Mwaka 2006, kwa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, COVID-19. Kutokana na hofu ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, mabaharia wengi walizuiliwa kwenye meli zao, hali ambayo imepelekea mabaharia wengi kuanza kusumbuliwa na afya ya akili, uchovu pamoja na kupunguza uwezo wao wa kufanya kazi. Hali ya mabaharia kuendelea kufanya kazi katika mazingira haya magumu na hatarishi ni hatari sana kwa mabaharia weyewe, hali ambayo pia inahatarisha usalama wa baharini amesema Bwana Guy Ryder, Mkurugenzi mkuu wa wa Shirika la Kazi Duniani, ILO.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa mabaharia pamoja na familia zao anasema, Jumuiya ya Kimataifa inapitia kipindi kigumu katika historia yake kutokana na janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Maisha na kazi ya mabaharia pamoja na wavuvi imeonesha umuhimu wake wa pekee katika kipindi hiki, kwa sababu wamesaidia sana kutoa chakula pamoja na mahitaji msingi kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza na kuwashukuru kwa sadaka na majitoleo yao. Anatambua fika hatari za maisha wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Katika miezi ya hivi karibuni, maisha na kazi za mabaharia pamoja na wavuvi zimebadilika sana, kwa sababu wanapaswa kuendelea kujisadaka zaidi bila ya kujibakiza. Wametumia muda mrefu zaidi wakiwa kwenye vyombo vyao bila ya kuruhusia kutua nanga kwa hofu ya kusambaza maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19. Wameendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kutengwa na ndugu, jamaa, marafiki na hata nchi zao wenyewe.

Matatizo na changamoto zote hizi si rahisi sana kwa wao kuweza kuzibeba na hasa katika kipindi hiki! Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia kwamba, wasidhani wako pweke na kwamba, wamesahauliwa. Kwa njia ya maisha na utume wao baharini unaweza kuwajengea mazingira kwamba, wako pweke, lakini watambue kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawahifadhi na kuwaombea kila wakati kutoka katika undani wa moyo wake. Sala hii inasindikizwa pia na wahudumu wa maisha ya kiroho pamoja na watu wa kujitolea wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwenye Utume wa Bahari, maarufu kama “Stella Maris” yaani “Nyota ya Bahari”. Injili Takatifu inawakumbusha waamini kwamba, Mitume wa kwanza wa Kristo Yesu, walikuwa ni wavuvi. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kuwapatia ujumbe; sala ya matumaini na faraja mintarafu matatizo na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu anapenda pia kuwatia shime, wahudumu wa maisha ya kiroho na watu wa kujitolea, wanaoshirikiana nao bega kwa bega katika utume wa bahari kwa ajili ya mabaharia na wavuvi. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea wote pamoja na familia zao, heri na baraka. Anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira maria, Nyota ya uinjilishaji. Mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume na kuendelea kuwahakikishia kwamba, daima wako kwenye mawazo na sala zake. Amewasihi wao pia kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Siku ya Mabaharia Duniani 2020
25 June 2020, 13:55