Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asema, Ekaristi Takatifu ni Zawadi na Kumbukumbu ya Matendo Makuu ya Mungu katika maisha ya waja wake. Baba Mtakatifu Francisko asema, Ekaristi Takatifu ni Zawadi na Kumbukumbu ya Matendo Makuu ya Mungu katika maisha ya waja wake. 

Papa: Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Kumbukumbu Endelevu!

Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu amekazia kuhusu: Ekaristi kama kumbukumbu ya matendo makuu ya Mungu na Pasaka ya Kristo Yesu. Ekaristi Takatifu ni tiba muafaka ya kumbukumbu yatima, yenye mwelekeo hasi na ambayo imejifungia katika ubinafsi wake, ili hatimaye, kujenga na kudumisha mnyororo wa upendo, umoja na mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha, utume na muhtasari wa imani ya Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Huu ni ukumbusho wa maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu na sala ya waja wake mbele ya Baba yake wa Mbinguni. Ni fumbo Linalohitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Hili ni Fumbo kubwa linalopaswa kuadhimishwa vyema; Kuabudiwa na Kutafakariwa kikamilifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu ya Bwana Wetu Yesu Kristo, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 14 Juni 2020 amekazia kuhusu: Ekaristi kama kumbukumbu ya matendo makuu ya Mungu na Pasaka ya Kristo Yesu. Ekaristi Takatifu ni tiba muafaka ya kumbukumbu yatima, yenye mwelekeo hasi na ambayo imejifungia katika ubinafsi wake, ili hatimaye, kujenga na kudumisha mnyororo wa upendo na mshikamano! Musa katika Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati, anawaalika Waisraeli kuikumbuka njia yote ya Bwana Mungu wao. Baba Mtakatifu anasema, waamini wamepewa Maandiko Matakatifu ili wasimsahau Mwenyezi Mungu aliyefanya mambo ya ajabu katika nchi ya Misri. Bila kumbukumbu endelevu, waamini watagenishwa na kuwa ni wapita njia tu; watapeperushwa na kukumbwa na kimbunga kikali.

Kumbukumbu endelevu inawaimarisha waamini katika mambo msingi ya kihistoria na utambulisho wao kama jamii ya watu. Kumbukumbu inawaunganisha waamini kati yao wenyewe na kati yao na Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo kumbukumbu endelevu ambayo Waisraeli walipaswa kuwarithisha watoto wao, kwa kuwasimulia kwamba, kuna wakati katika historia, walikuwa watumwa wa Farao huko Misri; Mwenyezi Mungu akawatoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu. Akaonya ishara na maajabu, makubwa na mazito mbele ya macho yao. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mwenyezi Mungu amewaachia waja wake kumbukumbu endelevu si tu katika: Neno lake kwa sababu ni rahisi mno kuweza kusahau; amewaachia Maandiko Matakatifu, lakini ni rahisi mno kusahau kile ambacho mtu amesoma. Amewaachia alama, lakini pia mtu anaweza kusahau kile alichoona. Lakini kubwa zaidi ni kwamba, Kristo Yesu amewaachia waja wake Chakula ambacho si rahisi sana kusahau ladha yake.

Kristo Yesu ni Mkate wa uzima na chemchemi ya upendo! Ndiyo maana amewaamuru waja wake kumkumbuka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Pasaka ya Bwana inayopyaishwa kwa ajili ya waja wake. Katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu waamini wanafanya kumbukumbu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Hii ni Ibada inayoadhimishwa kama familia, jumuiya ya waamini na watu wa Mungu, kwa sabababu hii ni kumbukumbu ya uwepo endelevu wa Mungu inayoganga na kuponya kumbukumbu ya waamini ambayo imejeruhiwa. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanaganga na kuponya kumbukumbu yatima! Hii ni kutokana na ukosefu wa upendo wa dhati na usaliti ambao umewapokonya watu upendo, na kuiacha roho kama “mtoto yatima”. Si rahisi kurejea tena nyuma kwenye historia ili kupyaisha tena yale mambo ya zamani.

Mwenyezi Mungu anaganga na kuponya kumbukumbu hii kwa kuwakirimia waja wake upendo usiokuwa na mipaka. Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini upendo aminifu wa Mungu, unaoganga na kuponya uyatima wao. Mwenyezi Mungu anawakarimia upendo wa Kristo Yesu, aliyegeuza kaburi kuwa ni mwanzo na mwisho katika maisha ya waamini. Mwenyezi Mungu anawakirimia  upendo wa Roho Mtakatifu, unaowafariji, ili wasibaki pweke, bali anauguza na kufunga jeraha zao! Ekaristi Takatifu inaganga na kuponya kumbukumbu hasi, kwa kuondokana na “majigambo” yanayowaacha kwenye huzuni, kwa kuwaaminisha kwamba, wao si mali kitu! Ni watenda maovu. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anawajia waja wake, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na waja wake, kila mara wanapompokea kwa kuwakumbusha kwamba, wana thamani kubwa. Wamealikwa kwenye Karamu ya Bwana kwa sababu ya ukarimu na upendo wake wa hali ya juu. Mwenyezi Mungu anawakumbusha waja wake kwamba dhambi na ubaya wa moyo si sehemu ya vinasaba vya utambulisho wao na badala yake ni magonjwa. Ekaristi Takatifu ni kinga madhubuti kwa ajili ya kumbukumbu ambazo zinashambuliwa na magonjwa. Kwa njia hii, Kristo Yesu anapenda kuwapatia kinga.

