Tafuta

Katika Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Kristo, Kanisa pia linaadhimisha Siku ya Kuombea Kanisa Katoliki nchini China, siku ambayo ilianzishwa na Papa Mstaafu Benedikto XVI mwaka 2007. Katika Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Kristo, Kanisa pia linaadhimisha Siku ya Kuombea Kanisa Katoliki nchini China, siku ambayo ilianzishwa na Papa Mstaafu Benedikto XVI mwaka 2007. 

Siku ya Sala ya Kuombea Kanisa Katoliki China: Tarehe 24 Mei

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2007 akatangaza tarehe 24 Mei ya kila Mwaka kuwa ni Siku ya Kuombea China. Hii ni siku ambayo China pia inaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria wa Sheshan. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipenda kukazia: Hali ya Kanisa Katoliki nchini China Katika Mwono wa Kitaalimungu. Pili, ni Mwelekeo wa Shughuli za Kichungaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku kuu ya Bikira Maria msaada wa Wakristo inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei, ilianzishwa na Papa Pio wa VII kunako mwaka 1815. Huu ulikuwa ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha mbele ya Bikira Maria msaada wa Wakristo, ili awasaidie kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kunako mwaka 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Bikira Maria, Msaada wa Wakristo kuwa ni Mama na msimamizi wa Familia ya Mungu nchini China. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2007 akatangaza tarehe 24 Mei ya kila Mwaka kuwa ni Siku ya Kuombea China. Tangu wakati huo, Kanisa zima linakimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa ajili ya familia ya Mungu nchini China; siku ambayo China pia inaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria wa Sheshan.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika barua yake Kwa Wakatoliki Nchini China aliyoichapisha tarehe 27 Mei 2007 alipenda kukazia mambo makuu mawili: Hali ya Kanisa Katoliki nchini China Katika Mwono wa Kitaalimungu. Pili, ni Mwelekeo wa Shughuli za Kichungaji. Katika barua hii, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anaangalia kwa kina na mapana kuhusu utandawazi, mamboleo na ukanimungu. Anakazia umuhimu wa majadiliano katika ukweli na kuheshimiana; msamaha na upatanisho. Anaangalia uhusiano kati ya Kanisa na Serikali unaopaswa kujengeka katika misingi ya ukweli na upendo. Anapembua pia hali ya Maaskofu Katoliki China sanjari na uteuzi wao. Hali ya Kanisa Katoliki katika mtazamo wa shughuli za kichungaji, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anapembua kuhusu maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; Uongozi wa Kanisa katika Majimbo na Parokia; Wakleri, Jumuiya za Wakatoliki; Wito na Malezi; Ukatekumeni, Waamini walei na familia na mwishoni anaangalia wito wa kimisionari.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, tarehe 24 Mei, Siku ya Kuombea Kanisa Nchini China, iwe ni: Siku ya sala na muda wa kupyaisha imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake sanjari na kuonesha uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni siku ya kuombea umoja na mshikamano unaoonekana kwa kujikita katika Amri kuu ya upendo. Amri ya upendo kwa Mwenyezi Mungu na jirani ni muhtasari wa mafundisho makuu yaliyotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kuhakikisha kwamba, upendo huu unamwilishwa katika uhalisia wa maisha na kamwe usibaki unaelea katika ombwe! Huu ni upendo na sala kwa ajili ya kuwaombea adui zao. Ni siku ya kuombea umoja, upendo na mshikamano wa dhati ili hatimaye, kuendelea kudumu katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili hata katika mateso, dhuluma na nyanyaso.

Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, amekuwa na jicho la pekee kwa familia ya Mungu nchini China. Daima amependa kuonesha uwepo wake wa kibaba katika furaha, mateso na magumu mbali mbali wanayokabiliana nayo huku akiwataka wadumu katika imani, matumaini na mapendo. Daima wawe wepesi kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Msaada wa Wakristo. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa maboresho ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Serikali ya China. Mkazo ni ushirikiano kati ya Vatican na China kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya pande hizi mbili. Askofu Giuseppe Guo Jincai na Askofu Giovanni Battista Yang Xiaoting, kwa ruhusa ya Serikali ya China, waliweza kuhudhuria na kushiriki Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iliyoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba 2018.

