Tafuta

Umoja wa Ulaya unaadhimisha Kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman lilipotolewa tarehe 9 Mei 1950! Mwanzo wa dhana ya Umoja wa Ulaya. Umoja wa Ulaya unaadhimisha Kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman lilipotolewa tarehe 9 Mei 1950! Mwanzo wa dhana ya Umoja wa Ulaya. 

Miaka 70 ya Tamko la Schuman: Amani, umoja na maendeleo!

Kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman, Waziri Mkuu wa Ufaransa lilipotolewa kunako tarehe 9 Mei 1950 na hilo likawa ni chimbuko la Umoja wa Ulaya, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, iliyokuwa imehitimishwa miaka mitano iliyokuwa imetangulia. Ni Tamko lililopania kuhakikisha kwamba, hakutakuwepo tena na vita kwa siku za usoni huko Barani Ulaya. Amani na Ustawi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Ulaya tarehe 9 Mei 2020 imeadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman, Waziri Mkuu wa Ufaransa lilipotolewa kunako tarehe 9 Mei 1950 na hilo likawa ni chimbuko la Umoja wa Ulaya, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, iliyokuwa imehitimishwa miaka mitano iliyokuwa imetangulia. Ni Tamko lililopania kuhakikisha kwamba, hakutakuwepo tena na vita kwa siku za usoni huko Barani Ulaya. Ufaransa na Ujerumani, waliokuwa hawawezi kupikika chungu kimoja, wakaunganishwa kwa pamoja, ili kuunganisha nguvu za kiuchumi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Ulaya.

Amani Duniani itaweza kulindwa na kudumishwa kwa kujikita katika umoja na mshikamano, kwa kukusanya nguvu na rasilimali kwa ajili ya kupambana na mambo yale ambayo yanatishia: utulivu, amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Kama kutatokea umuhimu wa kuingia vitani, basi Umoja wa Ulaya katika ujumla wake, ushikamane na kupambana na adui atakayekuwa amejitokeza. Kumbe, hapa jambo la msingi ni umoja na mshikamano miongoni mwa Umoja wa Ulaya. Matumizi ya pamoja ya rasilimali za Bara la Ulaya, yatasaidia mchakato wa kulinda na kudumisha amani; maendeleo fungamani ya binadamu na ustawi wa wengi.

Tamko linatambua umuhimu wa amani kama msingi wa maendeleo fungamani ya binadamu na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kati ya watu wa Mataifa ambao kwa miaka mingi walikuwa wanakinzana na kupigana ovyo! Msingi wa Umoja wa Ulaya pamoja na mambo mengine, ulipania kukuza na kudumisha amani duniani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mambo yote haya yalihitaji rasilimali na mtaji kwa ajili ya utekelezaji wake, mwanzo wa kuwa na Benki ya Umoja wa Ulaya itakayosimamia na kuratibu kodi, ili hatimaye, kukoleza mchakato wa uzalishaji mali na huduma; mambo yanayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu, ili kuongeza tija katika uzalishaji na huduma. Pale ambapo kutajitokeza hali ya kutoelewana miongoni mwa Nchi wanachama basi, awepo kiongozi atakayesaidia kutoa suluhu ya amani. Umoja wa Ulaya utaendeleza pia ushirikiano na mshikamano na Umoja wa Mataifa kwa kuwa na mwakilishi ambaye atatoa taarifa mara mbili kwa mwaka kuhusu jitihada za Umoja wa Ulaya za kukuza na kudumisha amani, ustawi na maendeleo ya wananchi wake.

Hii ndiyo misingi inayoufanya Umoja wa Ulaya tarehe 9 Mei 2020 kuadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Robert Schuman, Waziri Mkuu wa Ufaransa kwa wakati huo! Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wa Pasaka “Urbi et Orbi” kwa mwaka 2020 ameikumbusha Jumuiya ya Ulaya kwamba, nchi nyingi ziliweza kusimama tena baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kutokana na mshikamano uliowasaidia kuvuka kinzani na misigano ya zamani. Umoja na mshikamano uwe ni utambulisho wa watu wa Mungu Barani Ulaya, kwa kusaidiana kwa hali na mali. Hii ni changamoto changamani kwa Jumuiya ya Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake. Huu ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha mshikamano kwa kujikita hata katika suluhu mpya. Watu wasilogwe kwa kutaka kuyakumbatia yaliyopita, kwa sababu mwelekeo wa namna hii unaweza kuhatarisha amani, mafungamano ya kijamii pamoja na maendeleo fungamani kwa vizazi vijavyo! Huu si muda wa kuendekeza kinzani na migawanyiko, bali kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anasema si wakati hata kidogo wa kuendelea kutengeneza, kulimbikiza na kutumia silaha na badala yake, rasilimali fedha hii, itumike kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu.

Miaka 70 ya Tamko la Robert Schuman

 

 

 

 

09 May 2020, 13:29