Daima, waamini mbele ya macho yao wataendelea kuona jinsi wanavyoteleza na kuanguka; mateso na mahangaiko yao ya kila siku; matatizo na changamoto zinazoendelea kuibuliwa nyumbani na maeneo ya kazi. Wataendelea kuona ndoto zao zinayeyuka na kupotea kama “umande wa asubuhi”. Lakini ikumbukwe kwamba, uzito wa matendo yote haya, kamwe hauwezi kuwakandamiza na kuwazamisha chini kabisa “kama soli ya kiatu”! Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu ni msingi wa maisha yao, anayewatia shime kwa njia ya upendo wake wa dhati! Ekaristi Takatifu inawawezesha waamini kuwa ni vyombo vya kumbebea Mungu na mashuhuda wa furaha. Baba Mtakatifu anapenda kuwauliza waamini baada ya maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni mambo yepi wanayowashirikisha walimwengu wengine? Je, ni huzuni, machungu ya moyo au furaha ya Kristo Yesu? Inasikitisha kuona kwamba, watu wanakula “Chakula cha Malaika” kilichoshuka kutoka mbinguni, lakini midomoni mwao, ni watu wa kulalama daima, kwa kuwashambulia jirani zao na hatimaye, kujililia wenyewe. Ikumbukwe kwamba, furaha ya kweli inapyaisha na kuleta mabadiliko katika maisha.

Ekaristi Takatifu anasema Baba Mtakatifu Francisko inaganga na kuponya kumbukumbu zilizojifungia katika ubinafsi kutokana na madonda makubwa wanayobeba ndani mwao, kiasi cha kuleta usumbufu si tu kwa waamini wenyewe bali hata pia kwa jirani zao. Wanawaona jirani zao kuwa kama tishio na watu wakutiliwa mashaka kila wakati, na baada ya muda mrefu, hali hii inawajengea waamini ukavu wa maisha ya kiroho na tabia ya kutojali. Matokeo yake ni kiburi na jeuri kama njia ya kudhibiti hali ilivyo. Lakini, ikumbukwe kwamba, upendo unaganga na kuponya kutoka katika mzizi wake wa hofu na kuwaweka huru kutoka katika mambo yaliyowafunga. Hivi ndivyo anavyofanya Kristo Yesu anapowaendea waja wake katika Fumbo la Ekaristi. Kristo Yesu anakuwa ni Mkate uliomegwa ili kuvunjilia mbali ubinafsi; anajitoa na kujisadaka, ili kuwakomboa kutoka katika mambo yanayogumisha undani wa maisha na roho zao.

Kristo Yesu anajitoa mwenyewe kama sadaka katika maumbo ya Mkate na Divai, changamoto na mwaliko wa kuvunjilia mbali mambo yasiyo msingi yanayowafanya kuendelea kuwa tegemezi, hali inayowaachia waamini utupu katika maisha yao ya ndani! Ekaristi Takatifu inawasha moto wa upendo na kiu ya kutaka kuhudumia. Inawainua na kuwakumbusha kwamba, si tu kwamba, wanapaswa kulishwa kama “makinda ya ndege”, lakini wao pia, ni mikono ya Mungu kwa ajili ya kuwalisha jirani. Baba Mtakatifu anasema kwamba, huu ni wakati muafaka wa kusimama kidete ili kupambana na baa la njaa kwa kuwalisha wenye njaa; kuendelea kupigania: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa wasiokuwa na ajira na maskini ambao wanaendelea kupambana na hali ngumu ya maisha. Mawazo haya mazuri yanapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kama Chakula kinachotolewa na Kristo Yesu. Lengo ni kujenga mnyororo wa upendo na mshikamano, kwa sababu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anakuwa jirani zaidi kwa waja wake na anaendelea kuambatana nao, ili kamwe wasibaki kuwa wapweke.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini kuendelea kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu linaloganga na kuponya kumbukumbu yao. Ibada ya Misa Takatifu ni amana na utajiri unaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ndani ya Kanisa na katika maisha. Ni wakati muafaka wa kugundua tena na tena umuhimu wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Kwa hakika, waamini wanapaswa kugangwa na kuponywa kutoka katika undani wao na hasa kwa wakati huu! Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu amewaongoza waamini kuabudu Ekaristi Takatifu na baadaye, akawabariki kwa Sakramenti kuu. Ibada hii imefanyika ndani ya Kanisa kwa kuzungatia Protokali ya kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa mwaka 2020, sehemu kubwa ya Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, yamefanyika bila maandamano ya Ekaristi Takatifu, kielelezo na ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo anayefanya hija na waja wake, kama ilivyokuwa kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya.

Papa: Ekaristi 2020
14 June 2020, 14:17