Tafuta

Vatican News
Papa: patriarca Bartolomeo sarà a Bari a incontro pace in Mo Papa: patriarca Bartolomeo sarà a Bari a incontro pace in Mo   (ANSA)

Barua ya Papa kwa Kard.Koch katika fursa ya miaka 25 ya Wosia wa Ut unum sint!

Papa Francisko ameandika Barua kwa Kardinali Kurt Koch Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo katika muktadha wa maadhimisho ya miaka 25,tangu kutangazwa kwa Wosia wa Kitume wa “Ut unum sint” kuhusu masuala ya umoja wa kikristo uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 25 Mei 1995.

Na  Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Papa Francisko ameandika Barua kwa Kardinali Kurt Koch Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo katika muktadha wa maadhimisho ya miaka 25, tangu kutangazwa kwa Wosia wa “Ut unum sint”. Katika ujumbe wake Papa amesema “ ni miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II aliweka sahihi katika Wosia wa Ut unum sint, katika matazamio wa Jubilei  ya miaka 2000 ambapo alikuwa anataka kuwa safari ya kuelekea Milenia ya tatu, Kanisa liweze kuzingatia sala ya Mwalimu wake na Bwana: “ili wote wawe na umoja”(Yh 17,21).  Kwa maana hiyo aliandika Wosia huo ambao unathibitisha kwa namna isiyobadilishwa ya jitihada za kiekumene katika Kanisa Katoliki.

Uwepo wa umoja wa wakristo wote, umetokana na neema ya Roho Mtakatifu

Papa Francisko anasema, Wosia huo ulitangazwa katika Siku kuu ya Kupaa kwa Bwana kwa kuukabidhi chini ya ishara ya Roho Mtakatifu ambaye ni kiongozi wa umoja katika tofauti na katika mantiki za kiliturujia na kiroho ambamo sisi sote tunafanya kumbu kumbu na kupendekeza kwa watu wote wa Mungu. Mtaguso wa Vatican II ulitambua kuwa mchakato wa uwepo wa umoja wa wakristo wote, umetokana na neema ya Roho Mtakatifu (Unitatis redintegratio, 1). Ulidhihirisha pia kwamba Roho wakati anatimiza utofauti wa neema na huduma, ni msingi wa umoja wa Kanisa (ibid., 2). Na Wosia wa Ut unum sint unathibitisha kuwa utofauti halali haupingani na umoja wa Kanisa, kwa upande wake unaongeza uzuri na unachangia sana kutimiza utume wake (n. 50). Kwa hakika ni Roho Mtakatifu tu anaweza kukuza tofauti na wingi na wakati huo huo kufanya kazi ndani ya umoja (…). Ni yeye anayeleta maelewano ya Kanisa kwa sababu, kama asemavyo Mtakatifu Bazil Mkuu, “ Yeye mwenyewe ni maelewano( Mahaubri katika Kanisa kuu la Roho Mtakatifu, Istanbul, 29 Novemba 2014). 

Hatua nyingi zimefanyika za kuponyesha majeraha kadhaa

Papa Francisko katika barua hiyo anamshukuru Bwana kwa ajili ya mchakato wa safari, ambayo imewezesha kutimiza kama wakristo katika kutafuta kwa ukamilifu muungano. Vile vile amebainisha juu ya kuunga  mkono kwa wale wanaofikiria kuwa inawezekana na inabidi kufanya jitihada zaidi. Licha ya hayo hatupaswi kukosa imani na utambuzi wa hatua nyingi ambazo zimefanyika kwa miaka kadhaa ya kuponya majeraha ya karne na milenia; kumekuwa na ongezeko la utambuzi na sifa za pamoja na zile za upendo pia na  aina mbali mbali za ushirikiano katika majadiliano ya maisha, juu ya mpango ya kichungaji na kiutamaduni.  Papa Francisko amekumbuka ndugu ambao ni viongozi wa Makanisa na jumuiya za kikristo. Hawa ni pamoja na kaka na dada wa kila tamaduni ya kikristo ambao ni wasindikizaji wenzetu katika safari. Kama mitume wa Emau tunaweza kuhisi uwepo wa Kristo Mfufuka ambaye anatembea karibu nasi na kutuelezea juu ya Maandiko na kuweza kumtambua wakati wa kumegwa mkate, kwa matarajio ya kushirikishana pamoja katika Meza ya Ekaristi.

Shukrani kwa Baraza kuendeleza uhai wa muungano wa Kanisa

Papa Francisko amerudia kutoa shukrani kubwa kwa wale ambao wamejikita katika Baraza hilo ili kuendeleza kutoa uhai katika Kanisa kwa utambuzi wa kile ambacho hakiwezi kuachwa hatma yake. Kwa namna ya pekee amepongeza hata kuanzishwa kwa mambo kadhaa. Awali ya yote kutunga mwongozo wa kiekumene kwa ajili ya Maaskofu ambao utatangazwa hivi karibuni kama kuwatia moyo na kuongoza zoezi la uwajibikaji wao wa kiekumene. Kwa hakika huduma hiyo amesema ni mantiki msingi wa utume wa Askofu, ambaye ni kioo  na msingi wa umoja katika Kanisa lake mahalia  (rej Lumen gentium, 23;  na CIC 383§3; CCEO 902-908). Pili ni katika kutoa gazeti la Acta Œcumenica, ambalo linapyaisha Huduma ya Mawasiliano ya Baraza, kwa kupendekeza kama miongozo  kwa wale ambao wanafanya kazi katika huduma ya umoja.

Ni muhimu kufanya kumbu kubu ya michakati ya safari

Katika njia inayotupelekea katika umoja kamili, Papa Francisko amesema ni muhimu kufanya kumbu kumbu ya michato ya safari, lakini zaidi ni kuangalia upeo  kwa kujiuliza maswali na wosia wa Ut unum sint:Quanta est nobis via?” (n. 77), yaani “yamebaki mangapi ya kufanya katika njia? Jambo moja ni hakika, kuwa umoja siyo msingi wa matokeo ya matendo yetu, bali ni zawadi ya Roho Mtakatifu. Hata hivyo mwishowe hayatakuja kwa miujiza, kwa maana umoja unakuja kupitia katika safari, ambayo anaifanya Roho Mtakatifu wakati wa  safari. (Mahubiri katika Masifu ya jioni, Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo 25 Januari  2014).   Kwa kuhitimisha barua yake, Papa Francisko anasema tuombe kwa imani Roho ili aongoze hatua zetu na kila mmoja ahisi kupyaishwa na wito wa nguvu wa kufanya kwa ajili ya uekumene; Yeye aongoze ishara mpya za kinabii na kuimarisha upendo kidugu kati ya wafuasi wote wa Kristo, ili ulimwengu upate kuamini. (Yh 17,21) na kuongezeka kwa sifa kwa Baba aliye mbinguni.

25 May 2020, 10:33