Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II ametuma Ujumbe kwa Vijana wa Kizazi Kipya nchini Poland. Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II ametuma Ujumbe kwa Vijana wa Kizazi Kipya nchini Poland.  (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 100: Kuzaliwa kwa Mt. Yohane Paulo II: Vijana!

Papa Francisko katika ujumbe wake kwa vijana nchini Poland anagusia: historia fupi ya maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II; Ibada kwa Huruma ya Mungu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na mwishoni anawataka vijana kuthubutu kujiachia mikononi mwa Mungu ili aweze kuwatumia kadiri ya mapenzi yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Poland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo wa II, alikuwa na karama ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, kwani hawa kwake walikuwa ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Huu ni utume ambao unaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Majadiliano kati ya Mtakatifu Yohane Paulo II na vijana wa kizazi kipya, waliompenda upeo, ni ushuhuda unaojionesha hadi wakati huu kutokana na maadhimisho ya Siku za vijana kitaifa na kimataifa. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, hapo tarehe 18 Mei 2020, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe kwa njia ya video, vijana wote wa Poland.

Ujumbe huu, umerushwa mubashara na Kituo cha Televisheni cha Taifa “Televizia Poska” “Telewizja Polska Program 1” Majira ya saa 2:00 za Usiku kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa vijana nchini Poland anagusia: historia fupi ya maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II; Ibada kwa Huruma ya Mungu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na mwishoni anawataka vijana kuthubutu kujiachia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwatumia kadiri ya mapenzi yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Poland. Baba Mtakatifu anasema, bado anayo kumbukumbu hai ya maadhimisho ya hija yake ya kumi na tano ya kitume nchini Poland, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, iliyoongozwa na kauli mbiu “heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Maadhimisho haya yalitimua vumbi kuanzia tarehe 26  – 31 Julai 2016.

Mtakatifu Yohane Paulo II amekuwa ni zawadi ya pekee kabisa kwa Kanisa na Poland katika ujumla wake. Alianza hija yake ya maisha ya hapa duniani tarehe 18 Mei 1920 huko Wavowice, akaendeleza sehemu ya maisha yake mjini Roma kwa muda wa miaka 15. Tangu awali ni kiongozi aliyejipambanua kuwa ni mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; aliguswa kwa namna ya pekee na Fumbo la Mungu, Kazi ya Uumbaji na Utakatifu wa maisha ya mwanadamu. Ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu. Adhimisho la Jumapili ya huruma ya Mungu, linapata chimbuko lake wakati wa adhimisho la Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Huruma ya Mungu inakita mizizi yake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa.

Mtakatifu Yohane Paulo II kwa mwanga wa upendo wa Mungu wenye huruma, alipata mang’amuzi ya pekee kuhusu uzuri na utakatifu wa wito wa watu wa Mungu; akatambua umuhimu wa watoto katika jamii, vijana sanjari na watu wazima. Aliangalia muktadha wa hali za kitamaduni na kijamii. Haya ni mambo ambayo kila mtu aliweza kuyafanyia majaribio na hata vijana wa kizazi kipya wanaweza kuyafanyia mang’amuzi anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa sasa wanafahamu historia ya maisha sanjari na mafundisho yake msingi ambayo yanaweza kupatikana kwa njia ya internet. Kila kijana anachukua ndani mwake chapa ya tunu msingi za familia yake, hii ndiyo tabia ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Mafundisho yake ni msingi thabiti na rejea yenye uhakika inayoweza kumsaidia kijana kupata suluhu halisi ya matatizo na changamoto mbali mbali za maisha ambayo familia mbali mbali zinakumbana nayo katika ulimwengu mamboleo. Lakini, ikumbukwe kwamba, matatizo binafsi na yale ya kifamilia si kizingiti katika mchakato wa utakatifu wa maisha na furaha ya kweli. Matatizo na changamoto hizi, kamwe hazikuwa ni kikwazo kwa kijana Karol Wojtyla, ambaye tangu mwanzo wa ujana wake, aliwapoteza wazazi na kaka yake mpendwa. Akiwa mwanafunzi, akaonja mateso ya utawala wa kinazi, “uliofyekelea” mbali marafiki zake. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kama Padre na Askofu, ilimbidi kusimama kidete kupambana na ukomunisti, usiomwamini Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba,  changamoto na matatizo hata kama yakiwa ni magumu kiasi gani, ni sehemu ya majaribu ya ukomavu wa imani na yanaweza kupatiwa ufumbuzi wake, ikiwa kama yatasimikwa kwenye nguvu ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hii ni kumbu kumbu endelevu kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye katika Wosia wake wa kwanza wa Kitume “Redemptor Hominis” yaani “Mkombozi pekee wa Binadamu” anasema, ikiwa kama mwanadamu anataka kujifahamu vyema zaidi lazima atambue pia mahangaiko yake ya ndani, wasi wasi, udhaifu na dhambi zinazomwandama katika maisha; kwa njia ya maisha na kifo ili kumkaribia zaidi Kristo Yesu. Mwamini anapaswa kumwendea na kumwingia Kristo Yesu “mzima mzima”.

Haya ndiyo matamanio ya Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana wa kizazi kipya ili wahakikishe kwamba, wanamwendea Kristo Yesu, wazima wazima bila ya kujibakiza hata kidogo. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, yawe ni kikolezo kwa vijana kuweza kusimama na kutembea kwa ujasiri, huku wakiwa wameungana na Kristo Yesu, ambaye ni “Bwana anayethubutu na ni Bwana anayekwenda mbele zaidi”. Kama ilivyokuwa wakati wa Sherehe ya Pentekoste, Kristo Yesu anataka kutekeleza muujiza mkubwa ambao wanaweza hata wao kuufanyia mang’amuzi: Mwenyezi Mungu anataka kutumia mikono yao inayogeuzwa kuwa ni alama upatanisho, umoja na mwendelezo wa kazi ya uumbaji. Mwenyezi Mungu anaitaka mikono ya vijana wa kizazi kipya ili aendeleze kazi ya uumbaji wa ulimwengu mamboleo. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka vijana wote wa Poland nchini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yohane Paulo II na hatimaye, akawapatia baraka zake za Kitume!

Papa: Vijana Poland

 

 

19 May 2020, 13:19