Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono jitihada za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU pamoja na Umoja wa Mataifa kuhusu hatima ya Siria pamoja na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono jitihada za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU pamoja na Umoja wa Mataifa kuhusu hatima ya Siria pamoja na Mashariki ya Kati katika ujumla wake.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Mkutano IV wa Kimataifa Kuhusu Siria! Amani!

Jumanne, tarehe 30 Juni 2020, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa wanafanya Mkutano IV wa Kimataifa kuhusu Hatima ya Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati. Imegota miaka kumi tangu Siria ilipotumbukia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoungwa mkono na Mataifa makubwa duniani, kila taifa likijitahidi kutetea mafao yake binafsi. AMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 28 Juni 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameyaelekeza macho na mawazo yake mjini Brussels, nchini Ubelgiji, ambako, Jumanne, tarehe 30 Juni 2020, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa wanafanya Mkutano IV wa Kimataifa kuhusu Hatima ya Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati. Imegota miaka kumi tangu Siria ilipotumbukia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoungwa mkono na Mataifa makubwa duniani, kila taifa likijitahidi kutetea mafao yake binafsi. Vita ya Siria imekwisha kusababisha mamilioni ya watu kukimbia makazi na nchi yao wenyewe na kuna maelfu ya wananchi ambao hawana makazi ya kudumu. Matatizo na changamoto zote hizi, zimegumishwa zaidi kutokana na janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna watoto wanaoendelea kufariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Umefika wakati kwa Jumuiya ya KImataifa kujizatiti kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, kweli amani na utulivu vinapatikana nchini Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati

Mkutano huu wa Kimataifa unapania pamoja na mambo mengine, kupembua kwa kina na mapana hali halisi ya Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Ni fursa ya kuangalia hali ya siasa mtambuka na suluhu zake; mchakato wa kutafuta fedha ili kuweza kugharimia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Siria wanaopata hifadhi katika nchi jirani pamoja na kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendeleza majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Huu ni wakati muafaka wa kuangalia mahitaji msingi ya binadamu, usitishwaji wa mapambano ya kivita na kuanza kujielekeza zaidi katika suluhu ya kisiasa. Hizi ni juhudi za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU kutaka kuunga mkono sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa, ili kuweza hatimaye, kupata suluhu ya amani nchini Siria na katika Ukanda wa Mashariki ya Kati. Ni wakati wa kuendelea kukazia umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kuziwezesha nchi za Lebanon, Yordan na Uturuki zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa katika nchi hizi.

Misri na Iraq nazo zitashirikisha matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika kipeo kizima cha vita huko Mashariki ya Kati. Mkutano huu wa Kimataifa, utawashirikisha pia wadau kutoka katika Mashirika ya Kimataifa, Asasi za Kiraia pamoja na nchi wahisani wanaotoa hifadhi kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisasa kutoka Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kuombea Mkutano IV wa Kimataifa kuhusu Hatima ya Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati, ili uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani, amani, utulivu na maridhiano kati ya watu, chachu muhimu sana katika mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu. Mkutano huu, usaidie maboresho ya maisha ya watu wa Mungu nchini Siria na Lebanon kutokana na matatizo na changamoto zinazotokana na hali tete ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea wananchi wa Yemen, na hasa zaidi watoto na wanawake wanaoteseka kutokana na mapambano ya silaha nchini humo. Amewakumbuka pia wananchi wa Ukraine ya Magharibi ambao wamekumbwa na mafuriko ambayo kwa hakika yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wote hawa, Baba Mtakatifu amewaombea faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mshikamano wa upendo kutoka kwa Wasamaria na majirani wema, ambao wako tayari kuwasaidia ndugu zao kwa hali na mali! Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa waamini walioshiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa kufuata Madhehebu ya Kikongo, kwa ajili ya kuwaombea watu wa Mungu nchini DRC.

Papa: Siria
28 June 2020, 14:15