Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 14 Mei 2020 ni Siku Maalum kwa Waamini wa Dini Zote: Kusali, Kufunga na Kufanya Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Papa Francisko tarehe 14 Mei 2020 ni Siku Maalum kwa Waamini wa Dini Zote: Kusali, Kufunga na Kufanya Matendo ya huruma: kiroho na kimwili.  (Vatican Media)

Tarehe 14 Mei 2020 ni Siku ya Sala, Kufunga na Matendo ya Huruma

Baba Mtakatifu Francisko amepokea na kuridhia Mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, ili kwamba, hapo tarehe 14 Mei 2020 waamini wa dini na madhehebu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waweze kuunganika na kushikamana kwa njia ya sala, kufunga na kutenda matendo ya huruma ili kukimbilia huruma na mapendo ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari ya Sala ya Malkia wa Mbingu amewakumbusha waamini kwamba, ni muda mfupi tu umekwisha kuyoyoma tangu Mwezi Mei ulipoanza. Kadiri ya Mapokeo ya Kanisa huu ni Mwezi uliotengwa kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Hiki ni kipindi ambacho waamini wengi wanapenda kutembelea Madhabahu yaliyowekwa wakfu kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria. Lakini kwa mwaka 2020 kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 haiwezekani kutembelea Madhabahu haya. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutembelea Madhabahu haya ya imani na ibada kwa Bikira Maria, ili kumpelekea Bikira Maria wasi wasi, hofu na mashaka; matamanio halali pamoja na matarajio kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sala ina umuhimu wake wa pekee katika maisha ya waamini ndiyo maana amepokea na kuridhia Mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, ili kwamba, hapo tarehe 14 Mei 2020 waamini wa dini na madhehebu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waweze kuunganika na kushikamana kwa njia ya sala hapo tarehe 14 Mei 2020, ili kusali, kufunga na kutenda matendo ya huruma kama njia ya kumwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aweze kuwasaidia binadamu kuvuka Janga hili la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Katika kipindi hiki cha Janga kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kiasi cha kuzua taharuki, hofu na wasi wasi kubwa miongoni mwa watu wa Mungu, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia waamini wote Barua kwa ajili ya Mwezi Mei, 2020 ambao kadiri ya Mapokeo ya Kanisa umetengwa maalum kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, Mwezi Mei, waamini kwa namna ya pekee kabisa wanaonesha upendo na ibada yao kwa Bikira Maria. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Kipindi hiki cha Mwezi Mei waamini wamejenga utamaduni wa kusali Rozari Takatifu katika familia zao. Huu ni wakati muafaka wa kukazia dhana ya familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limewalazimisha hata waamini kuimarisha zaidi tunu msingi za maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu Francisko anasema ni katika muktadha huu, ameona kwamba ni jambo jema sana, kwa waamini kugundua tena uzuri na umuhimu wa kusali Rozari Takatifu majumbani mwao wakati wa Mwezi Mei, 2020. Anawaalika waamini kusali Rozari kama mtu binafsi au kama familia kadiri ya hali na mazingira ya watu husika. Mapendekezo yote mawili yanaweza kutumiwa kwa kusoma alama za nyakati. Baba Mtakatifu anasema, siri kubwa ni urahisi wa kuweza kupata utaratibu mzuri wa kuweza kufuata na kusali Rozari Takatifu. Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema Sala mbili kwa Bikira Maria, ambazo hata yeye mwenyewe atazitumia wakati wa kusali Rozari Takatifu, Mwezi Mei 2020, akiwa ameungana moja kwa moja kiroho na waamini wote.

Sala hizi zimeambatanishwa kwenye Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Waamini Wote Kipindi cha Mwezi Mei, 2020, ili ziweze kuwekwa hadharani kwa ajili ya matumizi ya watu wote wa Mungu! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa pamoja Uso wa Kristo, wakiwa wamehifadhiwa kwenye Moyo Mtakatifu wa Bikira Maria, Mama wa Kanisa, anayewawezesha kuungana kwa pamoja kiroho kama familia na atawasaidia kuvuka salama katika majaribu haya mazito yanayomwandama mwanadamu kwa wakati huu. Baba Mtakatifu anasema, atawakumbuka na kuwaombea na kwa namna ya pekee kabisa, anawakumbuka wale wote wanaoteseka! Anawaalika hata wao pia kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwishoni, anawashukuru waamini wote na kuwapatia baraka zake za Kitume!

IBADA YA ROZARI TAKATIFU: Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Mwezi Mei ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, silaha za pambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo ni: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti ya Upatanisho pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ibada ya Rozari Takatifu wakati huu ambapo watu wengi wako majumbani mwao ni muhimu sana, ili kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano katika maisha ya kiroho kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani. Ifuatayo ni Sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Bikira Maria katika Kipindi cha Mwezi Mei, 2020 Uliotengwa Maalum kwa ajili ya Ibada ya Rozari Takatifu.

