Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 20 Juni 2020 amekutana na kuzungumza na familia ya Mungu kutoka mkoa wa Lombardia, mkoa ulioathirika sana na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 20 Juni 2020 amekutana na kuzungumza na familia ya Mungu kutoka mkoa wa Lombardia, mkoa ulioathirika sana na Virusi vya Corona, COVID-19.  (ANSA)

Hotuba ya Papa Francisko kwa Ujumbe Kutoka Lombardia! COVID-19!

Papa Francisko amegusia: Madhara yaliyosababishwa na COVID-19; Mashuhuda wa huruma na upendo waliojitokeza kuwahudumia na kuwasaidia waathirika. Ametaja matarajio yake baada ya kipeo cha ugonjwa wa COVID-19; kiroho na kimaadili, kwa kuambata na neema ya Mungu. Ni wakati wa kuendeleza mema na mazuri yaliyojitokeza wakati wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ya watu wa Mungu nchini Italia ni kati ya watu walioguswa na kutikiswa na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hadi kufikia Jumamosi asubuhi, tarehe 20 Juni 2020, takwimu za Serikali ya Italia zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 238, 000 wameambukizwa, wagonjwa 182,000 wamebahatika kupona na watu zaidi 34, 561 wamefariki dunia kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Maeneo yaliyoathirika sana ni Milano, Bergamo, Brescia, Cremona na Lodi. Kimsingi hili ni eleo la Mkoa wa Lombardia, ulioko Kaskazini mwa Italia. Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, Hospitali ya “Spallanzani” iliyoko mjini Roma, ambayo ni maarufu kwa kutibu magonjwa ya Ukanda wa Joto, imekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Wajumbe kutoka katika maeneo haya, Jumamosi, tarehe 20 Juni 2020 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Hii ni mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu kufanya mazungumzo na kundi kubwa la watu tangu itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ilipopitishwa nchini Italia. Katika hotuba yake, amegusia madhara yaliyosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19; Mashuhuda wa huruma na upendo waliojitokeza kuwahudumia na kuwasaidia waathirika kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Baba Mtakatifu ametaja matarajio yake baada ya kipeo cha ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19; kiroho na kimaadili, kwa kuambata na kushikamana na neema ya Mungu. Ni wakati wa kuendeleza mema na mazuri yaliyojitokeza wakati wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wadau mbali mbali walijitokeza na kujifunga kibwebwe kupambana na janga kubwa la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa ukarimu na uwajibikaji mkuu. Hizi ni juhudi zilizowaunganisha watu katika ngazi mbali mbali za maisha ya kijamii na kiroho. Madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Wametekeleza dhamana hii kwa moyo mkuu na ushupavu wa hali ya juu kabisa kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao na familia zao. Kuna baadhi yao wameambukizwa na wengine wamefariki dunia kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Lakini watu wameshuhudia jinsi ambavyo wadau mbali mbali walivyojisadaka kwa ajili ya huduma; wote hawa wamekumbukwa na Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake.

Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya wamejipambanua kuwa ni kimbilio salama kwa wagonjwa lakini kwa namna ya pekee wanafamilia ambao waliweka matumaini yao kwa wafanyakazi hawa kwa sababu hawakuwa na nafasi ya kuweza kuwatembelea ndugu zao. Ni katika muktadha huu, wafanyakazi katika sekta ya afya wakaunganisha taaluma na weledi kuwa ni chemchemi ya upendo. Wagonjwa wakajisikia kuwa kandoni mwao, walikwepo “Malaika walinzi” waliowasaidia kuboresha tena afya zao; wakawafariji katika mateso na mahangaiko yao ya ndani; wakawatia shime katika safari yao kuelekea kwenye maisha na uzima wa milele, ili kukutana na Mwenyezi Mungu. Wafanyakazi hawa wamekuwa kweli mashuhuda, vyombo na madaraja ya kuwakutanisha wagonjwa na ndugu zao hata katika mambo ya madogo madogo kama kuwaunganisha kwa njia ya simu. Wadau katika sekta ya afya, walipata nguvu, ari na mwamko mkuu wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuungwa mkono na viongozi wa maisha ya kiroho wanaotekeleza dhamana na wajibu wao hospitalini.

