Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewatumia Ujumbe Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kama sehemu ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mwaka 2020 ambao umeahirishwa. Baba Mtakatifu Francisko amewatumia Ujumbe Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kama sehemu ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mwaka 2020 ambao umeahirishwa. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa

Baba Mtakatifu Francisko anakazia: Umuhimu wa utume wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; Mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji; karama na mapaji yanayopaswa kuendelezwa; ushauri wa kichungaji kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa na mwishoni, ni mchango wa mshikamano kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kimisionari sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa uliokuwa umepangwa kufanyika mjini Roma tarehe 21 Mei 2020 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbingu, umeahirishwa na badala yake, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, ujumbe maalum. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa utume wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; Mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji; karama na mapaji yanayopaswa kuendelezwa; ushauri wa kichungaji kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa na mwishoni, ni mchango wa mshikamano kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kimisionari sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anasema kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ni dhamana na utume wa Mama Kanisa unaokwenda kinyume kabisa cha wongofu wa shuruti unaoweza kutekelezwa kwa njia za: kisiasa, kitamaduni, kisaikolojia au kidini. Kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ni zawadi ya bure ambayo Roho Mtakatifu amelikirimia Kanisa lake na wala si matokeo ya nia au tafakari zinazofanywa na watu binafsi. Kupokea furaha inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu ni neema na nguvu ya pekee inayowawezesha waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa. Ikumbukwe kwamba, wokovu wa watu wa Mungu si matokeo ya juhudi za kimisionari au mahubiri kuhusu “Fumbo la Umwilisho”. Wokovu ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake kwa kukutana na ufunuo wa Uso wa Kristo Yesu, anayewaita waja wake, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa shukrani na furaha ya Injili. Kimsingi, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kama utume kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anafafanua mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika uinjilishaji mpya. Jambo la kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linakuwa na mvuto na mashiko yanayowahamasisha watu wa Mataifa kujiunga nalo na wala Kanisa haliwezi kukua na kuongezeka kwa wongofu wa shuruti. Watu wanapaswa kuguswa na chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Pili ni moyo wa shukrani na majitoleo pasi na kujibakiza hata kidogo, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa kwa njia ya unyenyekevu kwa kutambua kwamba, mafanikio yanayopatikana si kutokana na jasho au juhudi za wamisionari wenyewe. Mchakato wa uinjilishaji mpya hauna budi kurahisishwa na wala hakuna sababu ya kugumisha mambo na kuwakatisha watu tamaa. Kimsingi, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya unyenyekevu na wala hakuna sababu ya “kujimwambafai”.

Utume wa kweli unaotolewa na Mama Kanisa hauwezi hata kidogo kuwatwisha watu mzigo wala kuwapatia majiundo makali, mambo ambayo Kristo Yesu anaweza kuwakirimia waja wake kwa urahisi sana, kama “uji kwa mgonjwa”. Mihimili ya uinjilishaji inapaswa kuwa karibu zaidi na watu wanaoinjilishwa, kadiri ya hali na mazingira yao pamoja na kuzingatia ufahamu wa watu wa Mungu “Sensus fidei” pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja ya kukuza na kudumisha karama zinazoweza kuboresha ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa wabatizwa. Hiki ndicho kile kinachoitwa “Sensum fidei” yaani “Ufahamu ya waamini” unaofumbatwa katika msingi wa sala na matendo ya huruma. Katika muktadha huu, waamini walei wamekuwa wakiheshimiwa sana na Mama Kanisa, kwa kutambua mchango na ushiriki wao wa kawaida katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Huu ni mtandao unaopaswa kukuzwa na kudumishwa ili kuonesha utajiri unaobubujika kutoka kwa watu wenye mawazo na mitazo tofauti.

Baba Mtakatifu anayataka Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuondokana na dhana ya kutaka kujitafuta yenyewe, kwa ajili ya kujiendeleza, hali ambayo inaweza kufananishwa na watu “wanaotaka kujipigia debe ili kukuza shughuli zao kwa mafao yao binafsi”. Viongozi wa Mashirika haya waondokane na uchu wa madaraka kwa kutaka kuamrisha kila jambo, bali watambue kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya watu wa Mungu na wala si vinginevyo! Ubaguzi na tabia ya kuwatenga watu kwa misingi ya matabaka yao, ni jambo ambalo linapaswa “kufyekelewa mbali” katika maisha na utume wa Kanisa. Viongozi wasitafute vigezo vya ufanisi wa mambo ya kidunia. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii, kuyashauri Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuhakikisha kwamba, kwa mara nyingine tena yanagundua na kulinda ufahamu wa waamini, kwa kuzama katika maisha ya watu wa Mungu, ili kujenga na kudumisha mtandao wa upendo na mshikamano katika ngazi mbali mbali kuanzia kwa kuwaunganisha wanachama wa vyama na mashirika mbali mbali ya kazi za kitume.

Mashirika haya yawe mstari wa mbele katika sala sanjari na kukusanya fedha kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii ni huduma muhimu kwa ajili ya utume wa Makanisa mahalia, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari. Kuna haja ya kurahisisha miundombinu ya utume huu. Baba Mtakatifu anasema, ni marufuku kwa viongozi kuyageuza Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuwa kama asasi za kujitegemea, kwa kujikita katika mchakato wa ukusanyaji wa fedha. Viongozi waondokane na kishawishi cha kutafuta wachangiaji “wazito na wenye mshiko mkubwa zaidi”. Dhamana na wajibu wa kuchangia shughuli mbali mbali za kimisionari iko mikononi mwa wabatizwa wote. Mchango unaotolewa na Makanisa yote, Mwezi Oktoba wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Duniani unapaswa kuimarishwa zaidi. Fedha inayokusanywa, isaidie kugharimia mahitaji msingi ya Kanisa mahalia na kuondokana na mtindo wa kutaka kuligeuza Kanisa kuwa kama “chombo cha kuwanyonya watu”. Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni mtandao wenye sura na tamaduni nyingi, changamoto na mwaliko ni kuhakikisha kwamba, imani ya Wakristo inashuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni vyombo vya Injili ya huruma na upendo inayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake, kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa kuyataka kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake kwa kutambua kwamba, yanapaswa kumtegemea Mwenyezi Mungu!

Papa Ujumbe kwa PMS 2020

 

21 May 2020, 13:57