“Tunakimbilia ulinzi wako, Mama Mtakatifu wa Mungu, katika hali tete na majonzi ambayo yameugubika ulimwengu mzima, tunakimbilia kwako Mama wa Mungu na Mama yetu, tunatafuta usalama chini ya ulinzi wako. Ee Bikira Maria, utuangalie kwa macho yako yenye huruma katika Janga hili la Virusi vya Corona, na uwafariji wale wanaohuzunika na kuomboleza kutokana na vifo vya ndugu zao; waliozikwa hata wakati mwingine katika mazingira yanayo uchoma moyo. Wahurumie wale wote wanaoteseka kwa ajili ya wagonjwa, ili kuzuia maambukizi hawawezi kuwa nao karibu. Wajalie imani watu wenye hofu kwa kutokuwa na uhakika wa maisha yao kwa siku za mbeleni kutokana na athari za kiuchumi na kazi.

Mama wa Mungu na Mama Yetu, tuombee kwa Mwenyezi Mungu, Baba wa huruma, ili kwamba, majaribu haya mazito yaweze kufikia ukomo na kuanza kurejea tena upeo wa matumaini na imani. Kama ilivyokuwa kwenye Harusi ya Kana ya Galilaya, ingilia kati na uwaombee mbele ya Mwana wa Mungu, ili aweze kuzifariji familia zenye wagonjwa na waathirika; afungue nyoyo zao ili ziweze kuwa na imani. Walinde madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea ambao katika Janga hili wamekuwa mstari wa mbele, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao, ili kuokoa maisha ya wengine. Wasindikize katika mahangaiko yao ya kishupavu; wajalie nguvu, wema na afya.

Uwe pembeni mwa wale wote ambao usiku na mchana wanawasaidia wagonjwa, na mapadre wakisukumwa na ari ya kichungaji na utume wa Kiinjili, wanajitahidi kuwasaidia na kuwahudumia wote. Bikira Maria angaza akili za wanasayansi, ili waweze kupata suluhu ili kushinda Virusi hivi. Wasaidie Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, ili waweze kutenda kwa hekima, huruma na ukarimu, kwa kuwasaidia wale wote wanaokosa mahitaji msingi ya maisha; kwa kuandaa programu zitakazotoa suluhu za kijamii na kiuchumi kwa kuwa na malengo ya muda mrefu wakiwa na moyo wa mshikamano.

Bikira Maria Mtakatifu, gusa dhamiri za watu ili kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika kutengeneza na kuboresha silaha za maangamizi, badala yake, fedha hii, itumike katika tafiti muhimu ili kuzuia majanga kama haya kwa siku za usoni. Bikira Maria Mama mpendelevu, saidia kukuza ulimwenguni utambuzi kwamba, watu wote wanaunda familia kubwa ya binadamu; ili kwamba, wote wakiwa wameunganishwa na mshikamano na udugu waweze kusaidia kupambana na umaskini na hali mbaya ya maisha ya mwanadamu. Waimarishe waamini katika imani, daima wakidumu katika sala na huduma. Bikira Maria Faraja ya wanaoteseka, wakumbatie wanao wote wanaoteseka, waombee kwa Mwenyezi Mungu ili kwa mkono wake wenye nguvu aweze kuwaokoa watu wake kutoka katika Janga hili, ili hatimaye, maisha yaweze kuanza tena katika hali ya kawaida na utulivu. Tunakutumainia, ili katika safari yetu uwe ni alama ya wokovu na matumaini, Ee mpole, Ee mwema Ee mpendevu, Bikira Maria. Amina.

IFUATAYO NI SALA YA PILI KUTOKA KWA Baba Mtakatifu Francisko kama kiambatanishi cha Barua yake kwa Waamini Wote kwa ajili ya Mwezi Mei, 2020 ambao kadiri ya Mapokeo ya Kanisa umetengwa maalum kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. “Bikira Maria unang’aa daima katika njia yetu kama alama ya wokovu na matumaini. Sisi tunakutumainia Wewe, Afya ya wagonjwa, ambaye chini ya Msalaba ulishiriki mateso ya Yesu, ukabaki thabiti katika imani yako. Wewe ambaye ni wokovu wa Warumi, unatambua ni kitu gani ambacho tunakihitaji kwa wakati huu na tuna matumaini kwamba, utaweza kutuombea, kama ilivyokuwa kwenye Harusi ya Kana ya Galilaya, furaha iweze kurejea tena baada ya kipindi hiki cha majaribu makubwa. Utusaidie Bikira Maria wa Upendo wa Mungu, utuimarishe katika kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa kufanya kile ambacho Yesu atasema, kwani amejitwika mateso na kuchukua machungu yetu na kutuongoza, ili kwa njia ya Msalaba, tuweze kufikia furaha ya Ufufuko. Amina. Tunakimbilia ulinzi wako mzazi Mtakatifu wa Mungu. Usitunyime tukiomba katika shida zetu, tuopoe siku zote kila tuingiapo hatarini, Ee Bikira Mtukufu na mwenye baraka. Amina.

Papa: Mwezi wa Rozari Takatifu
03 May 2020, 13:48