Kumekuwepo pia uteuzi wa Maaskofu mahalia uliofanya na Vatican. Katika mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, Vatican na Serikali ya China vimeshirikiana kwa karibu sana, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo. Kuna umati mkubwa wa waamini umeshiriki katika Ibada za Misa Takatifu zilizokuwa zinarushwa mubashara kutoka katika Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Hivi karibuni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Gazeti la “Global Times” linalochapishwa kila siku nchini China, amegusia kuhusu matunda ya makubaliano ya mpito kati ya Vatican na Serikali ya China kuhusu dhamana na wajibu wa uteuzi wa Maaskofu Katoliki nchini China; Utamadunisho; ushirikiano kati ya nchi hizi mbili; nafasi na dhamana ya viongozi wa kisiasa pamoja na ujumbe kwa familia ya Mungu nchini China!

Itakumbukwa kwamba, tarehe 22 Septemba 2018 Vatican na China vilitiliana sahihi makubaliano ya mpito kuhusu dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuteuwa Maaskofu Katoliki, makubaliano haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini China. Haya ni matunda ya majadiliano, maridhiano na uvumilivu, ili kuganga na kuponya madonda ya kinzani na kutoelewana kati ya nchini hizi mbili. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili familia ya Mungu nchini China iweze: kuamini, kutumaini na kupenda na hatimaye, kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao! Kardinali Parolin anakiri kwamba, kuna baadhi ya waamini na viongozi wa Kanisa nchini China wamekwaza na makubaliano haya ya mpito, lakini hii ni sehemu ya ukweli wa kibinadamu unaofumbatwa pia katika tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Hii ni sehemu ya mchakato wa majadiliano yanayolenga kwenye maboresho ya shughuli za kichungaji nchini China; kwa kuheshimu na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa katika mapokeo ya China! Matunda na makubaliano haya ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa majadiliano: kwa kusikilizana, ili hatimaye, kupata suluhu ya kudumu katika changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza ili hatimaye, kujenga mshikamano wa udugu wa binadamu. Waamini wa Kanisa Katoliki nchini China wanaomba ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Kardinali Parolin anakaza kusema, Utamadunisho wa Injili ni mbereko ya uinjilishaji na ushuhuda wa imani katika matendo. Mchakato huu nchini China ulianzishwa na Padre Matteo Ricci, ili kuwawezesha Wachina kuendelea kubaki Wachina, kwa kukita maisha yao katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Hii ni sehemu pia ya majadiliano ya kitamaduni. Wakatoliki nchini China ndio walengwa wakuu wanaopaswa kujisadaka bila ya kujibakiza, katika upatanisho wa kweli, ili waweze kuwa Wachina pasi na hila na Wakatoliki kweli kweli.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Vatican na China zinaweza kushirikiana zaidi katika: kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi; mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi; huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; kanuni maadili na utu wema katika tafiti na masuala ya kisayansi, bila kusahau uchumi fungamani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini China. Mambo muhimu ya kuzingatia ni: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kardinali Parolin anawakumbusha viongozi wa kisiasa na kijamii kwamba, uongozi kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ni huduma ya upendo hasa kwa maskini. Wawe ni watu wa imani na matumaini, wanaojitahidi kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa kibinadamu. Siasa iwe ni chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Kumbe, wanasiasa wanapaswa kuwajibika barabara katika maamuzi na shughuli zao za kila siku! Kardinali Parolin ana mshukuru Mungu kwa kumwezesha kupata uzoefu na mang’amuzi makubwa katika mchakato wa majadiliano kati ya Vatican na Serikali ya China. Utashi wa kisiasa, uvumilivu na hali ya kuheshimiana ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya Vatican na China. Ni fursa ya kufahamiana na kukuza yale mambo msingi yanayowaunganisha, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Anatambua mateso na mahangaiko ya Wakristo wengi nchini China, lakini hawa ni watu wenye matumaini makubwa! Kardinali Pietro Parolin, anasema, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini China ni huu: Wawe ni vyombo na wajenzi wa umoja na upatanisho; ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Waendelee kujikita katika mchakato wa utamadunisho pamoja na kuwekeza tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kimaadili kwa vijana wa kizazi kipya! China na Vatican ziendeleze mchakato wa majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Lengo ni kushinda kishawishi cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Watu wawe ni wajenzi wa amani, umoja na udugu wa kibinadamu!

Siku ya Kuombea China
23 May 2020, 14:13