Viongozi hawa wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma, upendo na uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na wagonjwa. Walitekeleza wajibu huu katika hali ya ukimya pasi na makuu, wakawa ni wasanii wa utamaduni wa udugu na huruma ya Mungu. Walimwengu wakashuhudia kwa macho yao makavu, wema na uzuri wa kazi yao katika hali na mazingira hatarishi. Walikosa hata mahali pa kulaza vichwa vyao. Walichoka na hata wakati mwingine kukata tamaa, lakini bado waliendelea kutekeleza wajibu wao kwa weledi kwa kujitoa bila ya kujibakiza hata kidogo na hiyo ikawa ni chemchemi na nguzo ya matumaini kwa watu wa Mungu nchini Italia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kwa moyo wake wote kuwashukuru madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya kwa sadaka na majitoleo yao katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Ni katika muktadha huu, wadau mbali mbali katika sekta ya afya waliwekeza sana nguvu kubwa na wakati mwingine, nguvu hii imepotea wakati wa kupambana na dharura ya janga la Corona, COVID-19. Lakini, hata katika mazingira kama haya, bado sehemu kubwa ya nguvu iliyowekezwa imezaa matunda kwa wakati huu na kuweka matumaini thabiti kwa siku zijazo mkoani Lombardia na Italia katika ujumla wake. Janga la Corona, COVID-19 limegusa na kutikisa maisha ya watu na historia ya Jumuiya. Kuna kila sababu ya kuendelea kuenzi mateso ya wagonjwa na wale wote waliofariki dunia; hususan wazee. Hili ni kundi ambalo kamwe, uzoefu na mang’amuzi yao ya maisha hayawezi kusahauliwa, kwa ajili ya ujenzi wa kesho iliyo bora zaidi. Hii ni dhamana inayohitaji uwajibikaji na sadaka ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa upendo wenye ukarimu pasi na makuu ambao umeacha chapa ya kudumu na isiyoweza kufutika kwenye dhamiri na mafungamano ya kijamii, kwa kuwafundisha watu umuhimu wa ujenzi wa ujirani mwema; huduma makini na sadaka kwa ajili ya kuhamasisha udugu wa kibinadamu na utulivu mkubwa.

Inawezekana kabisa, watu wa Mungu kutoka katika kipeo hiki cha mahangaiko ya maisha ya kiroho, kanuni maadili na utu wema, wakiwa imara zaidi, mambo yanayotegemea dhamiri nyofu na uwajibikaji wa kila mmoja, kwa kutegemea na kuambata neema ya Mungu. Ni wajibu wa waamini kutangaza na kushuhudia kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha waja wake, hata katika udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika Fumbo la Msalaba, hata waamini nao kwa msaada wa Mwenyezi Mungu wanaweza kupambana na matatizo na changamoto pevu, hatimaye wakaweza kuibuka kidedea! Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu ili aweze kujenga umoja na udugu wa kibinadamu, ili kuondokana na dhana ya uchoyo na ubinafsi, mambo yanayoonekana kuwa kama ni dira na mwongozo wa maisha ya walimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa angalisho kwa watu wote wa familia ya Mungu kutojisahau kwani mara tu baada ya kipeo cha janga la Corona, COVID-19 wakajikuta wakitumbukia katika ombwe na hali ya kufikirika. Ni rahisi sana kuwasahau majirani; au watu wengine wanaowahudumia; kwamba, kuna watu wanaowatia shime na ujasiri wa kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Watu wote wanamhitaji Mungu Baba Mwenyezi, anayeweza kuwashika mkono. Kumwomba Mungu kwa sala si dhana ya kufikirika, mbaya zaidi ni kufikiri na kutenda kana kwamba, hakuna Mungu. Sala ni kiini cha matumaini.Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, wakati wa janga la maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kuna umati mkubwa wa waamini umeshindwa kuhudhuria katika maadhimisho ya Ibada na Liturujia mbali mbali za Mama Kanisa, lakini bado waliendelea kujisikia kuwa ni sehemu ya Jumuiya ya waamini. Wamesali na kutafakari sana Neno la Mungu kama mtu binafsi na hata kama familia, huku wengi wao wakisaidiwa na vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Kwa njia hii, wameshikamana katika maisha ya kiroho, wakitambua kwamba, Kristo Yesu alikuwa anawakumbatia hata nje ya mipaka ya maeneo yao. Kuna baadhi ya vijana walikuwa wakorofi kiasi cha kushindwa kuzingatia sheria, taratibu na itifaki dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Mapadre wengi wameonesha ari na mwamko wa shughuli za kichungaji kwa kumwilisha hali hii katika ubunifu, ili kuwasaidia waamini kuendelea na safari ya imani bila kuyumbishwa na mateso, woga na taharuki ya ugonjwa wa Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kwa namna ya pekee kabisa ameguzwa na ari na moyo wa shughuli za kichungaji zilizotekelezwa na mapadre sehemu mbali mbali kwa kuendelea kuwa karibu zaidi na waamini wao katika uhalisia wa maisha yao, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Mungu anayefariji. Kwa bahati mbaya, kuna umati mkubwa wa Mapadre ambao wamepoteza maisha yao katika huduma kwa watu wa Mungu. Kwa neema na baraka ya Mungu, baadhi ya Mapadre waliweza kupona na leo wanaendelea kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kila mtu katika utekelezaji wa dhamana na wajibu wake, ametekeleza muujiza wa ajabu katika maisha ya watu wa Mungu nchini Italia. Jambo la msingi ni kuendelea kukuza na kudumisha imani, ili kuhitimisha vyema muujiza ulioanzishwa na Mwenyezi Mungu katika maisha

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wakleri wa Italia walionesha na kushuhudia ujasiri na upendo kwa watu wa Mungu nchini Italia. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wadau wote kwa kazi kubwa waliyotekeleza wakati wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Bikira Maria, anayeheshimiwa sana huko Kaskazini mwa Italia, awasindikize na kuwapatia hifadhi, ulinzi na tunza yake ya Kimama. Baba Mtakatifu anasema, ataendelea kuwakumbuka katika sala na sadaka yake, hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Papa: Lombardia
20 June 2020, 13:59